Tom Saintfiet alilia penalti kwa Morocco
Muktasari:
- Mechi hiyo ya Kundi B iliyochezwa mjini Rabat uliona timu zote mbili zikipata penalti, lakini Saintfiet anaamini uamuzi wa marefa uliwapendelea wenyeji wa michuano kwa kuinyima Mali penalti ya pili muhimu.
KOCHA mkuu wa Mali, Tom Saintfiet amekosoa uamuzi wa marefa walioichezesha timu hiyo dhidi ya wenyeji Morocco na kutoka nao sare ya bao 1-1, katika mechi ya raundi ya pili ya hatua ya makundi ya AFCON 2025.
Mechi hiyo ya Kundi B iliyochezwa mjini Rabat uliona timu zote mbili zikipata penalti, lakini Saintfiet anaamini uamuzi wa marefa uliwapendelea wenyeji wa michuano kwa kuinyima Mali penalti ya pili muhimu.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji aliyewahi kuinoa Yanga iliyopo Ligi Kuu Bara, alipinga penalti iliyotolewa kwa Morocco kwa kosa la mpira wa mkono, huku akisisitiza Mali ilinyimwa penalti nyingine baada ya kile alichokitaja kuwa mpira wa mkono wa wazi uliofanywa na beki wa Morocco, Nayef Aguerd.
“Niliona tukio hilo tena kupitia televisheni,” amesema Saintfiet na kuongeza; “Mlinzi aligusa mpira kwa mkono waziwazi. Inasikitisha kwamba hatukupewa penalti hiyo.”
Ingawa alikiri ugumu wa kazi ya waamuzi, kocha huyo wa Mali alielekeza lawama kwa maamuzi ya refa wa Cameroon,Abdou Abdel Mefire ambaye ndiye refa mdogo kucheza fainali hizo za Afcon akiwa na umri wa miaka 29, akisema yalikuwa sababu kuu ya matokeo ya mechi hiyo.
Licha ya kukerwa kwake, Saintfiet aliwasifu wachezaji wa Mali kwa kiwango walichoonyesha, hasa baada ya kupata sare ya pili mfululizo katika mashindano hayo ya 35 tangu yalipoasisiwa mwaka 1957.
“Ninafurahia uchezaji wa timu yangu, lakini sijaridhika kabisa na matokeo. Kama kocha, nataka kushinda kila mechi,” amesema Tom na kuongeza, Mali waliingia kwenye mashindano wakiwa na malengo wazi, yakiwemo kumaliza juu ya kundi, lengo ambalo sasa limekuwa gumu zaidi baada ya kushindwa kuifunga Zambia katika raundi iliyopita.
Akizungumza kuhusu mechi za mwisho za kundi, Saintfiet alikiri kuwa hatma ya Mali inaweza kutegemea matokeo ya timu nyingine.
“Natumaini Zambia watajitahidi kupata angalau pointi dhidi ya Morocco,” amesema.
“Sisi pia tutatoa kila kitu kushinda mechi yetu. Kumaliza kileleni mwa kundi kutaturahisishia mambo baadaye.”