Man City yakomaa kwa Ayyoub Bouaddi
Muktasari:
- Dau hilo linaweza kupungua endapo klabu itakayomnunua itakubali kumwacha Bouaddi aendelee kuichezea Lille kwa mkopo kwa msimu mmoja zaidi au kufikia makubaliano ya awali ya uhamisho yatakayotekelezwa baadaye.
Manchester City imeongeza juhudi za kumwania kiungo chipukizi wa Lille, Ayyoub Bouaddi, kufuatia kiwango alichoonyesha katika msimu uliopita na Kombe la Dunia, kwa mujibu wa taarifa za talkSPORT.
Hata hivyo klabu yake ya Lille inaendelea kumthaminisha nyota huyo wa kimataifa wa Morocco kwa ada inayokadiriwa kufikia euro100 milioni ikiwa klabu yoyote itataka kumsajili mara moja.
Dau hilo linaweza kupungua endapo klabu itakayomnunua itakubali kumwacha Bouaddi aendelee kuichezea Lille kwa mkopo kwa msimu mmoja zaidi au kufikia makubaliano ya awali ya uhamisho yatakayotekelezwa baadaye.
Baada ya Kombe la Dunia kumalizika, Bouaddi anatarajiwa kukutana na rais wa Lille, Olivier Letang, kujadili mustakabali wake.
Katika Kombe la Dunia alisaidia Morocco kumaliza katika robo fainali.
Gbemi Arubi
Klabu ya Burton Albion imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Dundalk, Gbemi Arubi, kwa mkataba wa miaka mitatu huku ikiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi. Klabu hiyo haijaweka wazi kiasi cha fedha kilichotumika kumsajili mshambuliaji huyo mwenye miaka 22, ambaye ameonyesha kiwango bora kwenye Ligi Kuu ya Ireland.
Matt Baker
Notts County imekamilisha usajili wa beki wa kati Matt Baker kwa mkataba wa miaka miwili, huku ikijiwekea chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi. Baker mwenye umri wa miaka 23 ni zao la akademi ya Stoke City na amejiunga na Notts County baada ya kumaliza safari yake ya miaka mitatu na nusu.
Morgan Rogers
Chelsea imefikia makubaliano ya rekodi ya Pauni117 milioni na Aston Villa kwa ajili ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa England, Morgan Rogers. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka sita katika Uwanja wa Stamford Bridge, huku Chelsea ikiwa na chaguo la kumuongezea mwaka mmoja zaidi.
Kelechi Iheanacho
Mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria, Kelechi Iheanacho, ameikataa ofa ya kuongeza mkataba na Celtic na badala yake amekamilisha uhamisho wake kwenda Bursaspor, klabu iliyopanda hivi karibuni Ligi Daraja la Kwanza nchini Uturuki. Hatua hiyo inahitimisha safari ya Iheanacho ndani ya kikosi cha mabingwa hao wa Scotland.
Reigan Heskey
Klabu ya Cologne ya Ujerumani imekamilisha usajili wa mshambuliaji chipukizi Reigan Heskey kutoka Manchester City katika dili lenye thamani inayoweza kufikia Pauni8 milioni. Heskey mwenye umri wa miaka 18, ambaye ni mtoto wa mshambuliaji wa zamani wa England, Emile Heskey.
Eduardo Camavinga
Kiungo wa Real Madrid, Eduardo Camavinga, anaweza kuruhusiwa kuondoka katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi huku klabu hiyo ikipanga kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 23 anaripotiwa kutaka kuendelea kubaki Santiago Bernabeu, lakini Real Madrid inaweza kumweka sokoni.
Francisco Trincao
Al Ahli imethibitisha rasmi kumsajili winga wa kimataifa wa Ureno, Francisco Trincao, akitokea Sporting CP katika moja ya usajili mkubwa wa dirisha hili. Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, klabu hiyo ya Saudi Arabia imelipa euro 40milioni pamoja na nyongeza ya euro4.3 milionikulingana na makubaliano ya bonasi.
Samuel Martinez
Liverpool ipo hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kiungo chipukizi Samuel Martinez kutoka Atletico Nacional kwa ada inayokadiriwa kufikia Pauni 750,000. Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, nyota huyo mwenye umri wa miaka 17 anatarajiwa kusafiri kuelekea Merseyside kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kusaini.
Cristian Romero
Tottenham Hotspur imeanza kujiandaa na uwezekano wa kumpoteza nahodha wake, Cristian ‘Cuti’ Romero, huku klabu kubwa za Ulaya zikionyesha nia ya kumsajili beki huyo wa kimataifa wa Argentina. Kwa mujibu wa TEAMtalk, Spurs inatarajia kupata takribani Pauni50 milioni kutokana na uhamisho wa Romero.