Solskjaer aitaka Man United, amsifu Carrick
Muktasari:
- Ole anaamini Carrick ana uwezo wa kuibadilisha timu hiyo na kuirejesha kwenye mafanikio, akisema licha ya kuonekana mtulivu, kocha huyo ana upande mkali ambao mashabiki wengi hawaufahamu.
MANCHESTER, ENGLAND: Aliyekuwa kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer anatamani kupata nafasi nyingine ya kuinoa Manchester United kutokana na kuhisi ana jambo hajalikamilisha, huku akimtetea Michael Carrick akiamini ana uwezo wa kubadili mwenendo wa timu hiyo.
Ole anaamini Carrick ana uwezo wa kuibadilisha timu hiyo na kuirejesha kwenye mafanikio, akisema licha ya kuonekana mtulivu, kocha huyo ana upande mkali ambao mashabiki wengi hawaufahamu.
Solskjaer, ambaye pia ni gwiji wa zamani wa United, amemtetea rafiki yake huyo licha ya kukabiliwa na presha kubwa kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo. Carrick anatajwa kuwa hatarini kupoteza kazi kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa, baada ya United kuanza msimu kwa kiwango kibaya zaidi katika ligi ndani ya miaka 40.
Akizungumza kuhusu uwezo wa Carrick, Solskjaer amesema anaamini ana sifa zinazohitajika kuiongoza United na kuifikisha mbali, akisisitiza kuwa anamfahamu vizuri klabu hiyo, mashabiki wake na matarajio yao.
“Michael ana kila kinachohitajika kuisogeza klabu hiyo mbele. Hamuuoni upande wake mkali, lakini anao, nami pia ninao. Tunafanana sana,” amesema Solskjaer.
Ameongeza kuwa Carrick anaielewa vizuri United na anafahamu mambo yanayohitajika ili kuiongoza klabu hiyo, akibainisha kuwa hata yeye mwenyewe hakutarajiwa na wengi kuwa kocha, achilia mbali kupewa nafasi ya kuinoa United.
Carrick amekuwa kwenye wakati mgumu baada ya kushindwa kushinda mechi tisa mfululizo katika mashindano yote, rekodi mbaya zaidi ya klabu hiyo ndani ya miaka 38. Hali hiyo imeongeza presha kwa uongozi wa United kutafuta njia ya kubadili mwenendo wa timu.
United ilifungwa mabao 2-0 na Chelsea Jumamosi, huku taarifa zikieleza kuwa viongozi wa klabu hiyo walikuwa wameamua kumfuta kazi Carrick. Hata hivyo, bado hawajafikia uamuzi kuhusu mrithi wake, baada ya kukabiliwa na changamoto ya kuwapata kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler, au Unai Emery wa Aston Villa.
Solskjaer, ambaye aliiongoza United kwa miaka mitatu baada ya kuitumikia kama mchezaji kwa misimu 11 na kushinda mataji 10 makubwa, amesema hana mpango wa kuwania nafasi ya Carrick. Hata hivyo, hakufunga mlango wa kurejea Old Trafford siku zijazo.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha TV2, raia huyo wa Norway amesema bado anahisi ana jambo ambalo hajalikamilisha ndani ya klabu hiyo na angefurahi kupata nafasi nyingine ya kuiongoza.
Amesema hata kama Carrick angeiongoza United kwa miaka 10 na baadaye kuamua kuondoka, asingekataa ombi la kuiongoza timu hiyo kwa muda mfupi endapo klabu ingemhitaji.
“Nimekuwa katika klabu hiyo kwa miaka 18 au 19, hivyo ni sehemu ya familia yangu. Lakini si jambo ninalolifikiria kwa sasa. Ninaikumbuka, ndiyo. Ningeweza kujiona nikiendelea kuwa hapo maisha yangu yote, lakini maisha yanaendelea. Kilikuwa kipindi cha kipekee,” amesema.
Solskjaer alifichua pia kuwa alifanya mazungumzo na viongozi wa United kabla ya Carrick kuteuliwa kuwa kocha wa muda Januari, kisha kupewa mkataba wa miaka miwili Mei ili kuiongoza timu hiyo kwa kudumu.
Amesema wakati huo hakukuwa na yeyote kati yao aliyekuwa akihangaikia kupata kazi hiyo, lakini wote walikuwa tayari kuitumikia klabu ikiwa wangeombwa.
Katika mazungumzo yake na viongozi wa United, Jason Wilcox na Omar Berrada, Solskjaer amesema alimpongeza Carrick na kuwaeleza kuwa wangepata mtu sahihi endapo wangemchagua.
Amesema naye Carrick alifanya vivyo hivyo kwa kumzungumzia vyema, huku akibainisha kuwa mazungumzo yao hayakuhusu muda wa mkataba wala masharti ya ajira, bali alijitolea kusaidia ikiwa klabu ingehitaji huduma yake.