Serena, Venus kurejea Cincinnati
Muktasari:
- Venus mwenye umri wa miaka 46 amepewa nafasi ya kucheza mchezo wa mmoja mmoja katika mashindano ya Cincinnati yatakayoanza Agosti 11, huku michuano ya US Open ikitarajiwa kuanza Agosti 31, New York.
WASHINGTON, MAREKANI: MASTAA wakongwe wa tenisi, Serena na Venus Williams wanatarajiwa kucheza mashindano ya Cincinnati Open katika mchezo wa wawili wawili mwezi huu baada ya kupewa nafasi maalumu (wild card).
Hatua hiyo inaashiria kurejea kwao kwenye mchezo huo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2022.
Kinadada hao wawili wamewahi kushinda mataji 14 makubwa ya mchezo wa wawili wawili (Grand Slam), yakiwemo sita ya Wimbledon, pamoja na medali tatu za dhahabu za Olimpiki.
Mara yao ya mwisho kucheza pamoja ilikuwa katika US Open 2022, ambapo walipoteza dhidi ya wachezaji wa Jamhuri ya Czech, Lucie Hradecka na Linda Noskova.
Mwezi uliopita, kinadada hao walilazimika kujiondoa katika orodha ya mchezo wa wawili wawili wa Wimbledon baada ya Serena, mwenye umri wa miaka 44, kupata tatizo la goti.
Serena alikuwa akirejea kwenye mashindano makubwa ya tenisi (Grand Slam) baada ya kuwa nje kwa miaka minne, lakini safari yake ilimalizika Wimbledon baada ya kupoteza katika raundi ya kwanza ya mchezo wa mmoja mmoja dhidi ya Muaustralia Maya Joint.
Venus mwenye umri wa miaka 46 amepewa nafasi ya kucheza mchezo wa mmoja mmoja katika mashindano ya Cincinnati yatakayoanza Agosti 11, huku michuano ya US Open ikitarajiwa kuanza Agosti 31, New York.