Kocha U-23 atoa matumaini mapya
Muktasari:
- Tanzania inaingia kwenye mchezo wa marudiano uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam ikiwa na kibarua kizito cha kupindua matokeo ya kichapo cha mabao 4-1 ilichokipokea Septemba 28, 2026 kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 23 (U23), Hamad Ally, ameweka wazi kuwa benchi lake la ufundi na wachezaji wamefanya tathmini ya kina ili kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza wa kufuzu AFCON U23 dhidi ya Kenya.
Tanzania inaingia kwenye mchezo wa marudiano uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam ikiwa na kibarua kizito cha kupindua matokeo ya kichapo cha mabao 4-1 ilichokipokea Septemba 28, 2026 kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Katika mchezo huo wa kwanza, Kenya ilifunga mabao yake kupitia Paul Osama dakika ya pili, Lawrence Okoth dakika ya 45, Kevin Wangaya (50) na Kelly Madada (75), huku bao pekee la Tanzania likifungwa na Shekhan Khamis kwa penalti katika dakika ya 54.
Akizungumzia maandalizi ya kuelekea mechi ya marudiano, Kocha Ally alieleza jinsi walivyotumia siku za mazoezi kufanyia kazi udhaifu wote uliojitokeza.
"Tulikuwa tuna maboresho tatizo la mechi iliyopita, kuangalia jinsi gani ambavyo tunaweza kusahihisha yale makosa ambayo yalipelekea kupoteza mechi. Leo tukabidi tupate mechi ili tuone jinsi gani ambavyo tumepunguza na kuona namna gani vijana wamepokea," alisema Ally na kuongeza
"Ni kitu kizuri, tumeona tena kutoka pale ambapo tulishia na kwa sasa tuna nafasi tena ya kurekebisha kuanzia leo, kesho na kesho kutwa kwa sababu tutakuwa tumebakiza kama siku tatu kuelekea mechi. Ni kipimo kizuri ambacho tumekipata na tutarudi kupanga kuona wapi ambapo tunahitaji kusahihisha zaidi ili kuwa bora zaidi."
Kwenye maandalizi ya mechi hiyo Tanzania ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Tanzania na kutoka sare ya 2-2.
Kocha huyo aliongeza kuwa wachezaji wamewahakikishia utayari wao wa kupambana ili kupata matokeo chanya nyumbani.
"Wao wameahidi kwamba walikubali tulianza vibaya mechi na Kenya hasa kipindi cha kwanza, lakini wamekubali pia kuona kwamba kama kweli wanaimini kwenye mipango na tukaenda kujitoa asilimia 100, tuna asilimia kubwa ya kupata matokeo."
Ili kusonga mbele katika hatua inayofuata na kukutana na Ivory Coast, Tanzania inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 3-0 nyumbani. Fainali za AFCON U23 zitakazofanyika mwakani nchini Misri ndizo njia kuu ya kukata tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2028 jijini Los Angeles, Marekani.