Ronaldo apiga 'hat-trick' afikisha bao la 985
Nyota wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo, wakati akishangilia moja ya bao katika mechi ya Ligi Kuu Saudi Arabia dhidi ya Al-Kholood
Muktasari:
- 'Hat-trick' hiyo imemfikisha Ronaldo kwenye idadi ya mabao 984 akiwa na Klabu pamoja na timu ya taifa.
RIYADH, SAUDI ARABIA: Nyota wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo, ameendeleza rekodi yake ya ufungaji baada ya kufunga mabao matatu (hat-trick) na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Al-Kholood katika mchezo wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia uliopigwa leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, amefunga mabao matatu katika kipindi cha pili, akifanya hivyo katika dakika za 66, 72 na 81, mabao ambayo yameiwezesha Al-Nassr kupata ushindi katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Kabla ya nyota huyo wa Ureno kuonyesha makali yake, Al Nassr ilikuwa imepata mabao mawili katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Ângelo Gabriel na Sadio Mané.
Hata hivyo, Al Kholood hawakuwa wanyonge baada ya Antoin Essomba kufunga bao moja pamoja na Julien Domingues kufunga mawili yaliyoifanya timu hiyo kuonyesha ushindani.
Ronaldo aibeba Al Nassr
Baada ya kipindi cha kwanza kilichoisha kwa sare ya mabao 2-2, Ronaldo aliibuka kuwa mchezaji muhimu katika kipindi cha pili akifunga mabao matatu ndani ya dakika 15
Dakika ya 66, Ronaldo alianza kwa kufunga bao la kwanza katika mchezo huo, kabla ya kuongeza la pili katika dakika ya 72 na kukamilisha idadi ya mabao matatu 'hat-trick' katika dakika ya 81.
Mabao hayo matatu yamekuwa sehemu muhimu ya ushindi wa Al Nassr, huku Ronaldo akiendelea kuonyesha uwezo wake wa kufunga licha ya umri mkubwa alionao.
Nyota wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo, wakati akishangilia moja ya bao katika mechi ya Ligi Kuu Saudi Arabia dhidi ya Al-Kholood
Asogelea rekodi ya mabao 1,000
Mbali na kuisaidia timu yake kupata ushindi, hat-trick hiyo imemfikisha Ronaldo kwenye idadi ya mabao 984 katika soka la kulipwa akiwa na Klabu pamoja na timu ya taifa.
Nyota huyo wa Ureno sasa amebakiza idadi ya mabao 16 ili kufikisha rekodi ya mabao 1000 katika historia ya soka.
Ronaldo amefunga mabao 450 akiwa na Real Madrid, 146 akiwa na timu ya taifa ya Ureno, 145 Manchester United, 138 Al Nassr, 101 Juventus huku akifunga mabao matano alipokuwa Sporting CP ya kwao Ureno.