Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kane aandika historia upya Ballon d’Or

KANE Pict

Muktasari:

  • Nyota huyo alikabidhiwa tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika London Palladium Jumatatu usiku, akishuhudia ndoto yake ya muda mrefu ikitimia mbele ya familia yake na mastaa mbalimbali wa soka duniani.

LONDON, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich na nahodha wa England, Harry Kane, ametwaa tuzo ya Ballon d’Or na kuandika historia kwa kuwa Mwingereza wa kwanza kushinda tuzo hiyo ya mchezaji bora wa dunia ndani ya miaka 25.

Kane amefanikiwa kuibuka mshindi mbele ya washindani wake wakuu, Kylian Mbappe na Lamine Yamal, kufuatia msimu uliopita uliokuwa wa mafanikio makubwa kwake.

Nyota huyo alikabidhiwa tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika London Palladium Jumatatu usiku, akishuhudia ndoto yake ya muda mrefu ikitimia mbele ya familia yake na mastaa mbalimbali wa soka duniani.

Hata hivyo, hafla hiyo ilianza kutawaliwa na sintofahamu saa chache kabla ya kuanza, baada ya tovuti rasmi ya Ballon d’Or kuchapisha makala tatu tofauti zilizowataja Kane, Mbappe na Yamal kuwa washindi wa tuzo kuu. Wakati huohuo, mapigano yaliripotiwa kutokea nje ya eneo la hafla kati ya mashabiki na walinzi waliokuwa wameandaliwa.

Licha ya vurugu hizo, Kane aliendelea kuwa mtulivu hadi alipotangazwa mshindi, akieleza kuwa alikosa maneno ya kuelezea furaha yake baada ya kutwaa tuzo hiyo kubwa zaidi katika maisha yake ya soka.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33, ambaye aliambatana na mke wake, Katie Goodland, alichapisha ujumbe kupitia mitandao ya kijamii baada ya ushindi wake.

“Fanya kazi kwa bidii kimya kimya. Acha mafanikio yako ndiyo yazungumze,” aliandika Kane.


KAN 01

MABAO 73

Mafanikio ya Kane yametokana kwa kiasi kikubwa na uwezo wake wa kufumania nyavu msimu uliopita, ambapo alifunga mabao 73 katika mashindano yote akiwa Bayern Munich na timu ya taifa ya England.

Akiwa na klabu hiyo ya Ujerumani, Kane alifunga mabao 61, idadi iliyomfanya kuwa mchezaji wa kwanza kufikia kiwango hicho katika msimu mmoja tangu Cristiano Ronaldo alipofunga mabao 61 akiwa Real Madrid msimu wa 2014/15.

Mabao yake 61 yalikuwa 19 zaidi ya mchezaji mwingine yeyote katika ligi tano kubwa za Ulaya kwa msimu huo, huku akiongeza mabao 12 aliyofunga akiwa na England na kufikisha jumla ya 73.

Kwa upande wa washindani wake, Mbappe alimaliza msimu akiwa na mabao 58, wakati Yamal alifunga 25.

Kane pia alichangia mabao kupitia pasi za mwisho, akifikisha jumla ya pasi za mabao 81, takwimu zilizompa nguvu katika kinyang’anyiro cha tuzo hiyo.

Msimu huo ulimshuhudia akipata mafanikio makubwa akiwa Bayern Munich, huku akiendelea kuiongoza England katika mashindano ya kimataifa.


KAN 02

“NAKOSA MANENO YA KUELEZEA”

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Kane alionekana kuzidiwa na hisia kutokana na ukubwa wa mafanikio aliyoyapata.

“Wow, wow, wow! Kwa kweli karibu nikose maneno. Kuwa hapa London kumefanya tukio hili kuwa la kipekee zaidi kwangu. Inaonekana limekuwa na bahati nzuri kwangu usiku huu,” alisema Kane.

Aliwashukuru wote waliompigia kura, akisema anaelewa kuwa ushindani wa mwaka huo ulikuwa mkali.

Kane aliguswa zaidi alipowataja wazazi wake, akieleza jinsi walivyojitolea kwa miaka mingi kumsaidia kufikia hatua hiyo.

“Mama na baba, huu ni wakati wa kipekee. Miaka yote ya kujitolea na kuniunga mkono, kunipeleka mazoezini na kuja kunitazama nikicheza, bila kujali nilikuwa wapi. Hata leo bado mpo pamoja nami,” alisema.

Aliongeza kuwa maadili na malezi aliyopata kutoka kwa wazazi wake ndiyo yaliyomsaidia kufikia mafanikio hayo.

Nyota huyo pia aliwatumia ujumbe watoto wake waliokuwa nyumbani wakifuatilia hafla hiyo, akitania kuwa muda ulikuwa umepita wa wao kwenda kulala.

“Nyinyi ndiyo sababu ya mimi kufanya haya. Hii ni tuzo ya kipekee sana. Siwezi kusubiri kuwaona na kusherehekea pamoja nanyi. Nawapenda sana,” alisema.

Hakumsahau mke wake, Kate, ambaye alimwelezea kama rafiki yake mkubwa na mtu aliyekuwa akimpa msaada mkubwa katika safari yake ya soka.

“Umekuwa msaidizi wangu mkubwa. Daima unanitakia mema na unajitolea ili kunisaidia kutimiza ndoto zangu. Bila wewe, hili lisingewezekana,” alisema.


KAN 02

AIPA HESHIMA BAYERN

Kane alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wachezaji wenzake wa Bayern Munich, makocha na wafanyakazi wa klabu hiyo kwa mchango wao katika mafanikio yake.

Alimpongeza kocha Vincent Kompany na kueleza kuwa tangu alipojiunga na Bayern, ameboresha uwezo wake wa kucheza soka, utu wake na uongozi ndani ya timu.

“Ni heshima kuchezea Bayern Munich. Kuiwakilisha klabu hii ni fursa kubwa kwangu, na ninafurahi kuirudishia klabu hii kombe hili,” alisema.

Pia aliwashukuru wachezaji wenzake wa England pamoja na kocha Thomas Tuchel, akieleza kuwa mwaka huo ulikuwa na nyakati nyingi nzuri licha ya kutokuwa mkamilifu kwa kila jambo.

Kane alisema anajivunia kuwa nahodha wa England na kuitumikia timu hiyo katika majukumu ya kuiongoza ndani na nje ya uwanja.

Katika sehemu iliyogusa hisia za mashabiki, Kane aliitaja pia Tottenham Hotspur, klabu aliyokulia kisoka kabla ya kujiunga na Bayern Munich.

“Napenda kuwashukuru Tottenham Hotspur pia. Bila Tottenham, nisingekuwa hapa nilipo leo. Nilijiunga nao nikiwa na umri wa miaka 11 na walinipa nafasi ya kuishi ndoto yangu,” alisema.

Alieleza kuwa changamoto na mafanikio aliyopitia akiwa Spurs vilikuwa sehemu muhimu ya safari iliyomfikisha kwenye kilele cha soka la dunia.


KAN 03

AWA WA KWANZA TANGU OWEN

Ushindi wa Kane unamfanya kuwa Mwingereza wa kwanza kutwaa Ballon d’Or tangu Michael Owen aliposhinda tuzo hiyo mwaka 2001.

Kwa kipindi cha miaka 25 iliyofuata, tuzo hiyo imewahi kutwaliwa na nyota mbalimbali wa soka duniani, akiwamo Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Luka Modric, Karim Benzema na Rodri.

Aidha, ushindi wake unakuwa wa kihistoria kwa Bundesliga, kwani anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka ligi hiyo kutwaa tuzo hiyo tangu Matthias Sammer wa Borussia Dortmund aliposhinda mwaka 1996.

Shirikisho la Soka England (FA) lilimulika Uwanja wa Wembley kwa heshima ya mafanikio ya nahodha huyo, huku Tuchel akimpongeza kwa kutambuliwa rasmi kama mchezaji bora duniani.

“Hongera Harry kwa kutwaa Ballon d’Or inayostahili. Nimeishiwa na maneno ya kuelezea kiwango cha uchezaji wako kwa muda mrefu, lakini ninafurahi kuona dunia ya soka hatimaye imetambua uwezo wako,” alisema Tuchel.

Kocha huyo aliongeza kuwa ushindi wa Kane ni jambo la kipekee kwa England, akieleza kuwa taifa hilo limepata nahodha anayestahili heshima hiyo baada ya kusubiri kwa robo karne.


KAN 04

ALIKUWA AKISUBIRI KWA HAMU

Kane alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotajwa kuwa na nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo kwa muda mrefu kabla ya hafla hiyo.

Tangu mwaka 2024, waandaaji wa Ballon d’Or kupitia jarida la France Football waliamua kutotangaza mshindi mapema kabla ya hafla, kwa lengo la kuongeza msisimko na kuzuia taarifa za mshindi kuvuja kabla ya wakati.

Hali hiyo imekuwa ikiwasumbua baadhi ya wachezaji na familia zao kutokana na presha ya kusubiri matokeo.

Kane mwenyewe alikiri kuwa mke wake na familia yake wangependa kujua matokeo mapema ili kupunguza msongo wa mawazo.

Hata hivyo, alisema alijitahidi kutokufikiria sana kuhusu tuzo hiyo na badala yake kuendelea na shughuli zake za kawaida.

Hatimaye, usiku wa Jumatatu uliishia kwa furaha kwa familia ya Kane, ambaye alipokea tuzo hiyo huku akishangiliwa na mastaa wenzake wa soka.

Kwa mshambuliaji huyo wa Bayern Munich, ushindi huo si tuzo nyingine katika kabati lake la mafanikio, bali ni kilele cha safari ya miaka mingi ya kujituma, kuvumilia na kuamini katika ndoto yake ya kuwa mchezaji bora duniani.