Robo fainali za moto WAFCON 2026
Muktasari:
- Timu hizo zitachuana kusaka ushindi utakaoipeleka timu moja hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, huku timu nne zitakazofika hatua hiyo zikipewa nafasi ya kufuzu moja kwa moja kushiriki Kombe la Dunia mwakani.
Mechi mbili za robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) zitapigwa leo, ambapo Ivory Coast itaikaribisha Algeria katika mchezo utakaopigwa saa mbili usiku, huku wenyeji Morocco wakiikaribisha Afrika Kusini saa tano usiku.
Mechi zote zitapigwa katika Uwanja wa Moulay Rachid jijini Rabat.
Timu hizo zitachuana kusaka ushindi utakaoipeleka timu moja hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, huku timu nne zitakazofika hatua hiyo zikipewa nafasi ya kufuzu moja kwa moja kushiriki Kombe la Dunia mwakani.
Mwanaspoti imechambua safari za timu hizo katika mashindano hayo, rekodi zao na kile kinachoweza kutokea katika mechi hizo za robo fainali.
SAFARI ZAO
Mwenyeji Morocco amefika robo fainali akiwa hajapoteza mchezo wowote katika hatua ya makundi.
Ilianza kampeni yake kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Kenya, kisha ikaibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Algeria kabla ya kutoka sare tasa na Senegal katika mchezo wa mwisho wa kundi.
Matokeo hayo yaliifanya Morocco kumaliza kileleni mwa Kundi A ikiwa na pointi saba, ikifunga mabao matano bila kuruhusu hata moja langoni mwake.
Rekodi hiyo inaifanya kuwa miongoni mwa timu zenye safu bora ya ulinzi katika mashindano ya mwaka huu.
Afrika Kusini imepitia njia ngumu zaidi kufika hatua hiyo. Mabingwa hao watetezi walianza kwa kushtushwa na Tanzania iliyowafunga mabao 2-1, matokeo yaliyowalazimu kupambana katika mechi zilizofuata.
Baada ya hapo, walitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Ivory Coast kabla ya kumaliza hatua ya makundi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Burkina Faso kupitia Thembi Kgatlana.
Pointi nne ziliwatosha kumaliza nafasi ya pili katika Kundi B na kukata tiketi ya robo fainali.
Ivory Coast ilimaliza kinara wa Kundi B ikiwa na pointi saba. Ilianza kwa ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Burkina Faso, kisha ikatoka sare ya 2-2 na Afrika Kusini na kumaliza hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania.
Kwa upande wa Algeria, ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi A. Ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Senegal, ikapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco, kisha ikashinda mabao 2-0 dhidi ya Kenya.
REKODI ZAO
Morocco inashiriki WAFCON kwa mara ya tano na katika ushiriki wake huo imefika fainali mara moja, mwaka 2022, huku mara nyingine ikiishia hatua ya makundi.
Hata hivyo, hivi karibuni timu hiyo imekuwa ikionyesha ushindani wa aina yake na kuibuka kwa kasi katika soka la wanawake barani Afrika.
Katika WAFCON ya mwaka huu, imeonyesha maendeleo makubwa zaidi kwa kumaliza hatua ya makundi bila kupoteza mchezo na bila kuruhusu bao lolote.
Rekodi hiyo imeifanya kuwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutinga hatua ya nusu fainali.
Kwa upande wa Afrika Kusini, ni moja ya mataifa yenye mafanikio makubwa katika historia ya WAFCON.
Banyana Banyana ilitwaa ubingwa wake wa kwanza mwaka 2022 baada ya kuifunga Morocco katika fainali.
Mbali na ubingwa huo, imewahi kumaliza nafasi ya pili mara tano na kushika nafasi ya tatu mara nne, jambo linaloifanya kuwa moja ya timu zenye uzoefu mkubwa zaidi katika hatua za mtoano za mashindano haya.
Mara ya mwisho timu hizi zilipokutana katika WAFCON ilikuwa katika fainali ya mwaka 2022 mjini Rabat.
Afrika Kusini ilishinda mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa Afrika, huku Morocco ikikosa nafasi ya kutwaa taji mbele ya mashabiki wake.
Mechi hiyo ndiyo inayoongeza uzito wa robo fainali ya mwaka huu, kwani Morocco inaingia ikiwa na dhamira ya kulipa kisasi.
Algeria, maarufu kama Les Fennecs, imekuwa na uzoefu mkubwa zaidi wa kushiriki michuano hiyo ikiwa imefanya hivyo mara saba, lakini bado inasaka mafanikio makubwa baada ya rekodi yake bora kuwa kufika robo fainali mwaka 2024.
Kwa upande mwingine, Ivory Coast, maarufu kama The Elephants, inarejea kwenye michuano hiyo baada ya kukaa nje kwa miaka 12, ikiwa na kumbukumbu ya kumaliza nafasi ya tatu mwaka 2014, ambayo ndiyo rekodi yake bora kabisa katika WAFCON.
Hii ni mara ya nne kwa Ivory Coast kushiriki WAFCON na haijawahi kutwaa ubingwa wala kufika fainali.
Hivyo, mchezo huo unawakutanisha timu mbili zenye kiu tofauti; Algeria ikitaka kuthibitisha kiwango chake baada ya kuvunja rekodi yake ya kufika robo fainali, huku Ivory Coast ikitaka kurejesha heshima ya kizazi kilichowahi kuipeleka hadi medali ya shaba mwaka 2014.
WACHEZAJI WA KUTAZAMWA
Morocco imekuwa ikimtegemea zaidi mshambuliaji Ibtissam Jraïdi, ambaye tayari amefunga mabao mawili katika mashindano haya. Uzoefu wake mbele ya lango unaweza kuwa silaha muhimu kwa wenyeji.
Mbali naye, wapo Sanaâ Mssoudy, aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Algeria, Sakina Ouzraoui, aliyeanza mashindano kwa kiwango bora dhidi ya Kenya, pamoja na kiungo Maryame Atiq, ambaye amekuwa akitengeneza nafasi nyingi za kufunga.
Kwa upande wa Afrika Kusini, macho yote yatakuwa kwa Thembi Kgatlana, mshambuliaji ambaye tayari amefunga mabao mawili na kuisaidia timu yake kufuzu robo fainali.
Pia yupo Hildah Magaia, mchezaji mwenye uzoefu wa kuamua mechi kubwa, huku nahodha wa safu ya ulinzi, Bambanani Mbane, akitarajiwa kuiongoza timu hiyo katika kuhimili mashambulizi ya Morocco.
Algeria itaongozwa na uzoefu wa wachezaji kama Lina Boussaha, ambaye aliwahi kukipiga PSG ya Ufaransa, pamoja na Amel Majri, wanaotarajiwa kutoa ubunifu na utulivu katika eneo la ushambuliaji.
Kwa upande wa Ivory Coast, tishio kubwa litakuwa kwa Habibou Ouedraogo na Rosemonde Kouassi, ambao kila mmoja amefunga mabao mawili. Wawili hao wana uwezo mkubwa wa kufunga na kuvuruga mipango ya wapinzani.