Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Roberto De Zerbi acharuka Spurs

ZERBI Pict

Muktasari:

  • Tottenham ilipoteza kwa mabao 3-2 katika mchezo huo, huku ikiwa nyuma kwa mabao 3-0 hadi dakika ya 86 kabla ya kufunga mabao mawili ya dakika za mwisho na kupunguza machungu ya kipigo hicho.

LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Tottenham Hotspur, Roberto De Zerbi, amewashukia vikali wachezaji wake baada ya timu hiyo kuendelea na mwanzo mbaya wa msimu kufuatia kipigo cha nyumbani dhidi ya Aston Villa.

Tottenham ilipoteza kwa mabao 3-2 katika mchezo huo, huku ikiwa nyuma kwa mabao 3-0 hadi dakika ya 86 kabla ya kufunga mabao mawili ya dakika za mwisho na kupunguza machungu ya kipigo hicho.

Matokeo hayo yanaifanya Spurs kubaki bila ushindi katika michezo yake mitano ya mwanzo ya Ligi Kuu England, huku ikikabiliwa na kipindi kigumu kabla ya kurejea uwanjani baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

De Zerbi hakuficha hasira na masikitiko yake baada ya mchezo huo, akilaumu zaidi udhaifu wa safu yake ya ulinzi na namna timu ilivyoruhusu mabao ambayo aliamini yangeweza kuzuilika.

“Nilikuwa nimekata tamaa sana, nilikuwa na huzuni na nimechanganyikiwa kutokana na kiwango chetu. Hatuwezi kupoteza mchezo kama huu. Hatuwezi kuruhusu bao la pili kwa namna ile,” alisema De Zerbi.

ZER 03

Kocha huyo alikerwa zaidi na bao la pili la Aston Villa, lililofungwa katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili baada ya Spurs kupoteza mpira katika eneo ambalo aliamini wachezaji wake walipaswa kuwa watulivu zaidi.

De Zerbi alisema aliwaasa washambuliaji wake wakati wa mapumziko kucheza kwa utulivu, kutumia akili na kuepuka kuchukua hatari zisizo za lazima.

“Dakika ya 51 ilikuwa bado mapema. Niliwaambia katika kipindi chote cha pili wawe watulivu, wacheze na wafurahie mchezo bila kuchukua hatari. Lakini bao tuliloruhusu lilikuwa la kushangaza,” alisema.

Kocha huyo pia hakufurahishwa na bao la kwanza la Villa, lililofungwa wakati Tottenham ikiwa na wachezaji 10 uwanjani. Micky van de Ven alikuwa nje ya uwanja akipatiwa matibabu baada ya kugongana kichwa na Tyrone Mings.

ZER 04

De Zerbi alisisitiza kuwa hata ikiwa timu ilikuwa pungufu kwa mchezaji mmoja, ilipaswa kujilinda kwa umakini zaidi.

“Tunapaswa kuwa imara zaidi, kuwasiliana zaidi na kujilinda kwa mpangilio. Niliweka Bentancur kuwa beki wa kati na Mateus Fernandes kwenye kiungo. Kama tungekuwa na kadi nyekundu, tungeweza kucheza dakika 60 tukiwa 10. Tatizo lingekuwa nini?”alihoji. Tottenham ilidhani imepata bao la kusawazisha kupitia mchezaji aliyekuwa ametokea benchi, Kudus, lakini bao hilo lilikataliwa na VAR kutokana na kuotea. Muda mfupi baadaye Villa ilifunga bao la pili.

De Zerbi alisema Tottenham ilipaswa kuwa imejiandaa kwa aina hiyo ya uchezaji, akibainisha kuwa Villa imekuwa ikitumia mipira mirefu kwa kiwango kikubwa zaidi msimu huu.

Alitaja pia haja ya viongozi wa timu kusimama wakati mambo yanapokuwa magumu.

“Mpira wa miguu ni kama maisha; ama unakuwa imara zaidi au unapoteza. Viongozi wanapaswa kuwa viongozi na kuiongoza timu,” alisema.


ZER 01

AWAKOSOA FERNANDES NA SOLANKE

De Zerbi hakusita pia kuwataja baadhi ya wachezaji aliowataka wafanye zaidi, akiwemo kiungo Mateus Fernandes, ambaye alitolewa wakati wa mapumziko.

“Nina imani kubwa na Mateus, lakini sikupenda kiwango chake. Kama ningekipenda, nisingembadilisha. Anajua hilo. Si kumshambulia Mateus, nampenda, lakini tunahitaji zaidi kutoka kwake,” alisema.

Kwa upande wa mshambuliaji Dominic Solanke, De Zerbi alisema timu inahitaji mchango mkubwa zaidi kutoka kwake, huku akibainisha kuwa hali yake ya kimwili bado haijawa katika kiwango kinachohitajika.

“Tunamhitaji zaidi, kwa hakika. Namkubali Dom kama mchezaji na nitasimama naye hadi mwisho. Anahitaji kuwa katika hali nzuri zaidi na kujisikia vizuri zaidi. Hali yake ya kimwili bado haitoshi,” alisema.

De Zerbi pia aliamini Solanke amepoteza sehemu ya kujiamini, akisisitiza kuwa uwezo wake ni mkubwa kuliko kiwango alichoonyesha kwa sasa.


ZER 02

SOKO LA USAJILI NALO LAMKERA

Kocha huyo aligusia pia changamoto zilizojitokeza katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi, akieleza kuwa klabu haikuweza kufanya baadhi ya mipango iliyokuwa imekusudiwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo masuala ya kanuni za Financial Fair Play.

Alisema Tottenham ilitarajia kuuza baadhi ya wachezaji ili kuwezesha kufanya usajili mwingine, lakini mipango hiyo haikutimia.

“Dirisha la usajili lilikuwa refu na mambo yalibadilika mara nyingi. Pia kulikuwa na Financial Fair Play ambayo tulipaswa kuiheshimu. Hatukuuza wachezaji ambao mwanzoni tulifikiri tungeweza kuwauza. Kuna sababu nyingi,” alisema.

De Zerbi alisisitiza kuwa yeye pamoja na uongozi wa klabu wanafahamu mapungufu yaliyopo na wanaendelea kutafuta namna ya kuyarekebisha.

Tottenham sasa itarejea uwanjani baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, ambapo itasafiri kucheza dhidi ya Manchester United.