Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rayon yaichapa KVZ, yaitambia APR 

RAYON Pict

Muktasari:

  • Mara baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, mashabiki wa Rayon Sports wameonyesha furaha yao huku wakitupa vijembe kwa wapinzani wao APR, waliopata fedheha ya kuchapwa mabao 5-0 na Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wao wa ufunguzi wa michuano hiyo.

MAISHA ya mashabiki wa Simba na Yanga nchini Tanzania yanafanana kwa kiasi fulani na ushindani uliopo kati ya APR na Rayon Sports hapa Rwanda, jambo lililojidhihirisha leo, Jumapili kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali baada ya Rayon Sports kuifunga KVZ ya Zanzibar mabao 2-0 katika mchezo wa Kundi C wa Kombe la CECAFA Kagame.

Mara baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, mashabiki wa Rayon Sports wameonyesha furaha yao huku wakitupa vijembe kwa wapinzani wao APR, waliopata fedheha ya kuchapwa mabao 5-0 na Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wao wa ufunguzi wa michuano hiyo.

Kwa mashabiki hao, ushindi huo ulikuwa nafasi ya kujivunia mbele ya wapinzani wao wa muda mrefu ambao wameanza vibaya mashindano hayo.

KVZ ilianza mchezo kwa kujilinda vizuri na kufanikiwa kuhimili mashambulizi ya wenyeji katika kipindi cha kwanza huku ikiwalazimu wachezaji wa Rayon Sports kutafuta mbinu tofauti za kuvunja ukuta wa safu ya ulinzi ya wageni, dakika 45 za kwanza zilimalizika bila timu yoyote kuona lango.

Hata hivyo, kipindi cha pili kilikuwa tofauti baada ya KVZ kupoteza utulivu na kuanza kufanya makosa yaliyoipa Rayon Sports nafasi ya kutawala mchezo.

Presha hiyo ilizaa matunda dakika ya 69 baada ya Rayon Sports kupata mkwaju wa penalti uliotekelezwa kwa utulivu na Kemeni Junior, aliyeandika bao la kwanza na kuamsha shangwe kwa mashabiki waliojitokeza Uwanja wa Amahoro.

Licha ya kuwa mbele kwa bao moja, Rayon Sports haikuridhika iliendelea kulisakama lango la KVZ na kufanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 82 kupitia Daniel Muhoza, aliyemalizia vizuri shambulizi lililoondoa kabisa matumaini ya timu hiyo ya Zanzibar kurejea mchezoni.

Baada ya ushindi huo, mashabiki wa Rayon Sports waliendelea kuimba nyimbo za kejeli dhidi ya APR, wakikumbushia kipigo kizito cha mabao 5-0 walichopata kutoka kwa Gor Mahia, juzi Ijumaa. 

Tukio hilo lilionyesha jinsi ushindani kati ya vigogo hao wa Rwanda ulivyo mkubwa, ukiwa na sura inayofanana na ule wa Simba na Yanga nchini Tanzania.

Ushindi huo unaipa Rayon Sports pointi tatu katika mbio za kusaka nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali huku ukiwa umeongeza furaha kwa mashabiki wao na kuwapa nafasi ya kujigamba mbele ya wapinzani wao APR.