Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Trump alivyoteka shoo na kuibua gumzo

TRUMP Pict

Muktasari:

  • Hispania ilitwaa ubingwa wake wa pili wa Kombe la Dunia kwa kuifunga Argentina bao 1-0 kupitia Ferran Torres katika muda wa nyongeza, lakini mchezo wenyewe haukuwa na matukio mengi ya kuvutia.

NEW YORK, MAREKANI: FAINALI ya Kombe la Dunia 2026 huenda isikumbukwe kwa ubora wa soka lililoonyeshwa uwanjani, bali kwa matukio makubwa yaliyoizunguka. Kuanzia Donald Trump, Tom Cruise, Madonna, Justin Bieber hadi fataki za mchana kweupe, kila kitu kilionekana kama tamasha kuliko mechi ya mpira wa miguu.

Hispania ilitwaa ubingwa wake wa pili wa Kombe la Dunia kwa kuifunga Argentina bao 1-0 kupitia Ferran Torres katika muda wa nyongeza, lakini mchezo wenyewe haukuwa na matukio mengi ya kuvutia.

Badala yake, kilichotawala mazungumzo ni kila kitu kilichotokea nje ya dakika 120 za mchezo.

TRUM 03

Trump afika kwa helikopta

Kombe la Dunia la mwaka huu liliandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico, lakini Marekani ndiyo iliyovuta macho zaidi kutokana na matukio yaliyomhusu Rais Donald Trump.

Katika kipindi chote cha mashindano, Trump alikuwa hajahudhuria mechi hata moja, jambo lililowafanya wengi kusubiri kwa hamu kuona kama angejitokeza kwenye fainali.

Hatimaye aliwasili Uwanja wa New York New Jersey kwa moja ya helikopta tatu zilizoruka juu ya uwanja kabla ya kutua.

Aliingia uwanjani dakika 20 kabla ya mchezo kuanza na kuketi pembeni ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino, akishuhudia sherehe za ufunguzi zilizopambwa na maonyesho ya Robbie Williams na Nicole Scherzinger.

Baadaye kamera zilimnasa akiwa anaangalia kwa karibu Kombe la Dunia kabla ya mchezo kuendelea.


Mapumziko marefu kuliko yote

Jambo jingine lililozua mjadala mkubwa ni mapumziko ya dakika 27 katikati ya mchezo, marefu zaidi kuwahi kushuhudiwa kwenye fainali ya Kombe la Dunia.

Badala ya dakika 15 za kawaida, waandaaji waliamua kuiga mfumo wa Super Bowl kwa kuandaa tamasha kubwa la muziki.

Madonna, BTS, Coldplay, Shakira pamoja na Justin Bieber walitumbuiza mashabiki waliojaa uwanjani.

Shakira aliimba wimbo rasmi wa mashindano, Dai Dai, huku Bieber akibadilisha mwelekeo wa burudani kwa kupiga gitaa la akustiki na kuimba Everything Hallelujah.

TRUM 02

Lakini si kila mtu alivutiwa na tamasha hilo.

Mshambuliaji wa zamani wa England, Wayne Rooney, aliliponda waziwazi.

“Lilikuwa baya. Maonyesho hayakuwa mazuri na muda haukuwa sahihi. Tuacheni tuangalie mpira,” amesema Rooney.


Tom Cruise afungua pazia

Kabla ya mchezo kuanza, mwigizaji maarufu wa Hollywood, Tom Cruise, aliingia uwanjani na kutoa hotuba ya hamasa mbele ya maelfu ya mashabiki.

Sherehe  hizo zilipambwa pia na muziki mkubwa, ngoma na fataki nyingi zilizolipuliwa mchana kweupe, jambo lililoongeza taswira ya tamasha kubwa la burudani.


Trump karibu aibe shoo ya kombe

Baada ya mchezo kumalizika, macho yote yalielekezwa kwenye jukwaa la kukabidhi medali na kombe.

Trump, akiwa sambamba na Infantino, aliwavalisha medali wachezaji wa Argentina na Hispania kabla ya kukabidhi kombe kwa mabingwa.

Kama ilivyotokea kwenye fainali ya Kombe la Dunia la Klabu mwaka uliopita, Trump alionekana kuchelewa kuondoka jukwaani wakati wa sherehe za ushindi.

Katika tukio hilo la mwaka jana, nahodha wa Chelsea, Reece James, amesema Trump alitakiwa kukabidhi kombe na kuondoka, lakini aliamua kubaki kusherehekea na wachezaji.

Safari hii hakukaa muda mrefu kama ilivyokuwa awali, lakini alibaki jukwaani kwa muda mfupi wakati Hispania ikianza kushangilia ubingwa wake.

TRUM 01

Mashabiki wamzomea

Wakati Trump na Infantino walipotokea kwa ajili ya kukabidhi medali, sehemu ya mashabiki ilisikika ikiwazomea.

Kulikuwa pia na tukio lililovuta hisia baada ya beki wa Argentina, Cristian Romero, kuonekana akipita moja kwa moja bila kumsalimia Trump, akipokea medali yake kutoka kwa Infantino na kuendelea mbele.

Licha ya Hispania kutwaa ubingwa kwa ushindi wa Ferran Torres, wengi wataikumbuka fainali hii kwa tamasha, si kwa soka.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, burudani ya nje ya uwanja ilionekana kuuteka mchezo wenyewe.