POLLARD: Bondia mwenye rekodi ya vipigo anayeamini mshindi
Muktasari:
- Ungekuwa wewe ungeweza kuendelea na kazi hiyo ambayo mara nyingi mabondia wazuri hupimwa kwa mikanda na rekodi za ushindi walizoziweka.
HIVI unajua kuna bondia ambaye katika mapambano 101 aliyowahi kucheza katika ngumi za kulipwa, ameshinda pambano moja tu na kupoteza 100, lakini bado anaamini yeye ni mshindi na hajakata tamaa anaendelea kucheza.
Ungekuwa wewe ungeweza kuendelea na kazi hiyo ambayo mara nyingi mabondia wazuri hupimwa kwa mikanda na rekodi za ushindi walizoziweka.
Jake Pollard, Muingereza ambaye wakati mashabiki wakimshanhazwa na rekodi yake ya kushinda pambano moja yeye binafsi anaamini amepata ushindi mkubwa zaidi ya mikanda na sifa zinazotafutwa na mabondia wengi duniani.
Pollard, aliyezaliwa Bradford, nchini Uingereza, alianza kucheza mchezo wa ngumi akiwa na umri wa miaka 21. Tofauti na mabondia wengi wanaoingia kwenye mchezo huo wakiwa na ndoto za kutwaa mataji makubwa, safari yake ilichukua tofauti.
Kwa mtu anayetazama rekodi yake, anaweza kudhani Pollard hana uwezo wa kushindana, lakini yeye ana mtazamo mwingine akisema kazi yake siyo lazima iwe kushinda kila pambano, bali kuhakikisha vijana wanaotaka kujenga majina yao wanapata upinzani ulingoni.
“Watu wanaweza kuniita majina wanayotaka. Wengine huniita bondia wa upande wa pili, mshindwa kila siku, wa kulipwa na hata majina mengine mabaya. Ukweli ni kwamba sijali,” alisema Pollard katika mahojiano na Uncrowned
Katika mchezo wa ngumi za kulipwa, mabondia wa aina yake hujulikana kama 'Journeymen'. Hawa ni wapiganaji ambao mara nyingi hupangwa kupambana na mabondia wanaoanza safari zao za kulipwa, kwa lengo la kuwapa uzoefu na kupima uwezo wao. Ingawa mara nyingi huingia ulingoni wakiwa upande usiopewa nafasi kubwa ya kushinda, mchango wao katika safari za mabondia wanaochipukia ni sehemu ya biashara ya mchezo huo.
Pollard anasema amekubali nafasi hiyo na anaiona kama kazi inayomuwezesha kuendesha maisha yake. Kwa mtazamo wake, bondia anayeanza ngumi anapaswa kupimwa na mtu ambaye hatapata ushindi kirahisi.
“Nipo kuhakikisha ninawapima vijana hao na kuona kama wana uwezo au la. Mimi ni hatua ya kwanza kwenye ngazi yao ya mafanikio. Lakini kama hawana uwezo, watagundua hilo pindi nitakapowapiga,” anasema.
ALIANZIA HUKU
Safari yake haikuanza moja kwa moja kwenye ngumi za kulipwa. Pollard anasema mwanzoni alijaribu ngumi za ridhaa, lakini hakuridhishwa na mazingira yake, ndipo kocha wake alipomuelekeza kwenye mashindano ya 'white-collar boxing'.
Haya ni mashindano yanayowashirikisha watu ambao si lazima wawe mabondia wa kitaalamu, lakini hupata mafunzo na kushiriki mapambano yaliyopangwa kwa utaratibu maalumu.
Alipokuwa akishiriki mashindano hayo, alianza kupata nafasi za kupigana katika maeneo mbalimbali nchini Uingereza. Kadiri alivyoendelea, ndivyo alivyovutia watu waliokuwa wakitafuta mabondia wa kuwapa vijana wao changamoto. Kocha wake wa pili, Peter Cannon, ndiye aliyemshawishi kuhamia kwenye ngumi za kulipwa ili aweze kupata kipato kikubwa zaidi.
KWENYE NGUMI
Mwaka 2018, Pollard aliingia rasmi kwenye ngumi za kulipwa. Pambano lake la kwanza lilikuwa dhidi ya Delmar Thomas mjini Nottingham. Alipoteza kwa pointi, lakini hakukata tamaa.
Badala yake, alianza kutengeneza jina kama bondia anayekubali kupigana katika maeneo mbalimbali, wakati mwingine akipewa taarifa za pambano saa chache kabla ya kupanda ulingoni.
Hata hivyo, Pollard anasema kazi hiyo inahitaji akili katika kupanga malipo na kutambua hatari. Anapokubali kupambana na bondia mwenye uwezo mkubwa wa kumpiga kwa nguvu, anataka malipo yaendane na hatari anayochukua.
Anaeleza kuwa akipigwa ngumi nzito na kulazwa hospitali, anaweza asicheze kwa siku 28 na hivyo kukosa nafasi ya kupata kipato katika kipindi hicho.
Kwa pambano la kawaida la raundi nne, Pollard alisema anaweza kulipwa takribani pauni 1,400. Anaiona hiyo kuwa fedha nzuri kwa kazi inayoweza kumalizika ndani ya usiku mmoja, tofauti na mtu anayefanya kazi kwa saa nyingi kwa siku kadhaa ili kupata kiasi hicho.
ANAVYOENDELEA KUPIGANA
Lakini kinachoshangaza zaidi ni ujasiri wake wa kuendelea kupigana licha ya rekodi yake mbovu. Katika mapambano yake 100 aliyopoteza, amesimamishwa na mwamuzi kwa kupigwa mara sita pekee. Anasema amejifunza kujilinda na kutambua wakati wa kujihatarisha na wakati wa kupunguza mashambulizi ya mpinzani.
“Nimewahi kupoteza mara nyingi, lakini sijawahi kupelekwa hospitali baada ya pambano wala kurudi nyumbani kwa gari la wagonjwa. Kwa mtazamo wangu, nina ushindi 101,” alisema.
Kauli hiyo inaeleza namna anavyopima mafanikio yake. Kwake ushindi si lazima ashinde pambano bali afya yake akiamini kutoka salama ulingoni ni mafanikio yake makubwa.
MTUNZA VIATU
Nje ya ngumi, Pollard anafanya kazi ya kutunza kwato na viatu vya farasi. Kazi hiyo nayo ina ugumu wake, hasa wakati wa baridi, anapolazimika kufanya kazi kwenye matope na mvua huku akishughulika na mnyama mwenye uzito mkubwa. Hata hivyo, anasema kazi zote mbili zinamsaidia kuendesha maisha yake.
Jambo analolipa uzito mkubwa ni familia yake, hasa mtoto wake Roman. Pollard anasema kipato anachopata kupitia mapambano kinamwezesha kumtunza mwanawe, kumpeleka matembezini na kumfanyia mambo ambayo huenda yasingekuwa rahisi bila kazi hiyo.
Mpenzi wake, Reanne, anasema anajivunia kujituma kwake, ingawa huwa na wasiwasi anapomwona akiendelea kupambana mara kwa mara. Anatambua kuwa mwili wa binadamu haujaumbwa kustahimili mapigo ya ngumi kila mwisho wa wiki, lakini pia anajua mchezo huo ni sehemu muhimu ya maisha ya Pollard.
BADO YUMO
Pollard anakiri kuwa muda wa maisha yake ya ndondi una mwisho, lakini kwa sasa hana mpango wa kuacha. Anachotaka ni kuendelea kufanya kazi.
Kwa bondia mwingine, rekodi ya ushindi mmoja na vipigo 100 inaweza kuwa sababu ya kuachana na mchezo huo. Lakini kwa Pollard, kurejea nyumbani akiwa salama, kupata kipato na kucheza mpira na mwanawe ndiko kunakomfanya aamini bado anashinda.
“Ushindi unategemea namna unavyoutazama,” alisema, akieleza falsafa yake ya maisha ndani ya mchezo ambao wengi huupima kwa mikanda, mataji na idadi ya mapambano yaliyoshindwa.