LeBron anavyoandika jina vitabu vya rekodi za NBA
Muktasari:
- Mchezaji huyo nyota wa Philadelphia 76ers amepanda hadi nafasi ya tatu katika orodha ya wachezaji waliotoa asisti nyingi zaidi kwenye historia ya NBA, baada ya mechi dhidi ya Portland Trail Blazers majuzi.
LOS ANGELES, MAREKANI: KATIKA msimu wake wa 24, LeBron James anaendelea kushikilia nafasi za juu katika vipengele mbalimbali vya historia ya Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), huku akiendelea kuvunja na kufukuzia rekodi nyingine.
Mchezaji huyo nyota wa Philadelphia 76ers amepanda hadi nafasi ya tatu katika orodha ya wachezaji waliotoa asisti nyingi zaidi kwenye historia ya NBA, baada ya mechi dhidi ya Portland Trail Blazers majuzi.
LeBron aliipita rekodi ya Jason Kidd aliyekuwa na pasi 12,091, baada ya kufikisha 12,092 na hivyo kuendelea kuthibitisha ubora wake kama mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya NBA katika kutengeneza nafasi za kufunga kwa wenzake.
Uwezo wa LeBron kuona mchezo na kusoma mienendo ya wapinzani umekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yake akitawala katika mfumo wa mashambulizi wa 'high pick-and-roll', ambapo anaweza kupenya hadi karibu na kikapu au kutoa pasi kwa wachezaji wenzake, huku akiendelea kuwa makini kuwaona wachezaji wanaokata njia kuelekea kwenye kikapu.
LeBron akizungumza baada ya kuipita rekodi ya Kidd, alisema mafanikio hayo yanatokana pia na mchango wa wachezaji wenzake.
"Inamaanisha nilikuwa na wachezaji wengi wazuri wenzangu. Unahitaji kuwa na wachezaji wanaoweza kuingiza mpira ndani ya kikapu. Kazi yangu ni kuhakikisha ninatoa pasi kwa wakati sahihi na mahali sahihi," alisema LeBron.
Aliongeza: "Ninapenda historia ya mchezo huu. Ninawapenda wachezaji waliotangulia kabla yangu. Hii ni heshima kubwa sana."
LeBron alisema amekuwa akifurahia kuona wachezaji wenzake wakifunga tangu siku yake ya kwanza alipoanza kucheza mchezo wa kikapu.
"Daima nimekuwa nikifurahia na kupata furaha kubwa ninapowaona wachezaji wenzangu wakifunga. Ilikuwa hisia nzuri sana kwangu. Nilielewa namna nguvu na hamasa inayotokana na pasi moja inavyoweza kuambukiza timu nzima," alisema.
Alianza taaluma yake akiwa na wastani wa pasi 5.9 kwa kila mchezo katika msimu wake wa kwanza (rookie), lakini katika misimu 23 iliyofuata hakuwahi kushuka tena chini ya wastani huo. Alikuwa akikusanya wastani wa pasi kati ya 6.0 na 10.2 kwa kila mchezo.
Wastani huo wa pasi 10.2 ulimwezesha kutwaa tuzo ya mchezaji aliyetoa pasi nyingi zaidi katika msimu wa 2019/20, huku akiisaidia Los Angeles Lakers kutwaa ubingwa wa NBA. Lakini, mbali na rekodi hiyo, mchezaji huyo anayejulikana kwa jina la utani la King ana nafasi gani katika vipengele vingine vya historia ya NBA?
POINTI, RIBAUNDI
LeBron ndiye kinara wa muda wote wa ufungaji wa pointi katika historia ya NBA akiwa nazo 43,606. Hakuna mchezaji mwingine katika historia ya NBA ambaye amefikisha pointi 40,000, huku ni wachezaji wanane pekee waliovuka alama ya pointi 30,000.
Vilevile, LeBron anashika nafasi ya 23 katika orodha ya wachezaji waliokusanya ribaundi nyingi zaidi katika historia ya NBA, akiwa nazo 12,174, ambapo mchezaji anayemfuatia katika orodha ni Charles Oakley mwenye 12,205.
Oakley aliwahi kuwa na wastani wa ribaundi zaidi ya 13.0 kwa kila mchezo katika misimu miwili na alimaliza akiwa nafasi ya pili nyuma ya Michael Cage katika mbio za karibu sana za kuwania ufalme wa ribaundi msimu wa 1987/88.
Mchezaji maarufu Dennis Rodman, ambaye alitwaa tuzo ya mchezaji aliyekusanya ribaundi nyingi zaidi kwa misimu saba mfululizo kuanzia 1992 hadi 1998, anashika nafasi inayofuata nyuma ya LeBron akiwa nazo 11,954. LeBron pia ndiye kinara wa muda wote wa Cleveland Cavaliers katika kipengele cha ribaundi akikokusanya 6,190 akiwa na klabu hiyo.
KUZUIA, KUPORA
LeBron alimaliza mechi iliyopita dhidi Portland Trail Blazers akiwa na blocks (kuzuia) 1,193, zinazomfanya kushika nafasi ya 66 katika historia ya NBA. Bo Outlaw na Adonal Foyle nao wana idadi kama hiyo, huku Chris Webber akiwa mbele yao kwa kuwa nazo 1,200.
Katika eneo la uporaji mipira (steals), LeBron anashika nafasi ya sita katika orodha ya wachezaji waliopora mara nyingi zaidi katika historia ya NBA, akifanya hizo 2,430. Gary Payton anashika nafasi iliyo mbele yake akipora 2,445, huku Maurice Cheeks akiwa nyuma yake kwa kuwa nazo 2,310. Rekodi nyingine za LeBron mbali na mafanikio hayo, pia ndiye kinara wa muda wote wa NBA katika michezo mingi zaidi iliyochezwa (1,635), dakika nyingi zaidi alizotumika uwanjani (61,421), mipira mingi zaidi iliyofanikiwa kuingia kikapuni (16,040), majaribio mengi zaidi ya kufunga (31,672), misimu mingi zaidi ya kucheza katika NBA (24).
Pia nyota huyo anashika nafasi ya pili katika idadi ya mipira ya adhabu iliyofanikiwa kuingizwa kikapuni (free throws made) akiwa nayo 8,923 na majaribio ya mipira hiyo (free throws attempted) 12,106. Na katika rekodi za triple-doubles, anashika nafasi ya tano, huku akiwa nafasi ya sita katika idadi ya mipira ya pointi tatu (three-pointers) aliyofanikiwa kufunga.