Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pochettino abatizwa kwa moto

POCHETTINO Pict

Muktasari:

  • Pochettino aliwasili Manchester United akibeba matumaini ya kuanza enzi mpya, kurejesha imani na kuleta mabadiliko katika klabu hiyo. Hata hivyo, matarajio hayo yaligeuka kuwa majanga ndani ya dakika chache, huku mfumo wa timu ukivurugika na kila kitu kuonekana kwenda kombo. Dakika 15 za mwanzo za mchezo zilikuwa za aibu kubwa.

LONDON, ENGLAND: Mashabiki wa Liverpool hawakupoteza muda kuanza kumkejeli Mauricio Pochettino wakati mambo yalipokuwa yakienda mrama kwa Manchester United. Waliimba kwa dhihaka, “Poch ndiye anayeendesha timu”, wakimlenga kocha huyo mpya. Lakini swali ni je, alikuwa akiendesha timu au gari la vichekesho? Uso wa Pochettino uliojaa hasira na kukata tamaa ulieleza kila kitu baada ya kuanza kwa matokeo mabaya zaidi kuwahi kurekodiwa na kocha yeyote wa Manchester United katika kipindi cha miaka 100.

Pochettino aliwasili Manchester United akibeba matumaini ya kuanza enzi mpya, kurejesha imani na kuleta mabadiliko katika klabu hiyo. Hata hivyo, matarajio hayo yaligeuka kuwa majanga ndani ya dakika chache, huku mfumo wa timu ukivurugika na kila kitu kuonekana kwenda kombo. Dakika 15 za mwanzo za mchezo zilikuwa za aibu kubwa.

Akiwa ugenini dhidi ya Liverpool, United ilikuwa tayari imefungwa mabao 2-0, ikabaki na wachezaji 10 baada ya mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu, huku matumaini ya kupata matokeo yakizimika mapema.

Ikiwa Pochettino alikuwa na mashaka kuhusu ukubwa wa kazi inayomkabili, mchezo huo ulimpa picha halisi ya changamoto zilizopo. Ni kweli United ilikuwa na sababu ya kujitetea kwa kucheza karibu mchezo mzima ikiwa na wachezaji 10, lakini timu nyingine zimewahi kukabiliana na hali kama hiyo na kuonyesha upinzani na uimara mkubwa zaidi. Kwa United, wakati ilipoanza kufanya hivyo, mchezo ulikuwa tayari umeamuliwa. Hakuna aliyekuwa akitarajia Pochettino abadilishe mambo mara moja, lakini kiwango kilichoonyeshwa kilikuwa cha kusikitisha.

POCHE 01

Je, Mauricio anajutia uamuzi wake? Bila kujali mshahara anaolipwa, huenda angekuwa na sababu za kujilaumu alipokuwa akitazama timu yake ikichezea kichapo hicho. Hali hiyo ni tofauti kabisa na alipokuwa akiinoa timu ya taifa ya Marekani na kushuhudia ikiichapa Haiti jumla ya mabao 8-0 katika michezo miwili iliyopita wiki iliyopita. Liverpool ingekuwa makini zaidi kutumia nafasi zake, huenda United nayo ingepokea kichapo cha mabao 8-0.

Hata hivyo, mchezo huo ulimalizika kwa United kufungwa mabao 4-0, matokeo yanayofanana na yale yaliyompata Lal Hilditch katika mchezo wake wa kwanza akiwa kocha wa United, ilipofungwa kwa idadi hiyo na Bolton Wanderers Oktoba 1926.

Hilditch alikuwa kocha wa muda ambaye pia alikuwa mchezaji wa timu hiyo. Pochettino, aliyewahi kucheza nafasi ya beki wa kati, huenda alitamani hata kuingia uwanjani kusaidia timu yake, licha ya kuwa na umri wa miaka 54. Pengine asingefanya vibaya zaidi ya wachezaji aliokuwa akiwaangalia.

POCHE 03

Hata hivyo, Pochettino naye hawezi kukwepa lawama. Uamuzi wake wa kumwacha Harry Maguire nje ya kikosi cha kwanza uliibua maswali, hasa baada ya kulazimika kumuingiza dakika ya 22. Nafasi yake ilichukuliwa na Matthijs de Ligt, ambaye alikuwa akianza kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu England baada ya siku 357. Hata hivyo, De Ligt alihusika katika bao la kwanza na kwa kiasi kikubwa pia la pili.

Pia, kulikuwa na mkanganyiko kuhusu mfumo alioutumia Pochettino. Je, alianza na mabeki watatu au wanne? Hata wachezaji walionekana kutokuwa na uhakika, kabla ya mfumo huo hatimaye kuishia kuwa wa mabeki watano.

Lakini tatizo la United halikuwa la mtu mmoja. Lilikuwa ni kushindwa kwa pamoja, kuanzia viongozi wa juu wa klabu hadi wachezaji waliokuwa uwanjani. Hata mkurugenzi wa masuala ya soka, Jason Wilcox, alionekana kwenye kamera akiwa ameinamisha kichwa ndani ya koti lake, ishara iliyoakisi hali ya kukatisha tamaa iliyokuwa ikiikabili klabu hiyo.

Pochettino amekuwa akisisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni mzuri ndani ya timu. Sasa ana kazi ya kuondoa vichekesho na vurugu zilizotawala, kurejesha nidhamu na kuijengea upya United heshima na uaminifu.

POCHE 02

United imejikuta katika vita ya kuwania kusalia Ligi Kuu England, jambo ambalo halipaswi kupuuzwa. Ikiwa na pointi nane baada ya michezo 11, mwenendo wake wa sasa unaashiria huenda ikamaliza msimu ikiwa na chini ya pointi 28. Hiyo ni wastani mbaya zaidi wa pointi kwa kila mchezo ikilinganishwa na msimu iliposhuka daraja mwaka 1974, ilipokusanya pointi 32 katika michezo 42.

Kazi inayomkabili Pochettino ni kubwa mno. Mkakati wa usajili wa United umekuwa mgumu kueleweka, baada ya klabu hiyo kuamua kuimarisha safu ya ushambuliaji mwaka uliopita, kiungo msimu huu wa kiangazi na kusubiri hadi mwaka ujao kufanya marekebisho katika safu ya ulinzi.

Mapungufu ya mkakati huo yameonekana wazi kutokana na United kuruhusu mabao 34 msimu huu, ikiwa ni idadi kubwa zaidi miongoni mwa timu zinazoshiriki ligi tano kubwa za Ulaya.

POCHE 04

United inaweza kujitetea, na kwa kiasi fulani ina hoja, kwamba kadi nyekundu aliyoonyeshwa Leny Yoro dakika ya nane kwa kumzuia mpinzani aliyekuwa kwenye nafasi ya kufunga ilikuwa kali. Hii ni kutokana na Alexander Isak kuonekana tayari amepoteza udhibiti wa mpira.

Hata hivyo, Yoro alikuwa akifikiria nini alipomwangusha mshambuliaji huyo kutoka nyuma? Na De Ligt alikuwa akifanya nini aliposhindwa kufuatilia harakati za Ronald Araújo, aliyepokea pasi ndefu na kuanzisha shambulizi lililoleta hatari langoni mwa United?

Vipi kuhusu ukuta wa kujilinda wa United uliokuwa katika hali ya ovyo wakati wa mpira wa adhabu? Bruno Fernandes alionekana kujaribu kuzuia mpira kwa mguu, huku Dominik Szoboszlai akishangazwa na nafasi aliyoipata. Kiungo huyo wa Liverpool hakufanya kosa, akapiga mpira wa chini ulioishia moja kwa moja wavuni.

Bao la pili lilidhihirisha zaidi udhaifu wa safu ya ulinzi ya United. Rio Ngumoha alimzidi kwa urahisi Diogo Dalot, jambo ambalo halikuwa la kwanza wala la mwisho katika mchezo huo, kabla ya kupiga krosi iliyomkuta Florian Wirtz, aliyeumalizia mpira kwa kuugonga na kuuingiza wavuni kupitia mwamba wa juu. De Ligt naye alionekana kupoteza mwelekeo, akishindwa kudhibiti hali ya hatari iliyokuwa mbele yake.

POCHE 05

Inaweza kusemwa kuwa baada ya mwanzo huo mbaya, Pochettino alifanikiwa kuzuia United kuendelea kuruhusu mabao mengi zaidi. Hata hivyo, hilo huenda lilichangiwa pia na Liverpool kushindwa kutumia vyema nafasi ilizopata na kutokuwa na makali ya kutosha katika kumalizia mashambulizi.

Kipindi cha pili kilipoanza, mashabiki wa Liverpool waliokuwa upande wa Kop walianza kuimba kwa nguvu wakitaka timu yao ishambulie zaidi.

“Shambulieni, shambulieni, shambulieni,” ilikuwa ni sauti ya mashabiki waliotaka mabao zaidi, aibu zaidi kwa wapinzani wao na pengine kurudiwa kwa ushindi wa mabao 7-0 walioupata miaka mitatu iliyopita.

Liverpool ilipoteza nafasi kadhaa za wazi. Bradley Barcola alishindwa kudhibiti mpira na kuutoa nje wakati akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, huku Isak akipiga shuti lililopaa nje ya lango wakati akiwa amebaki kumkabili kipa Senne Lammens pekee.

Hata hivyo, bao la tatu lilipatikana baada ya Barcola kumzidi kwa urahisi Lisandro Martínez, ambaye alionekana kukata tamaa ya kuendelea kumzuia. Barcola alitumia kasi yake upande wa kulia kabla ya kupiga krosi ya chini iliyomkuta Ngumoha, aliyekuwa mmoja wa wachezaji bora wa Liverpool katika mchezo huo, na kuumalizia wavuni.

Kabla hata kipenga cha mwisho hakijapulizwa, baadhi ya mashabiki waaminifu wa United walianza kuondoka uwanjani. Wengine walionekana hata kugombana wao kwa wao, huku wakikosa kushuhudia bao la nne.

Bao hilo lilipatikana baada ya United kupoteza mpira kizembe. Mchezaji wa akiba Víctor Muñoz alicheza pasi za haraka na Wirtz kabla ya kupiga shuti maridadi lililopita pembeni ya Lammens na kuingia wavuni.

Mashabiki wa Liverpool waliendelea kuwakejeli wapinzani wao kwa kuimba, “Mnashuka daraja, mnashuka daraja,” kabla ya kuongeza, “Hamna tena umaarufu.”

Huenda United bado ni klabu kubwa kwa historia na jina lake, lakini kiwango ilichoonyesha katika mchezo huo kimeifanya kujikuta kwenye orodha ya timu zinazozungumziwa zaidi kwa sababu mbaya.