Mauaji Ngumoha aivunja rekodi ya Owen
Muktasari:
- Baadaye, wimbo mwingine kutoka enzi za bendi ya Duran Duran ulipamba uwanja. Hata hivyo, mashabiki wa eneo hilo wameubadilisha na kuupa maana mpya ili kuendana na hatua kubwa anazopiga kijana mwenye kipaji kikubwa katika safari yake ya soka.
LIVERPOOL, ENGLAND: ILIKUWA siku ya burudani iliyowalazimu ma-DJ wa uwanja kurejea nyimbo za zamani zilizowahi kuteka hisia za mashabiki. Wimbo wa Three Little Birds wa Bob Marley ulipigwa baada ya kipenga cha mwisho, huku You’ll Never Walk Alone ukianza kusikika baada ya kocha Andoni Iraola kuonyesha furaha yake na kushangiliwa na mashabiki waliomtaka mara tatu anyanyue ngumi yake kuelekea upande wa Kop kusherehekea ushindi.
Baadaye, wimbo mwingine kutoka enzi za bendi ya Duran Duran ulipamba uwanja. Hata hivyo, mashabiki wa eneo hilo wameubadilisha na kuupa maana mpya ili kuendana na hatua kubwa anazopiga kijana mwenye kipaji kikubwa katika safari yake ya soka.
“Jina lake ni Rio na anacheza kwa ustadi mkubwa pembeni ya uwanja!” alisikika shabiki mmoja mwenye furaha akisema alipokuwa akipanda ngazi za jukwaa kuu. Hakika, maneno hayo yalikuwa na uhalisia mkubwa yakielezea dakika 78 za kusisimua alizoonyesha mchezaji huyo mwenye jezi namba 73 ya Liverpool.
Rio Ngumoha ana safari kubwa mbele yake, jambo ambalo limekuwa likidhihirika katika kipindi cha miezi 18 iliyopita. Hata hivyo, katika kipindi hiki cha vuli, kiwango chake kimepanda zaidi na alithibitisha hilo katika mchezo ambao Manchester United ilikumbana na kipigo kikubwa.
Si rahisi kwa mchezaji chipukizi kuonyesha kiwango cha juu katika michezo yenye presha kubwa. Ni kweli United iliyofika Merseyside ilikuwa katika kiwango kibaya zaidi kuwahi kuonekana kwa muda mrefu, lakini hilo halikumaanisha kwamba Ngumoha angekuwa na siku rahisi ya kucheza kwa uhuru. Wala haikuwa na uhakika kwamba Liverpool ingeshinda mchezo huo.
Hata hivyo, Ngumoha alianza kwa kuutafuta mpira na mara moja akaanza kumtesa beki Diogo Dalot. Alimchezesha upande mmoja, akageuka upande mwingine na kumwacha beki huyo akionekana kuchanganyikiwa, kiasi cha kufanana na wahusika wa katuni wanaozungukwa na ndege kichwani baada ya kuzungushwa sana.
“Napokutana na beki yeyote, napenda kumkabili moja kwa moja na kucheza bila hofu,” alisema Ngumoha, ambaye kwa sasa anajijengea nafasi katika kikosi cha timu ya taifa ya England.
“Ulikuwa mchezo mzuri na nilichokifanya ni kuisaidia timu kupata pointi tatu. Hilo linanifurahisha.”
Katika dakika 15 za mwanzo, wakati United ikianza kuporomoka, Ngumoha alikuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia zaidi. Moja ya matukio yake bora ilikuwa pale alipomzidi Dalot kwa kuingia ndani kabla ya kupiga krosi iliyomkuta Florian Wirtz. Kiungo huyo alimalizia kwa ustadi mkubwa, akizunguka hewani na kuutumbukiza mpira wavuni kwa mguu wa kushoto, bao lililozua shangwe na mshangao kwa mashabiki.
Liverpool ilipokuwa mbele kwa mabao 2-0 huku United ikiwa imepungukiwa mchezaji mmoja, kulikuwa na swali kama wenyeji wangeweza kuvuka rekodi ya ushindi wa mabao 7-0 walioupata Machi 2023. Hata hivyo, Mauricio Pochettino alifanikiwa kuzuia timu yake kuendelea kuruhusu mabao kwa urahisi na kufanya mchezo kupoteza kasi yake ya awali.
Mchezo ulipozidi kukosa mtiririko kutokana na kusimama na kuanza mara kwa mara, baada ya dakika 57 mashabiki wa Kop walianza kuisukuma Liverpool kwa kuimba, “Shambulieni, shambulieni, shambulieni.” Hapo ndipo Ngumoha alipoacha alama nyingine muhimu katika mchezo huo.
Alifika eneo la mbali la lango na kuumalizia kwa bao krosi ya Bradley Barcola. Lilikuwa bao lililoongeza nguvu kwa Liverpool na kuondoa presha iliyokuwa imeanza kujitokeza. Zaidi ya hapo, lilimwingiza Ngumoha katika vitabu vya historia.
Alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao katika mchezo wa Liverpool dhidi ya Manchester United katika historia ya klabu hiyo, akiwapita mastaa waliowahi kuitumikia timu hiyo kama Michael Owen, Robbie Fowler na Steven Gerrard.
Pia, alikuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri wa miaka 18 kufunga bao na kutoa asisti katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu England tangu Owen alipofanya hivyo Desemba 1997.
“Hiki anachokifanya mtoto huyu si cha kawaida,” alisema Daniel Sturridge, ambaye anafahamu vizuri maana ya kuamua matokeo ya mchezo huu mkubwa, wakati akichambua mchezo huo katika studio za Sky Sports.
“Huwezi kumfundisha mtu kipaji cha aina hii.”
Hata hivyo, jambo muhimu zaidi ni kwamba Ngumoha bado anaendelea kujifunza na kukua kwa kasi. Historia ya soka imejaa mifano ya wachezaji vijana wanaoanza kwa kuvutia sana, lakini baadaye wanashindwa kuendeleza viwango vyao kwa sababu ya kukosa uwezo wa kujifunza na kubadilika kulingana na changamoto mpya.
‘NGUMOHA NI MGUMU KUMZUIA’
Mwanzoni mwa msimu huu, kila mtu alikuwa akijua kwamba Ngumoha ana mbinu ya kucheza inayohusisha kumdanganya beki kwa kukanyaga mpira na kuubadilisha mwelekeo kabla ya kuingia ndani na kupiga shuti.
Lakini swali lilikuwa, angefanya nini pale makocha wa timu pinzani watakapoanza kumtambua kama tishio na kuweka mikakati maalumu ya kumzuia?
“Nadhani Rio ni mchezaji ambaye ukiweza kumweka katika mazingira ambayo wapinzani hawawezi kumsaidia beki wao wa pembeni kumdhibiti, inakuwa vigumu sana kumzuia, hasa ndani ya eneo la hatari kwa sababu anaweza kutumia miguu yote miwili,” alisema Iraola.
“Ulikuwa mchezo mzuri. Wachezaji kama Rio na Florian, timu inapoweza kudhibiti mchezo, wanapata nafasi kubwa ya kumiliki mpira.”
Miongoni mwa michezo iliyokuwa na umuhimu mkubwa katika maendeleo yake ni ule wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Villarreal, ambao Liverpool ilishinda kwa mabao 4-3. Katika mchezo huo, alianza kuingia zaidi ndani ya eneo la hatari, akatumia vizuri zaidi nafasi za kumiliki mpira na, jambo muhimu zaidi, akaanza kufanya maamuzi sahihi.
Mchezo dhidi ya Manchester United ulikuwa hatua nyingine muhimu katika safari yake ya kukua kisoka. Inahitaji ujasiri na kujiamini kuendelea kuutafuta mpira wakati macho ya dunia nzima yameelekezwa kwako. Hata hivyo, Ngumoha amekuwa akiwavutia mashabiki na wachezaji wenzake kutokana na namna anavyocheza kwa uhuru na bila kuonyesha hofu.
“Ni vizuri kufunga bao, hasa katika mchezo mkubwa kama huu wa Liverpool dhidi ya United, ambao ni mchezo mkubwa zaidi England,” alisema Ngumoha.
“Kufanikiwa kufanya hivyo na kumpita mtu kama Michael Owen ni jambo la kipekee sana. Nina furaha.”
Hakika anapaswa kufurahi. Ikiwa ataendelea kucheza kwa kiwango hiki, mashabiki wa Liverpool wataendelea kuliimba jina lake kwa miaka mingi ijayo.
CHIPUKIZI WALIOFUNGA
Liverpool v Manchester United
Rio Ngumoha (Liverpool) Miaka 18, siku 85
Michael Owen (Liverpool) Miaka 18, siku 117
Kobbie Mainoo (Man United) Miaka 18, siku 354
Wayne Rooney (Man United) Miaka 19, siku 83
Anthony Martial (Man United) Miaka 19, siku 281
Ryan Giggs (Man United) Miaka 20, siku 36