Nani bado anamtaka Sterling Ulaya?
Muktasari:
- Sterling ana umri mdogo kwa miezi 16 kuliko Harry Kane, ambaye anaendelea kuvunja rekodi akiwa nahodha wa England na alifikisha rekodi yake binafsi ya mabao 73 msimu uliopita.
LONDON, ENGLAND: KATIKA ulimwengu mwingine, ambako maisha ya wachezaji yangechukua mwelekeo tofauti, Raheem Sterling angekuwa sehemu ya kikosi cha England sasa, akicheza chini ya kocha Thomas Tuchel, ambaye alimfanya kuwa mchezaji wa kwanza aliyelenga kumsajili katika enzi mpya ya Chelsea baada ya Todd Boehly na Clearlake Capital kuchukua umiliki wa klabu hiyo.
Sterling ana umri mdogo kwa miezi 16 kuliko Harry Kane, ambaye anaendelea kuvunja rekodi akiwa nahodha wa England na alifikisha rekodi yake binafsi ya mabao 73 msimu uliopita.
Sterling, kwa upande mwingine, hana klabu na anasubiri hukumu baada ya kukiri kuwa na hatia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Basingstoke kwa makosa ya kuendesha gari kwa njia hatarishi na umiliki oksidi ya nitrous (nusu dawa ya kulevya), kufuatia tukio ambalo mashahidi walihofia lingeweza kusababisha mtu kupoteza maisha.
Mastaa hao wawili, Kane na Sterling, kwa nini maisha yao ya soka yamekwenda tofauti kwa kiwango hiki? Kwa nini Kane anaendelea kufanya vizuri wakati Sterling anapitia anguko la kusikitisha na la kutisha nje ya uwanja?
Vyanzo kadhaa vilivyoomba majina yao yasitajwe ili kulinda uhusiano wao, vimeeleza picha tata kuhusu Sterling kwa The Guardian ya Uingereza kimoja kikimtaja kama “roho iliyopotea”, huku kingine kikiamini kuwa “amepotoshwa sana” katika maisha na kazi yake. Ili kuelewa anguko lake, ni muhimu kukumbuka ukubwa wa safari yake ya mafanikio.
MTU KAZI
Wale walioshuhudia kupanda kwa Sterling kutoka kuwa mtoto aliyekuwa akimsaidia mama yake katika kazi za usafi huko Stonebridge, hadi kuwa mwanasoka mwenye kipaji kikubwa katika akademi ya Queens Park Rangers (QPR), kisha kuingia katika kikosi cha kwanza cha Liverpool akiwa na miaka 17 wanamkumbuka kama mchezaji aliyeonekana kuwa na kila kitu kilichohitajika ili kufanikiwa.
“Raheem alikua na kujiamini,” anasema Mark Anderson, skauti wa watoto wa Liverpool aliyeishawishi klabu hiyo kumsajili akiwa mmoja wa vijana wenye umri wa miaka 15 waliogharimu fedha nyingi zaidi.
“Alikuwa akicheza kwa shauku na malengo. Tangu mara ya kwanza nilipomuona nilifikiri alikuwa na kila kitu cha kuwa mchezaji wa kiwango cha timu ya taifa.”
Sterling alianza haraka kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Liverpool, ambako wachezaji walishangazwa na ukweli kwamba nyota huyo mwembamba alikuwa na nguvu za asili zilizozidi hata za watu wazima wengi. Hakuonekana mara kwa mara kwenye uwanja wa mazoezi, lakini aliweza kukabiliana na mastaa kama Martin Skrtel, Mamadou Sakho na Kolo Toure ambao walikuwa wakubwa zaidi kimwili kuliko yeye.
“Raheem alikuwa mzuri zaidi kiakili kuliko ambavyo baadhi ya watu wangeweza kudhani,” Steven Gerrard aliandika katika kitabu chake My Story, akikiri kwamba yeye na Jamie Carragher hawakumpa nafasi nyepesi wakati wa mazoezi.
Ustahimilivu wa Sterling ulijaribiwa alipokataa mkataba wa mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki na kujikuta akizungukwa na mvutano mkubwa. Hilo ndilo jambo lililobadilisha namna alivyotazamwa; kutoka kuwa kipaji kikubwa zaidi cha England hadi kuonekana mwanasoka kijana mwenye majivuno; iwe ni kweli au la.
Sterling alifanyiwa mahojiano kwa BBC akisisitiza kwamba hakuwa “kijana mwenye tamaa ya fedha mwenye umri wa miaka 20”.
Wachambuzi waliokuwa wakiunga mkono Liverpool wakamgeukia. Mambo yalizidi kuwa mabaya pale wakala wake wakati huo, Aidy Ward, alipoiambia Evening Standard kwamba Sterling asingesaini mkataba mpya hata kama angepewa karibu Pauni 1 milioni kwa wiki. Liverpool ilimuuza Manchester City kwa Pauni 44 milioni katika majira hayo ya kiangazi.
Mtazamo wa umma ulikuwa umeanza kubadilika kutoka kuwa mchezaji wa tano kwa umri mdogo zaidi kucheza mechi yake ya kwanza kwa England hadi kuwa mchezaji aliyemwambia kocha wa timu hiyo ya taifa, Roy Hodgson, kwamba alikuwa amechoka sana kucheza dhidi ya Estonia na picha za kwanza za Sterling akivuta hewa kutoka kwenye puto iliyodaiwa kuwa na ‘oksidi ya nitrous’ zilijitokeza mwaka 2015.
MAISHA MAPYA
Kuondoka Liverpool kulizidisha hali hiyo, na taswira hiyo imeendelea kumwandama. Hasa akiwa na England, ambako alifanywa kuwa chanzo cha lawama baada ya timu hiyo kutolewa katika hatua ya 16 bora ya Euro 2016 dhidi ya Iceland. Unyanyasaji alioupata ulikuwa mkubwa kiasi kwamba Sterling aliibuka na hashtag #TheHatedOne# kwenye Instagram. Hapo alikuwa na umri wa miaka 21.
Ndani ya miaka miwili alikuwa mwathirika wa shambulio lililokuwa na chuki ya kibaguzi nje ya uwanja wa mazoezi wa Manchester City, na pia alitukanwa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi na mashabiki wa Chelsea wakati wa mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Katika kilele cha kiwango chake, alikuwa mchezaji wa kuvutia sana. Mwaka 2019, alishinda mataji matatu ya ndani akiwa na City, akafunga mabao mawili katika fainali ya FA Cup na mkwaju wa ushindi katika mikwaju ya penalti ya fainali ya Carabao, na akatwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo England (FWA).
Mwaka mmoja baadaye, Xavi Hernandez alisema Sterling alikuwa bora kiasi kwamba “atishinda mbio” za kuwarithi Lionel Messi na Cristiano Ronaldo na kwamba alikuwa ni mchezaji wa mitaani aliyetengenezwa na mifumo thabiti ya Pep Guardiola. Kufikia 2021 alikuwa amemaliza mara mbili ndani ya 15 bora katika upigaji kura wa Ballon d’Or.
Huyo alikuwa mchezaji aliyeendelea kufanya vizuri wakati muhimu England ilipofika fainali ya Euro 2020; akifunga mabao mawili pekee katika hatua ya makundi; moja dhidi ya Ujerumani katika hatua ya 16 bora na akasababisha penalti iliyozaa bao la ushindi dhidi ya Denmark katika nusu fainali. Lakini hata jitihada zake za kufanya mambo mazuri zilionekana kuwafanya baadhi ya watu wamgeukie.
Hata hivyo, alikuwa mmoja wa watu muhimu waliokuwa wakikemea ubaguzi wa rangi katika jamii, hasa baada ya namna alivyoonyeshwa na vyombo vya habari kufuatia kukosolewa kwa kununua nyumba kwa ajili ya mama yake. Mwaka 2020, alirekodi video ya kupinga ubaguzi wa rangi akisema: “Sitachukia kamwe kuwa mweusi,” huku akiwatumia ujumbe mastaa wenzake akiwamo Kevin De Bruyne, David Alaba na Jordan Henderson, kuwaomba washiriki katika video hiyo.
KAZI INAENDELEA
Mwaka mmoja baadaye alipewa tuzo ya MBE. Ikiwa kuna chochote, jambo hilo lilionekana kuwafanya baadhi ya watu ambao hawakumfahamu Sterling binafsi kumpinga kwa nguvu zaidi.
Chanzo kimoja kilichowahi kufanya kazi kwa karibu na Sterling kinamuelezea kama mstaarabu na mwenye mvuto, kikisema: “Haonekani kuwa mwenye majivuno au dharau. Ni mtu mzuri, mwenye aibu. Kwa kiasi fulani ni mtu mwenye haya.”
Katika baadhi ya maeneo, kumekuwa na aina fulani ya furaha ya kuona namna maisha yake ya soka yalivyoporomoka kwa kasi baada ya kujiunga na Chelsea. Alikuwa ameshinda karibu kila kitu na akiwa na miaka 27, alikuwa akiingia katika kipindi ambacho wachezaji wengi hufikia kilele cha viwango vyao.
Sterling ndiye mchezaji ambaye Tuchel alimwambia Boehly apewe kipaumbele na bilionea huyo wa Marekani alivutiwa na uwezekano wa kumfanya mshambuliaji huyo, ambaye alikuwa ametoka kushinda taji lake la nne la Ligi Kuu England ndani ya miaka mitano, kuwa usajili wao mkubwa.
Sterling alisaini mkataba wa miaka mitano wenye mshahara wa Pauni 325,000 kwa wiki, na Tuchel alifukuzwa kazi wiki saba baadaye.
Katika miaka iliyofuata, Sterling alicheza chini ya makocha Graham Potter, Frank Lampard, Mauricio Pochettino na Enzo Maresca.
Chanzo kimoja kinajiuliza kama kuondoka kwenye mifumo thabiti ya Brendan Rodgers huko Liverpool na Guardiola ndani ya Manchester City na kwenda katika mazingira yenye vurugu Chelsea kulimpoteza.
Kutoka kwenye takwimu za kushangaza alizokuwa akizalisha City; mabao 23 na asisti 14 msimu wa 2017-18, mabao 25 na asisti 16 ule wa 2018-19, na mabao 31 na asisti 10 msimu wa 2019-20, kiwango chake kilianza kushuka. Uamuzi wa pamoja ulifanyika Chelsea katika majira ya kiangazi ya 2024 wa kumuuza ukizingatia maisha yake binafsi na uwezo wake wa kucheza katika kikosi.
MAMBO MAGUMU
Katika wiki iliyokuwa ngumu sana, siku mbili kabla ya kuanza kwa msimu wa 2024-25, Maresca alimwambia Sterling kwamba hakuwa sehemu ya mipango yake na hakumjumuisha katika kikosi kilichocheza dhidi ya Manchester City wala katika mchezo wa Conference League dhidi ya Servette, ambako Pedro Neto alivalia jezi yake namba 7. Sterling alilazimika kufanya mazoezi mbali na kikosi cha kwanza.
Inaonekana kwamba Sterling pia hakuwa hana kosa kabisa katika suala hilo. The Guardian liliambiwa kwamba alijulikana kufika mazoezini akiwa amechelewa wakati alipaswa kuwa mfano kwa wengine, ingawa vyanzo vilivyo karibu na Sterling vilidai hakuwahi kupewa adhabu rasmi iliyoandikwa akiwa Chelsea.
Hatua alizochukuliwa hatimaye zilikuwa kali, ingawa inaeleweka kwamba Maresca aliwafanyia tathmini mawinga wake katika mechi za kirafiki kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho. Sterling aliweka wazi kwamba alitaka kubaki London kwa ajili ya familia yake, na Chelsea kwa kusita ikakubali kumtoa kwa mkopo kwenda Arsenal. Huko alifunga bao moja pekee, katika mchezo wa Carabao Cup dhidi ya Bolton ya League One Septemba 25, 2024, ambalo ndilo bao lake la mwisho katika soka la kulipwa.
Aliporejea Chelsea, vyanzo vilidai aliambiwa akae mbali na maeneo muhimu ya mazoezi ya klabu hiyo, Cobham, ingawa chanzo cha Chelsea kilikanusha kwamba hali hiyo haikutokea. Sterling alikataa ofa ya mkopo kutoka Juventus, lakini kufikia Januari, baada ya kukaa miezi sita bila kucheza alihitaji kuondoka kwa ajili ya kuokoa maisha yake ya soka.
Chelsea ilikubali kununua miezi 18 iliyokuwa imebaki katika mkataba wake kwa ada iliyopunguzwa. Taarifa ya klabu iliyotangaza kuondoka kwake ilikuwa na maneno 23 pekee. Sterling alichagua kujijenga upya chini ya Robin van Persie huko Feyenoord. Ilikuwa janga; alidhihakiwa bila huruma kwenye mitandao ya kijamii na mashabiki wa klabu hiyo, huku akichekwa uwanjani. Chanzo kimoja kilichowahi kufanya kazi na Sterling kililinganisha mwelekeo wa maisha yake ya soka na ule wa Michael Owen; vipaji viwili vilivyoibuka vikiwa na umri mdogo, ambavyo kasi ilikuwa moja ya silaha kubwa, lakini maisha yao ya soka yakaanza kufifia kasi hiyo ilipopungua.
Owen alicheza msimu wake wa mwisho Stoke City, akicheza mechi nane za Ligi Kuu England akitokea benchi, na kustaafu akiwa na miaka 33. Sterling atatimiza umri wa miaka 32 mwezi Desemba, mwaka huu.
Chanzo kingine kinajiuliza kama kushinda vitu vingi na kupata fedha nyingi kulipunguza bidii yake iliyohitajika ili kuendelea kuwa kileleni.
Sterling alirejea nyumbani England kutoka Uholanzi na, siku 11 baadaye, akaendesha Lamborghini yake kwa zaidi ya saa moja kwenye barabara moja wakati wa msongamano wa magari huku akivuta oksidi ya nitrous kutoka kwenye puto. Ilionekana kama kilio cha kuomba msaada.
Alipokamatwa mwezi Mei, aliwaambia maofisa wa polisi kwamba alikuwa na “tatizo” la oksidi ya nitrous; kauli nzito kutoka kwa mwanasoka ambaye bado alikuwa na matumaini ya kucheza tena.
“Ni jambo la kusikitisha kuona mtu akipambana na hali hiyo, kwa sababu alikuwa baba aliyejitolea kwa watoto wake na alikuwa mtu wa familia, mtu mzuri wa kuwa naye,” alisema Tuchel hivi karibuni.
“Inaonekana tu kwamba anapitia kipindi kigumu. Sina uhakika ni kwa kiasi gani ni kosa lake; wakati mwingine unaingia tu katika mzunguko wa ajabu katika maisha yako, mzunguko wa kushuka. Bila shaka, mawazo yetu yako pamoja naye. Imani ni kwamba anaweza kubadilisha hali hii.”
Akiwa amesimama kizimbani mahakamani akiwa amevaa mavazi meusi mwezi uliopita, wakati Liverpool ilikuwa ikijiandaa kwa mchezo wa Carabao dhidi ya Tottenham Hotspur, Sterling aliambiwa kwamba anakabiliwa na uwezekano wa kufungwa jela wakati mahakama itakapokutana tena Novemba, mwaka huu.
“Kabla hajawa Raheem Sterling, mwanasoka wa kimataifa, mchezaji wa Ligi Kuu England na jina ambalo kila mtu alilijua, alikuwa tu kijana mdogo mwenye mpira ambaye mtu fulani alipaswa kumwamini,” anasema Anderson. Je, bado kuna mtu atakayemwamini sasa?