Pauni 1 trilioni za usajili zampa presha De Zerbi
Muktasari:
- Tottenham iliingia kwenye msimu ikiwa na matumaini makubwa baada ya kufanya usajili mkubwa, huku mashabiki wakitarajia kuona timu ikirejea kwenye mbio za nafasi za juu na hata kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
LONDON, ENGLAND: Kocha wa Tottenham Hotspur, Roberto De Zerbi ameanza kuingia kwenye presha baada ya timu hiyo kuanza vibaya msimu mpya wa Ligi Kuu England, licha ya kutumia Pauni milioni 332 (zaidi ya Sh1.1 trilioni) kusajili wachezaji wapya 10.
Tottenham iliingia kwenye msimu ikiwa na matumaini makubwa baada ya kufanya usajili mkubwa, huku mashabiki wakitarajia kuona timu ikirejea kwenye mbio za nafasi za juu na hata kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti baada ya Spurs kushindwa kushinda katika mechi zake tatu za kwanza za ligi na haijafunga bao hata moja.
Timu hiyo ilipoteza dhidi ya Brentford na Newcastle United, kabla ya kupata pointi yake ya kwanza baada ya kutoka sare ya bila mabao dhidi ya Nottingham Forest.
Katika mchezo huo dhidi ya Forest, Tottenham ilishindwa hata kupiga shuti moja lililolenga lango, jambo ambalo halikuwa limetokea kwao katika mchezo wa ligi kwa zaidi ya miaka minne.
Tatizo la Spurs si kufunga pekee, bali pia kushindwa kutengeneza nafasi hatari. Takwimu zinaonyesha timu hiyo ipo chini kabisa kwa ubora wa mashuti, huku ikiwa ya tatu kutoka chini kwa jumla ya mabao yanayotarajiwa kufungwa (xG).
De Zerbi pia amekuwa akibadilisha safu yake ya ushambuliaji mara kwa mara. Katika mechi tatu za mwanzo, ametumia mchanganyiko tofauti wa washambuliaji, huku katika mechi 10 za ligi tangu aanze kuinoa Tottenham akiwa ametumia wachezaji 10 tofauti kwenye nafasi tatu za mbele.
Hali hiyo imechangiwa na majeraha na kutokuwa fiti kwa baadhi ya wachezaji muhimu, akiwamo Mohammed Kudus, Dejan Kulusevski na James Maddison.
Mbali na tatizo la ushambuliaji, Tottenham pia imeshuka katika kiwango cha kukimbia na kushindana kimwili. Imezidiwa kwa umbali wa kukimbia katika mechi zote tatu za ligi.
Pamoja na mwanzo huo mbaya, De Zerbi bado anaonekana kupewa muda kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika ndani ya kikosi. Hata hivyo, matumizi makubwa ya fedha yanamlazimisha kuanza kuonyesha maendeleo, huku mchezo dhidi ya Everton ukiwa mtihani mwingine muhimu kwake.