Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Paul Scholes awakataa Caicedo, Rice, akomaa na Sandro Tonali

Muktasari:

  • Ingawa msimu wa Ligi Kuu ya EPL una mechi saba hadi sasa, lakini mjadala kuhusu nani kiungo bora zaidi umechukua nafasi kwa wachambuzi wa soka. Wachezaji kama Caicedo na Rice wamevutia mashabiki kwa kuonyesha kiwango kizuri.

Wiki iliyopita gwiji wa Manchester United, Paul Scholes alimsifu Sandro Tonali kama kiungo bora zaidi katika Ligi Kuu ya England kwa sasa, na kumpa nafasi ya juu zaidi kuliko Moisés Caicedo wa Chelsea na Declan Rice wa Arsenal.

Ingawa msimu wa Ligi Kuu ya EPL una mechi saba hadi sasa, lakini mjadala kuhusu nani kiungo bora zaidi umechukua nafasi kwa wachambuzi wa soka. Wachezaji kama Caicedo na Rice wamevutia mashabiki kwa kuonyesha kiwango kizuri.

Hata hivyo, Scholes anaamini kuwa Caicedo si kiungo wa mwenye sifa zote, ingawa amekiri kiungo huyo raia wa Ecuador ni mzuri sana katika kuvuruga mipango ya timu pinzani.

Katika mazungumzo ya kwenye kipindi cha The Overlap, beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher amemuuliza Scholes ni nani kiungo bora zaidi wa Ligi Kuu ya EPL kwa sasa, naye amejibu: "Kwa sasa? Hilo ni gumu. Bado simuoni Moisés Caicedo kama kiungo mwenye sifa zote. Najua alifunga bao zuri na alicheza vizuri sana Jumamosi. Nililaumiwa sana mwaka jana kwa kumkosoa na nilikuwa karibu kubadilisha msimamo wangu kwa sababu alikuwa mzuri sana kwenye Kombe la Dunia la Klabu."

Scholes amesisitiza kuwa ingawa Caicedo ni mahiri kwenye upande wa ulinzi, lakini anakosa ubunifu na ustadi wa kiufundi unaomtambulisha kiungo kamili.

"Mimi hupendelea viungo wanaotawala mchezo, wanaocheza kwa mtindo mzuri na wanaofunga mabao mara kwa mara kuliko Caicedo. Ni kweli alifunga bao zuri, lakini huwezi kushangaa kama hatarudia tena hadi baada ya miezi 18. Yeye ni bora sana katika kazi yake ya kuvuruga mipango ya timu pinzani, hana mpinzani katika mbinu hiyo. Lakini napendelea aina nyingine ya viungo."

Nguli huyo wa Manchester United ameendelea kumsifia Alexis Mac Allister wa Liverpool kabla ya kumtaja Tonali kama chaguo lake la kwanza.

"Alexis Mac Allister alikuwa mzuri sana msimu uliopita, alidhibiti mipango ya wapinzani katika mechi nyingi, nafikiri Liverpool wanamkosa kwa sasa.

"Nampenda pia Sandro Tonali. Amekuwa mzuri sana. Ningemchagua Tonali kwa sasa," Scholes amebainisha.

Tonali alijiunga na Newcastle akitokea AC Milan mwaka 2023 kwa ada ya takribani Pauni 58.9 milioni. Hata hivyo, kiungo huyo kutoka Italia bado hajafunga bao lolote kwenye Ligi Kuu ya EPL msimu huu 2025/26, akiwa ametoa pasi moja ya bao pekee hadi sasa.

"Nafikiri ana kila kitu," Scholes amesitiza msimamo wake kuhusu Tonali kuwa kiungo bora zaidi Ligi Kuu ya EPL.

Uamuzi wa Scholes kumtaja Tonali kama kiungo bora zaidi wa Ligi Kuu kwa sasa uliwashangaza wengi. Alipoulizwa kama kweli alimaanisha hivyo, Scholes amesisitiza msimamo wake: "Ndiyo, mtasema Declan Rice, lakini nafikiri Tonali ni bora zaidi ya Rice. Nampenda Rice, nisieleweke vibaya, nafikiri ana kila kitu.

"Wakati mwingine anachukua muda mwingi na mpira na anajaribu kuwa na mtindo zaidi ya inavyohitajika. Anaweza kufanya kila kitu lakini sioni akifanya hayo vya kutosha. Napendelea Tonali, lakini wote ni wachezaji wazuri."