Pacha wa Man United wanaotikisa Cameroon
Muktasari:
- Wachezaji hao wenye umri wa miaka 16, ambao wote ni viungo, wanaiwakilisha Cameroon katika mashindano hayo huku pia wakiwa wanacheza pamoja katika klabu ya Manchester United ya England.
PACHA wa Cameroon, Douka na Bassirou Nkoto wamekuwa kivutio katika michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17, Qatar 2026, si kwa sababu ya kufanana kwa sura tu, bali pia kutokana na kipaji chao cha soka kinachowakutanisha ndani na nje ya uwanja.
Wachezaji hao wenye umri wa miaka 16, ambao wote ni viungo, wanaiwakilisha Cameroon katika mashindano hayo huku pia wakiwa wanacheza pamoja katika klabu ya Manchester United ya England.
Lakini mashindano hayo yamekuwa na neema ya kushuhudia pacha wengine, Edwin Quintero na Holger Quintero, wanaocheza katika akademi ya Independiente del Valle.
Akizungumza na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Douka alieleza namna undugu wao ulivyo wa tofauti kiasi kwamba wanaweza kuelewana wakiwa uwanjani bila hata kutazamana.
“Tunaweza kuwasiliana bila hata kutazamana,” alisema Douka akielezea uelewano wake na pacha wake.
Kwa upande wake, Bassirou alisema kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi hiyo katika Kombe la Dunia wakiwa pamoja ni jambo kubwa na la kujivunia, akiamini si kila mchezaji hupata fursa hiyo.
“Hili ni jambo kubwa sana kwetu. Si kila mtu hupata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia. Kuwa hapa pamoja ni heshima kubwa,” alisema Bassirou.
Licha ya kucheza nafasi ya kiungo wote wawili, pacha hao wana majukumu tofauti uwanjani. Bassirou hutumika zaidi kama kiungo mshambuliaji wa kati, akitumia uwezo wake wa kupiga pasi, kuona nafasi na kufunga mabao, wakati Douka amekuwa akicheza zaidi upande wa kushoto, ambako kasi yake na ufundi wa kuchezea mpira umemfanya kuwa tishio kwa mabeki.
Douka anakiri ushindani baina yao ulianza tangu wakiwa wadogo, lakini anautazama kama sehemu ya kujitengeneza na kumsaidia kila mmoja kuwa bora zaidi.
“Tangu tukiwa wadogo tumekuwa tukishindana. Kaka yangu ni mzuri anapokuwa na mpira, anatengeneza nafasi nyingi kwa washambuliaji kama mimi, ananipatia pasi na anafunga mabao. Ana ubunifu na nguvu kubwa katika mchezo,” alisema Douka.
Uelewano wao ulionekana katika mchezo wa timu za vijana za Manchester United dhidi ya Liverpool na Bassirou alitoa pasi kwa Douka kwenye nafasi ya kufunga na kumalizia kwa ustadi. Hata hivyo, Douka anasema bado hajatoa asisti kwa kaka yake, lakini ana matumaini huenda hilo likatokea katika Kombe la Dunia Qatar 2026.
“Bado sijafanya hivyo, lakini natumaini itatokea hivi karibuni. Labda katika Kombe hili la Dunia,” alisema Douka, kauli iliyomfanya Bassirou kumjibu kwa utani kuwa naye anapaswa kupewa pasi ili afunge.
Pacha hao walianza safari yao ya soka katika akademi ya Manchester United mwaka 2022, jambo ambalo Douka analielezea kama kutimia kwa ndoto kubwa waliyokuwa nayo tangu utotoni.
“Manchester ilikuwa ndoto yetu. Tunazungumzia moja ya klabu kubwa zaidi duniani. Kila mtu anatamani kucheza katika klabu hii, hivyo ni heshima kubwa kwetu. Walipotutafuta mwanzoni tulishangaa, lakini tulifurahi sana,” alisema Douka. Bassirou anaongeza kuwa ndoto ya kucheza Man United ilikuwa ndani yake tangu akiwa mdogo na klabu hiyo ilifanya mazungumzo na wazazi wao kabla ya kuwapa nafasi ya kujiunga nayo.
Pacha hao pia wamepata nafasi ya kujifunza kutoka kwa nyota wenzao wa Cameroon wanaocheza kikosi cha kwanza, Bryan Mbeumo na Carlos Baleba, ambao wamekuwa wakiwapa ushauri na kuwatia moyo katika safari yao ya soka.
Douka anasema Mbeumo na Baleba wamekuwa watu wa karibu kwao, huku Bassirou akimuelezea Baleba kama kaka mkubwa anayemsaidia kutokana na kucheza nafasi inayofanana na yake.
“Baleba ni kama kaka mkubwa kwangu, anajaribu kutuangalia na kutusaidia. Wakati mwingine tunapokuwa na mazoezi na kikosi cha kwanza tunazungumza nao. Bryan pia ni mtu mzuri, anatusalimia na kutuambia tufanye kazi kwa bidii ili tuweze kujiunga na kikosi cha kwanza haraka iwezekanavyo,” alisema Bassirou.
Katika Kombe la Dunia U-17 Qatar 2026, mapacha hao walicheza mechi yao ya kwanza Jumamosi Novemba 21, ambapo Cameroon ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Venezuela.
Bassirou anasema kikosi hiko kipo Qatar kikiwa na malengo makubwa ya kufanya vizuri na kuipa heshima nchi yao, akisisitiza kuwa wachezaji wote wameungana kama familia bila kujali kama wanacheza nje au ndani ya Cameroon.
Kwa mapacha hao, kucheza Kombe la Dunia pamoja ni mwanzo wa safari wanayotamani kuiandika katika historia ya soka la nchi yao. Wamekuwa wakitazama mfano wa mapacha wa zamani wa Brazil, Rafael na Fabio, waliowahi kucheza pamoja Manchester United na kuiwakilisha nchi yao katika Kombe la Dunia U-17 mwaka 2007.