Usky ngumi anazijua na mkwanja pia anao
Muktasari:
- Mapambano hayo mawili yamemfanya Usyk kumaliza mwaka jana akiwa na mkwanja wa kutosha na kuzidi kuongeza utajiri wake. Hapa tumekuletea utajiri kamili wa staa huyu na jinsi mapambano hayo mawili yalivyomfanya kuwa na fedha nyingi zaidi.
RIYADH, SAUDI ARABIA: BAADA ya pambano la kwanza la Mei mwaka jana kati ya Alexander Usky na Tyson Fury, wawili hawa walirudiana Desemba mwaka huo huo na Fury alipoteza kwa mara ya pili kwenye pambano hilo la raundi 12.
Mapambano hayo mawili yamemfanya Usyk kumaliza mwaka jana akiwa na mkwanja wa kutosha na kuzidi kuongeza utajiri wake. Hapa tumekuletea utajiri kamili wa staa huyu na jinsi mapambano hayo mawili yalivyomfanya kuwa na fedha nyingi zaidi.
ANAPIGAJE PESA
Alitajwa kuwa na utajiri unaofikia dola 50 milioni baada ya kuingiza Dola 45 milioni katika pambano la kwanza dhidi ya Fury na unatarajiwa kuongezeka baada ya pambano la pili ambalo alivuna zaidi ya Dola 100 milioni.
Pambano lake jingine ambalo linatajwa kwamba lilimtajirisaha sana ni lile dhidi ya Anthony Joshua mwaka 2022 ambalo alipata Pauni 42 milioni kama malipo ya ushindi baada ya kumchapa bondia huyo raia wa Uingereza.
Pia aliwahi kupata Dola 6 milioni kama pesa za ushindi baada ya kumpiga Daniel Dubois kwa KO.
Mbali ya mapambano hayo Usyk pia anakunja mkwanja wa kutosha katika biashara zake mbalimbali kwanza ni mmiliki mwenza wa kampuni ya ‘Ready to Fight’.
Bondia huyu mwenye umri wa miaka 37, pia ni mmiliki wa kampuni ya Usyk-17 Promotions, ambayo inajihusisha na uandaaji wa mapambano mbalimbali ya ngumi pamoja na kusimamia mabondia.
NDINGA
BMW M8 Gran Coupe-Dola 138,800
Mercedes-AMG-Dola 190,000
Smart Fortwo -Dola 24,650
Audi RS Q8 -Dola 125,800
MSAADA KWA JAMII
Ana taasisi yake iitwayo Usyk Foundation ambayo imejikita zaidi kusaidia wananchi wa Ukraine waliothirika na vita inayoendelea nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, taasisi hiyo imetoa msaada wa zaidi ya Dola 1 milioni hadi sasa ikiwa pamoja na chakula.
MJENGO
Anamiliki mjengo wa kifahari huko Vorzel, Ukrane ambayo baada ya vita kuanza, jeshi la Urusi liliteka eneo hilo ikiwa pamoja na nyumba yake lakini mwaka 2022 jeshi la Ukraine likafanikiwa kulikomboa na kupitia mtandao wa Instagram , Usky alipiga picha mbalimbali mara yake ya kwanza kurudi katika nyumba hiyo. Haijajulikana hasa thamani ya nyumba hiyo lakini ripoti zinaeleza haizidi Dola 1 milioni.
MAISHA NA BATA
Yupo kwenye ndoa na Yekaterina, ambaye alimuoa mwaka 2009, hadi sasa wamebahatika kupata mtoto mmoja wa kiume aitwaye Mykhailo Usyk. Bondia huyu sio mtu wa kupenda kuweka mambo yake mengi wazi na muda mwingi huuwekeza zaidi kwenye kujifua na kujiweka sawa kwa ajili ya mapambano akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 23 na kushinda yote, huku KO zikiwa 14.