Noma sana! OPTA yaanika kumi bora EPL
Muktasari:
- Ligi Kuu England imesimama kupisha mechi za kimataifa, wakati huu Liverpool ikiongoza baada ya kuwa na rekodi bora kwa asilimia 100 katika mechi ilizocheza, ikishinda zote tatu.
LONDON, ENGLAND: MASTAA 10 bora kwenye Ligi Kuu England msimu huu wamewekwa bayana kwa mujibu wa takwimu za Opta huku kiungo wa Chelsea, Moises Caicedo akiongoza kwa kufanya vizuri baada ya mechi tatu zilizochezwa hadi sasa.
Ligi Kuu England imesimama kupisha mechi za kimataifa, wakati huu Liverpool ikiongoza baada ya kuwa na rekodi bora kwa asilimia 100 katika mechi ilizocheza, ikishinda zote tatu.
Liverpool imekuwa na huduma bora kabisa kwenye safu yake ya ushambuliaji ikiwa na huduma ya Hugo Ekitike, ambaye amefanya vizuri kwenye mechi zote tatu ilizoshinda kwenye ligi.
Imeruhusu mabao manne katika mechi mbili za kwanza, dhidi ya Bournemouth na Newcastle United na ilihitaji ushindi wa dakika za jioni dhidi ya Arsenal kuweka rekodi ya kushinda zote.
Kwenye orodha hiyo ya mastaa 10 bora, hakuna hata mmoja wa Arsenal aliyepata pointi nyingi za Opta kupata nafasi. Vigezo vilivyotumika ni kipimo cha mchezaji kuchangia timu yake kwenye mabao, kukaba na kuruhusu mabao. Na kwa mchezaji aliyecheza dakika 90 anaweza kukusanya pointi kati ya 10 na 40 na mchezaji anayeshika namba moja ana wastani wa pointi 31.7.
Kiwango cha Caicedo kwenye eneo la kiungo kimekuwa kitu kikubwa huko Chelsea kutokana na namba zake. Kiungo mwingine anayeshika namba mbili kwa kufanya vizuri katika mechi tatu zilizochezwa kwenye Ligi Kuu England hadi sasa ni staa wa Nottingham Forest, Elliot Anderson.
Beki wa kati Trevoh Chalobah amekuwa na mwanzo mzuri kwenye kikosi cha Chelsea, ambapo kwa sasa msimu huu amekuwa mtu muhimu tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambapo kocha Enzo Maresca alikuwa anapiga hesabu za kumpiga bei.
Kipa wa Tottenham Hotspur, Guglielmo Vicario ndiye mchezaji pekee kwenye eneo la kipa kuingia kwenye 10 bora ya mastaa waliofanya vizuri kwenye mechi tatu za ligi zilizochezwa hadi sasa msimu huu baada ya kucheza mechi mbili bila ya kuruhusu mpira kugusa nyavu zake.
Viungo wawili wachezeshaji Bruno Fernandes na Lucas Paqueta, ambao wote wameshafunga mabao msimu huu, wanashika namba tano na sita kutokana na kuonyesha viwango bora kwa kuwa na mchango mkubwa kwa timu zao, hasa kwenye eneo la juu la kushambulia.
Kiwango cha kuvutia cha staa mpya wa Chelsea, Joao Pedro naye ametajwa kwenye orodha hiyo ya Opta, akishika namba nane kwa wachezaji waliofanya vizuri kwenye ligi.
Staa huyo wa Kibrazili amefunga mara mbili katika mechi tatu alizochezea Chelsea kwenye Ligi Kuu England baada ya usajili wake kutokea Brighton. Mchezaji mwenzake wa Chelsea, Enzo Fernandez naye akiingia kwenye orodha hiyo, ambapo kikosi cha The Blues kikiingiza mastaa wanne kwenye wakali 10 waliofanya vizuri katika ligi hadi sasa msimu huu.
Chelsea bado haijapoteza mechi msimu huu huku pointi pekee ilizoangusha zilikuwa kwenye sare ya mechi yao ya kwanza ya msimu dhidi ya Crystal Palace.
Licha ya Manchester City kuanza kwa kasi hafifu msimu huu, straika wao Erling Haaland amepata nafasi kwenye orodha hiyo ya mastaa 10 bora waliocheza kwenye ligi hadi sasa. Amefunga mabao matatu, mawili akitikisa nyavu kwenye mchezo dhidi ya Wolves.
Mchezaji mwenzake wa zamani Jack Grealish, ambaye anafurahia maisha yake mapya huko Everton alikonaswa kwa mkopo, amekuwa kwenye kiwango bora kabisa na kuingia kwenye orodha hiyo ya mastaa 10 bora kwa mujibu wa Opta.
Kiungo huyo mchezeshaji, Grealish atakipiga Everton kwa mkopo wa msimu mmoja na chini ya kocha David Moyes katika mechi mbili alizomwanzisha ameasisti mara nne.
Hii hapa orodha ya mastaa waliofunika kwenye mechi tatu za kwanza kwenye Ligi Kuu England msimu huu kwa mujibu wa Opta.
1. Moises Caicedo
2. Elliot Anderson
3. Trevoh Chalobah
4. Guglielmo Vicario
5. Bruno Fernandes
6. Lucas Paqueta
7. Enzo Fernandez
8. Joao Pedro
9. Erling Haaland
10. Jack Grealish