Nico Williams aiingiza Bayern Munich vitani

Muktasari:
- Nico mwenye umri wa miaka 22, mbali ya kuhitajika na Bayern, huduma yake pia inamezewa mate na Arsenal na Barcelona.
BAYERN Munich imeanza tena kuonyesha nia ya kutaka kumsajili winga wa Athletic Bilbao na timu ya taifa ya Hispania, Nico Williams dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Nico mwenye umri wa miaka 22, mbali ya kuhitajika na Bayern, huduma yake pia inamezewa mate na Arsenal na Barcelona.
Ripoti zinaeleza, Nico anaweza akaondoka mwisho wa msimu huu ikiwa timu inayomhitaji italipa kiasi cha pesa kinachohitajika kwa mujibu wa mkataba wake ambacho ni kati ya Euro 60 milioni hadi Euro 80 milioni.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, Msimu huu amecheza mechi 36 za michuanbo yote, amefunga mabao tisa na kutoa asisti saba.
Alexander Isak
STRAIKA anayewindwa na vigogo wengi barani Ulaya, Alexander Isak, 25, wa Newcastle United ameweka wazi anatarajia kufanya mazungumzo ya mkataba mpya na timu hiyo baada ya msimu huu kumalizika. Isak ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 32 za michuano yote na kufunga mabao 22. Liverpool na Arsenal ni kati ya timu ambazo zinataka saini yake.
Dario Essug
CHELSEA imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa Sporting Lisbon raia wa Ureno, Dario Essugo katika dirisa lijalo la majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 21 milioni baada ya kuvutiwa na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu akiwa Las Palmas anayoichezea kwa mkopo. Mkataba wa Dario na Lisbon unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na kuna kila dalili akaondoka mwisho wa msimu kusaka changamoto mpya kwengine.
Jarrad Branthwaite
REAL Madrid inawatazama beki wa Tottenham na Argentina, Cristian Romero, 26, na beki wa Everton na England, Jarrad Branthwaite, 22, kama miongoni mwa wachezaji inaoweza kuwasajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mabeki hawa ambao mikataba yao haina muda mrefu sana kabla ya kuisha ni miongoni mwa mastaa tegemeo wa timu zao, lakini huenda wakaondoka mwisho wa msimu.
Leroy Sane
LIVERPOOL huenda ikakutana na upinzani wa kutosha kutoka kwa Arsenal juu ya mpango wao wa kutaka kumsajili winga wa Bayern Munich na Ujerumani, Leroy Sane, 29, ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Licha ya vigogo hawa kuonyesha nia ya kutaka kumsajili Sane, staa huyo anaweza pia akasaini mkataba mpya wa kuendelea kubakia Bayern.
Yasin Ayari
BRIGHTON inatarajia kupokea kiasi kisichopungua Pauni 20 milioni kutoka kwa timu zinazohitaji saini ya kiungo wao raia wa Sweden, Yasin Ayari katika dirisha lijalo. Timu nyingi zinahitaji huduma ya Ayari lakini Borussia Dortmund na AC Milan ndizo zinaonekana kuwekeza nguvu zaidi. Mkataba wake na Brighton unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Malick Fofana
ARSENAL na Liverpool ni miongoni mwa timu zinazohitaji saini ya winga wa Olympique Lyon na Ubelgiji, Malick Fofana, 19, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Malick amekuwa katika kiwango bora tangu mwanzo wa msimu huu kiasi cha kuvutia vigogo wengi waliojaribu kumsajili Januari lakini ikashindikana.
Jorrel Hato
LIVERPOOL imetuma maskauti wake kwenda Uholanzi kwa ajili ya kumtazama beki wa kushoto wa Ajax, Jorrel Hato, mwenye umri wa miaka 19, ambaye amecheza mara tano katika kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi. Hato ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, msimu huu amecheza mechi 40 za michuano yote.