Man City yaandaliwa ofa Madrid kwa Rodri
Muktasari:
- Hata hivyo, Manchester City inajiandaa kupokea ofa kutoka Real Madrid kwa ajili ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30, ingawa mabingwa hao wa zamani wa England bado wana matumaini ya kumuongezea mkataba mpya.
PARIS Saint-Germain (PSG) haina mpango wa kuwasilisha ofa ya kumsajili kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Hispania, Rodrigo Hernandez Cascante maarufu Rodri ambaye alishinda Kombe la Dunia 2026 hivi majuzi huko Marekani.
Hata hivyo, Manchester City inajiandaa kupokea ofa kutoka Real Madrid kwa ajili ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30, ingawa mabingwa hao wa zamani wa England bado wana matumaini ya kumuongezea mkataba mpya.
Kwa muda mrefu sasa ishu ya Rodri kutaka kuondoka Manchester City imeendelea kutingisha viunga vya Etihad tangu kabla ya fainali za kombe la Dunia na hasa kutokana na kauli aliyoitoa mapema tu baada ya msimu wa 2025/26 kumalizika alipodai kwamba hatima ya wapi atacheza msimu ujao itajulikana mara tu baada ya michuano hiyo.
Ingawa mwenyewe hajazungumza lolote hadi sasa, lakini ameendelea kuhusishwa na Real Madrid ikizingatiwa kiwango aliochokionyesha katika fainali za Kombe la Dunia zilizomalika ambako aling’ara akiibeba Hispania kutwaa ubingwa wake wa pili wa mashindani hayo tangu yalipoanza 1930.
James Trafford
LEEDS United inatarajiwa kukamilisha dili la kumsajili kipa wa Manchester City, James Trafford, kwa ada ya Pauni milioni 40. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye ni kipa wa timu ya taifa ya England, anatarajiwa kujiunga na Leeds katika hatua ya kuimarisha kikosi hicho akiachana na Man City ambako amekuwa akisugua benchi.
Joshua Zirkzee
MANCHESTER United inadaiwa kuingia kwenye mazungumzo ya hatua za juu ya kumpeleka kwa mkopo mshambuliaji wa kimataifa wa Uholanzi, Joshua Zirkzee, katika kikosi cha Juventus msimu mmoja. Inadaiwa kwamba iwapo itakamilika mkataba unatarajiwa kuwa na kipengele cha kumuuza moja kwa moja kwa thamani ya Pauni milioni 30.
Zion Suzuki
PARIS Saint-Germain imeonyesha nia ya kumsajili kipa wa Parma, Zion Suzuki, mwenye umri wa miaka 23. Kipa huyo wa kimataifa wa Japan pia amekuwa akihusishwa na Aston Villa na Juventus ambazo zinamfukuzia kwenda kufukia mashimo katika vikosi vyao. Suzuki alionyesha ubora wa juu katika michuano ya Kombe la Dunia 2026, ambako aliiongoza vyema Japan kutinga hatua ya 16 bora.
Raphael Le Guen
CRYSTAL Palace inadaiwa kufikia makubaliano binafsi na beki wa kati wa Brest, Raphael Le Guen, ambapo mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 19 anatarajiwa kujiunga na kikosi hicho baada ya mazungumzo kufikia hatua nzuri. Kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba pande mbili, yaani mchezaji na Palace wanakamilisha makubaliano ya kimkataba.
Ibrahim Mbaye
MSHAMBULIAJI wa PSG, Ibrahim Mbaye, amepewa nafasi ya kujiunga na Liverpool au Manchester City baada ya mawakala wake kueleza kuwa hatajiunga na Aston Villa msimu huu ambako anaamini kwamba siyo sehemu sahihi kwake kwani huenda akakumbana na ushindani mkali wa namba. Mbaye, 18, ni mshambuliaji wa kimataifa wa Senegal ambaye amekuwa akisugua sana benchi PSG
Yan Diomande
REAL Madrid imewasilisha ofa ya pili yenye thamani ya kati ya Pauni milioni 94 na 98 kwa ajili ya winga wa Ivory Coast, Yan Diomande. Hata hivyo, mazungumzo zaidi yanahitajika ili kufikia makubaliano na RB Leipzig kuhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, ambaye pia alikuwa akiwaniwa na Liverpool, ingawa karibu kila kitu ni kama kimekamilika kwa ajili ya nyota huyo kutua Madrid.
RubenVargas
SEVILLA imetangaza bei ya Ruben Vargas ambaye iko tayari kumuuza kwa Euro milioni 20, sawa na takribani Pauni milioni 17 kutokana na utitiri wa timu zinazomtaka huko Ulaya. Brighton, Newcastle United na Aston Villa ni miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England zinazovutiwa na winga huyo wa kimataifa wa Uswisi mwenye umri wa miaka 22.
Dayann Methalie
SUNDERLAND inadaiwa kufikia makubaliano binafsi na beki wa kushoto wa Toulouse na timu ya taifa ya Ufaransa chini ya miaka 21, Dayann Methalie, ambapo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 anatarajia kuhamia Ligi Kuu Engaland kwenda kukuza kipaji chake kilichoanzia kwenye akademi za Ufaransa.
SasaLukic
FULHAM imeingizwa majaribuni baada ya kiungo wake wa kimataifa wa Serbia, Sasa Lukic, mwenye umri wa miaka 29, kuwa mmoja wa wachezaji wanaofukuziwa kwa kasi na Ipswich Town katika dirisha hili la usajili. Mchezaji huyo ambaye amekuwa na panda shuka nyingi kikosini amekuwa akipambana kuondoka Fulham baada ya kuwapo kwa timu nyingi zilizoanza kumfuatilia.