Ndoto ya China kutamba kisoka duniani shakani
Muktasari:
- Miaka mitano iliyopita, chini ya Rais Xi Jinping, China iliahidi kuwa mbabe wa soka duniani ifikapo mwaka 2050.
Shanghai, China (AFP). Miaka mitano iliyopita, chini ya Rais Xi Jinping, China iliahidi kuwa mbabe wa soka duniani ifikapo mwaka 2050.
Lakini kuporomoka kifedha kwa mabingwa wapya wa soka, kumeibua maswali kuhusu ndoto hiyo.
Jumapili, klabu ya Jiangsu FC ilisema imefunga "uendeshaji" -- ikiwa ni miezi mitatu tu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu -- mafanikio yaliyoelezewa na vyombo vya habari kuwa "ya kushtua".
Baada ya kukimbilia kupata upendeleo kutoka kwa Rais Xi na chama tawala cha kikomunisti, wawekezaji wanaanza kurudi nyuma tena na mwaka jana timu 16 zilijitoa katika soka nchini China. Nyingine zaidi zinatarajiwa kufuata mkondo.
Ni tatizo tofauti sana na wakati Ligi Kuu ya China ilipovunja rekodi ya usajili barani Asia mara tano katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, ikiishia kwa kiungo wa zamani wa Chelsea, Oscar kujiunga na klabu ya Shanghai SIPG kwa Euro 60 milioni (sawa na Sh166.9 bilioni za Kitanzania) Januari mwaka 2017.
Mshambuliaji wa Argentina, Carlos Tevez alivutwa na Shanghai Shenhua katika kipindi cha usajili msimu huo kwa mshahara wa Euro 730,000 kwa wiki (sawa na Sh2 bilioni za Kitanzania), kiwango ambacho ni cha juu kuliko vyote duniani.
Lakini shirika la habari la serikali, Xinhua lilisema wiki hii kuwa kupanda kw amishahara na ada za uhamisho kunakotokana na ushindani wa klabu, kumetengeneza puto ambalo sasa linapasuka.
Ikirejea takwimu za Chama cha Soka cha China, Xinhua ilisema matumizi ya kawaida kwa msimu wa mwaka 2018 kwa klabu 16 za Ligi Kuu yalikuwa dola 170 milioni za Kimarekani (sawa na Sh394.2 bilioni za Kitanzania), kulinganisha na mapato ya wastani wa yuan 686 milioni(sawa na Sh220.7 bilioni za Kitanzania).
"Matumizi ya klabu za CSL (Ligi Kuu) ni takriban mara kumi zaidi kulinganisha na ya Ligi Kuu ya Korea Kusini na mara tatu zaidi ya Ligi Kuu ya Japan," alisema rais wa CFA, Chen Xuyuan kwa mwezi Desemba, wakati kiwango cha juu cha mishahara kilipotangazwa.
Mwandishi wa habari, Ma Dexing alisema katika miaka 30 ya kuandika habari za soka la China ameona zaidi ya klabu 200, akionyesha tatizo kubwa zaidi ya la sasa na janga la virusi vya corona, ambalo lilichelewesha kuanza kwa Ligi Kuu kwa miezi kadhaa mwaka jana na kulazimisha mechi zichezwe bila ya mashabiki.
Tianjin Tigers, klabu ambayo imekuwepo Ligi Kuu tangu ilipoanzishwa mwaka 2004, inategemewa kuvunjwa ndani ya siku chache zijazo na kampuni inayomiliki klabu ya Hebei FC iko taabani kw amadeni.
"Sababu kubwa ni kwamba msingi wa soka la kulipwa la China ni dhaifu sana," alisema Ma, ambaye ana wafuasi milioni 1.5 katika akaunti yake ya Weibo, ambayo ni sawa na Twitter.
Klabu zinaundwa na kuendeshwa na kampuni ambazo zina muunganiko kidogo na jamii za maeneo yao, alisema Ma.
"Kwa hiyo kudumu kwa sopka la kulipwa la China kunategemea hali ya kiuchumi wa taasisi za kibiashara au kampuni," aliandika.
"Wakati kampuni au taasisi za biashara zinapokuwa na matatizo, klabu zinakufa."
Hicho ndicho kilichotokea kwa Jiangsu FC, ambayo hadi hivi karibuni ilikuwa inaitwa Jiangsu Suning, jina la waliokuwa wakiifadhili.
Suning, ambayo ina kampuni za biashara tofauti na ambayo pia inaimiliki klabu ya Inter Milan inayoongoza Ligi Kuu ya Italia, iko katika matatizo ya kifedha na imeiondoa klabu hiyo.
Amri ya hivi karibuni ya CFA kwa klabu kuwaondoa wadhamini katika majina yao rasmi -- labda kwa lengo la kulazimisha utamaduni wa mpira wa miguu -- ni mrija mpya kwa baadhi ya wawekezaji, limesema gazeti la Beijing News.
Kutegemea 'kunyonya damu'
Akizungumza na AFP mwaka jana, katibu mkuu wa CFA, Liu Yi alisema Ligi Kuu yenye afya ni muhimu kwa soka nchini Chinaambayo mipango yake pia ni kuandaa fainali za Kombe la Dunia na hata kutwaa kombe.
Ili kukabiliana na matumizi makubwa ya klabu na kutokuwepo kwa soko la wachezaji wa China, CFA ilianzisha kodi ya asilimia 100 katika uhamisho mwaka 2017 kwa wachezaji kutoka nje, pamoja na mishahara na kiwango cha uwekezaji.
Gazeti la Shanghai Observer lilisema klabu ni lazima ziondokane na mfumo wa mmiliki mmoja ili kutoa nafasi kwa umiliki wa wengi "kama serikali, kampuni, jamii na hata watu binafsi".
"Klabu za Ligi Kuu haziwezi kutegemea kunyonya damu kutoka kampuni mama lakini kuvutia udhamini zaidi, mapato ya siku za mechi (na kuboresha) shughuli za usajili sokoni," lilisema gazeti hilo katika safu ya maoni.
Liu aliiambia AFP kwamba China inaendelea na nia yake ya mipango ya muda mrefu, ikieleza kuwa wachezaji nyota kutoka nje, wakiwemo Oscar, Paulinho na Marouane Fellaini watabakia Ligi Kuu.
Lakini hakuna uhakika wa mipango ya muda mfupi.
Ligi Kuu yenye fedha zaidi inatarajiwa kuanza kipidi cha masika lakini huku janga la virusi vya corona likiendelea, CFA bado haijatangaza tarehe ya kuanza. Kwa kuzingatia matatizo ya Jiangsu na Tianjin, pia haieleweki ni timu gani zitahusishwa.
Wakati huohuo, timu ya taifa ya wanaume imepanda kwa nafasi tano katika orodha ya ubora ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) tangu China ilipoweka bayana ndoto yake kisoka mwaka 2016. Hivi sasa inashika nafasi ya 75, ikiwa juu kidogo ya Syria, ambayo inasumbuliwa na vita.
China imefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mara moja tu, mwaka 2002, wakati walipoondoka bila ya kufunga hata bao moja au kushinda mechi zao za hatua ya makundi.