Msumbiji yashinda mechi ya kwanza ikiichapa Gabon
Muktasari:
- Jambo hilo linaifanya Msumbiji kuandika historia tofauti kabisa kutoka ile ya kushindwa kupata ushindi katika mashindano hayo ya Afcon katika mechi zake 16 ilizowahi kucheza katika mashindano hayo.
RABAT, MOROCCO: MSUMBIJI imepata ushindi wa kibabe wa mabao 3-2 dhidi ya Gabon uwanjani Agadir na hivyo kuandikisha ushindi wao wa kwanza kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na hivyo kujiweka pazuri kwenye vita ya kuwania nafasi ya kutinga mtoano.
Jambo hilo linaifanya Msumbiji kuandika historia tofauti kabisa kutoka ile ya kushindwa kupata ushindi katika mashindano hayo ya Afcon katika mechi zake 16 ilizowahi kucheza katika mashindano hayo.
Kikosi hicho cha kocha Chiquinho Conde sasa kimepata matumaini ya kutinga mtoano, lakini ni pigo kubwa kwa Gabon, ambayo imepoteza mechi yake ya pili kwenye Kundi F baada ya kuchapwa pia na Cameroon kwenye mechi ya kwanza.
Bao la kichwa la Faisal Bangal lililotokana na mpira wa kona na mkwaju wa penalti wa Geny Catamo uliifanya Msumbiji kuwa kwenye utawala wa mchezo huo hadi hapo nahodha wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang alipofunga la kusawazisha kwenye dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza kuirudisha Panthers mchezoni.
Beki wa kulia, Diogo Calila alifunga kwa kichwa mapema kwenye kipindi cha pili kuifanya Msumbiji kuongoza tena kwa tofauti ya mabao mawili, kabla ya Aubameyang kuifungia Gabon bao la pili baada ya piga nikupige iliyotolea langoni mwa Msumbiji.
Jambo hilo lilifanya dakika 20 za mwisho kwenye mechi hiyo kuwa na mvuto mkubwa, kila timu ikijaribu kusaka bao, Gabon ikitaka la kusawazisha na Msumbiji ikitaka la kujihakikishia ushindi, lakini hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi Mehrez Melki wa Tunisia, ni mabao matano tu ndiyo yaliyotinga nyavuni katika mechi hiyo, Mambas ikiibuka na ushindi muhimu.
Matokeo hayo yanaifanya Msumbiji inayoshika namba 102 kwenye viwango vya ubora duniani kushika nafasi ya tatu kwenye Kundi F, ikiwa na pointi sawa na Ivory Coast na Cameroon kabla ya mechi yao ya Jumapili usiku huko Marrakesh.
Gabon sasa itahitaji kuichapa Ivory Coast katika mchezo wao wa mwisho huko Marrakesh ili kufufua matumaini ya kusonga mbele, wakati Msumbiji itakuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na Cameroon huko Agadir siku hiyo hiyo, Jumatano.