Mkataba mpya kumpa ukwasi Haaland
Muktasari:
- Amekuwa ni silaha muhimu iliyoiwezesha Manchester City kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England katika misimu miwili mfululizo iliyoichezea ambayo pia alimaliza akiwa kinara wa kufumania nyavu.
Manchester, England. Manchester City inajiandaa kumpa mkataba mpya mshambuliaji wake Erling Haaland utakaomfanya awe mchezaji anayelipwa kiasi kikubwa zaidi cha fedha katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Mkataba huo mpya ambao Man City inamuandalia nyota huyo wa Norway, utamfanya Haaland apokee mshahara wa kitita cha Pauni 850,000 kwa wiki ambacho kitakuwa ni mara mbili ya kile anachopata Kevin De Bruyne ambaye ndiye kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji anayelipwa kiasi kikubwa zaidi cha fedha kwenye EPL.
De Bruyne analipwa kiasi cha Pauni 425,000 kwa wiki hivi sasa akiwa na mkataba utakaomuweka katika klabu ya Manchester City hadi Juni 30 mwakani.
Katika mkataba huo mpya ambao Man City inataka kumpa Haaland, timu hiyo imepanga kuweka kipengele cha kumuuza mshambuliaji huyo kwa dau kubwa la fedha ili kuzikatisha tamaa timu ambazo zinamtolea udenda staa huyo wa Norway mwenye umri wa miaka 24.
Miongoni mwa timu ambazo Manchester City inazihofia kuwa zinaweza kumshawishi Haaland aondoken ili zimnyakue ni Real Madrid ambayo ilionyesha nia ya kumtaka Haaland tangu alipokuwa Ujerumani akiitumikia Borussia Dortmund.
Hata hivyo, kitendo cha Real Madrid kumsajili Kylian Mbappe kinaonekana kinapunguza uwezekano wa kuendelea na tamaa ya kumpata Haaland ingawa Manchester City inaonekana haitaki kuamini moja kwa moja kuwa miamba hiyo ya Hispania haina mpango wa kumnasa nyota huyo wa zamani wa Molde FK na RB Salzburg.
Haaland amekuwa mwiba kwa nyavu za timu pinzani tangu alipojiunga na Manchester City mwaka 2022 akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya uhamisho kiasi cha Pauni 51.2 milioni.
Tangu wakati huo hadi sasa, ameichezea timu hiyo idadi ya mechi 102 za mashindano tofauti na kuifungia mabao 97.
Amekuwa ni silaha muhimu iliyoiwezesha Manchester City kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England katika misimu miwili mfululizo iliyoichezea ambayo pia alimaliza akiwa kinara wa kufumania nyavu.
Ni mchezaji ambaye ameonyesha muendelezo mzuri wa kufumania nyavu katika kipindi chote alichoichezea Man City tangu alipojiunga nayo ambapo kwa misimu miwili iliyopita aliweka kimiani mpira zaidi ya mara 30 kwa kila msimu.
Na hilo anaonekana ataendelea nalo msimu huu kutokana na kasi ya kufumania nyavu aliyoanza kuionyesha katika mechi tatu za Ligi Kuu England ambazo Manchester City imeshacheza dhidi ya Chelsea, Ipswich na West Ham United mtawalia.
Katika mechi hizo, Haaland ameshafumania nyavu mara saba ambapo alifunga mabao matatu (hat trick) katika mchezo dhidi ya West Ham na Ipswich