Messi ashindwa kutamba kwa Al Ahly Kombe la Dunia la Klabu

Muktasari:
- Mechi ya pili ya kundi hilo itachezwa leo usiku wa kuamkia Jumatatu saa 7:00 kati ya Palmeiras ya Brazil na Porto ya Ureno.
FLORIDA, MAREKANI: Inter Miami ya Lionel Messi wa imelazimishwa suluhu na Al Ahly ya Misri katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu.
Messi aliongoza mashambulizi makali kipindi cha pili katika mchezo huo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia la Klabu, hata hivyo mbinu na uzoefu wake haukufua dafu kwa Al Ahly.

Mshambuliaji huyo wa Argentina, kama ilivyokuwa kwa wenzake, alikuwa kimya katika kipindi cha kwanza katika mchezo uliopigwa usiku wa kuamkia leo Jumapili kwenye Uwanja wa Hard Rock jijini Miami.
Mabingwa wa Misri, Al Ahly, walitawala mchezo na nafasi nyingi dakika 45 za mwanzo, hata hivyo, mashambulizi yao yalishindwa kupenya kwa kipa wa Inter Miami, Oscar Ustari.
Ilionekana kama juhudi za mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 39 zingekuwa bure wakati Mahmoud Trezeguet aliposimama kupiga penalti dakika ya 43, lakini Ustari alikata matumaini ya Al Ahly kubeba pointi tatu kutoka kwa Inter Miami baada ya kukosa penalti.

Kipindi cha pili kilikuwa na mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Marekani (Major League Soccer) na kilihitimishwa kwa Messi kupiga shuti la mbali lililogonga mtambaa wa panya.
Kipa wa Al Ahly, Mohamed El Shenawy, alifanikiwa kugusa kwa vidole shuti hilo la Messi lililopigwa kwa mguu wa kushoto mwishoni mwa mchezo.

El Shenawy pia kwa umakini wa hali ya juu alifanikiwa kuzima shambulio la kona dakika za majeruhi baada ya kuzuia kichwacha Maximiliano Falcon.
Unaweza kusema Inter Miami ilinusuriwa na kipa, Ustari, aliyekuwa imara golini kwa Inter Miami kipindi cha kwanza, hali iliyomfanya kocha wa Inter, Javier Mascherano, kusema kuwa timu yake imebebwa kwa kiasi kikubwa na kipa huyo.
Al Ahly walinyimwa bao baada ya Zizo kuchezewa rafu mbaya kutoka nyuma na Telasco Segovia jambo lililoipatia Al Ahly penalti, hata hivyo, mchezaji wa zamani wa Ligi Kuu ya England, aliyewahi kuichezea Aston Villa, Trezeguet, alipiga penalti iliyookolewa na Ustari.
“Ninafurahia kiwango tulichokionesha. Kipindi cha pili kilikuwa bora zaidi,” amesema Mascherano baada ya filimbi ya mwisho.
“Kipindi cha kwanza tulipoteza mipira na nafasi za mpito, ambazo wao walikuwa hatari sana.Tulitawala kipindi cha pili na tulikuwa na nafasi za kushinda mechi,” amesema.
Kwa upande wake kocha wa Al Ahly, Jose Riviera akizungumza na DAZN baada ya mchezo huo amesema: “Sio kwamba kuna kitu kilikwenda vibaya. Tulikuwa na nafasi nyingi kipindi cha kwanza kupeleka mechi katika mwelekeo tofauti. Hatukuweza,”
“Kipindi cha pili tulikuwa na wakati mgumu, lakini bado kuna mambo mengi chanya na maeneo ya kurekebisha kwa mara nyingine. Ilikuwa kama tunacheza Cairo. Kwa kweli ilinistaajabisha kwenye mechi yangu ya kwanza. Natumaini wakati ujao tutawapa mashambiki wetu ushindi,”
Mechi ya pili ya kundi hilo itachezwa leo usiku wa kuamkia Jumatatu saa 7:00 kati ya Palmeiras ya Brazil na Porto ya Ureno.
Inter Miami watacheza na Porto, huku Al Ahly wakivaana na Palmeiras kwenye mechi inayofuata siku ya Alhamisi Juni 19, mwaka huu.
Michezo mingine itakayopigwa leo ni PSG itavaana na Atletico Madrid saa 4:00 usiku, mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich wataivaa Auckland City ya New Zealand saa 1:00 usiku.