McTominay kufanyiwa upasuaji wa moyo
Kiungo wa Napoli na timu ya taifa ya Scotland, Scott McTominay. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Katika mechi 82 ambazo McTominay ameichezea Napoli, amefunga mabao 27 na kutoa pasi 10 za mwisho.
Naples, Italia. Kiungo wa Napoli na timu ya taifa ya Scotland, Scott McTominay, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo, baada ya kubainika kuwa na tatizo dogo la mpangilio wa mapigo ya moyo.
Napoli imethibitisha kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, atafanyiwa utaratibu maalumu wa kurekebisha tatizo hilo, unaojulikana kama cardiac arrhythmia ablation (PFA), katika siku chache zijazo.
“Kufuatia kuanza kwa arrhythmia (mpangilio usio wa kawaida wa mapigo ya moyo) isiyo kali na isiyo hatarishi, Scott McTominay atafanyiwa upasuaji wa kurekebisha tatizo hilo kwa kutumia ablation ya cardiac arrhythmia (PFA) katika siku zijazo,” imesema taarifa ya Napoli.
Klabu hiyo imeongeza kuwa, McTominay anatarajiwa kurejea uwanjani baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Kiungo wa Napoli na timu ya taifa ya Scotland, Scott McTominay. Picha na Mtandao
Utaratibu wa PFA hutumia nishati ya joto au baridi kutengeneza makovu madogo kwenye moyo, hatua inayosaidia kuzuia ishara za umeme zinazoweza kusababisha mapigo yasiyo ya kawaida na kurejesha mpangilio wa kawaida wa moyo.
Kutokana na matibabu hayo, McTominay anatarajiwa kukosa mechi za timu ya taifa ya Scotland zitakazochezwa katika kipindi hiki cha mapumziko ya kimataifa.
Hii ina maana kwamba, kiungo huyo hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachokuwa chini ya kocha mpya wa Scotland, Sebastien Pocognoli, katika mechi zake nne za mwanzo.
McTominay alicheza mechi yake ya mwisho kwa Napoli katika mchezo wa Serie A dhidi ya Como Jumapili iliyopita, ambapo Napoli ilipoteza kwa mabao 2-1. Katika mchezo huo, alitolewa dakika ya 56.
Kabla ya hapo, alicheza kwa dakika zote 90 katika ushindi wa Napoli wa mabao 2-0 dhidi ya Genoa kwenye mchezo wa kwanza wa msimu.
McTominay amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi Napoli, tangu alipohamia klabu hiyo, akitokea Manchester United mwaka 2024.
Katika mechi 82, alizoichezea Napoli, amefunga mabao 27 na kutoa pasi 10 za mwisho.
Kiungo wa Napoli na timu ya taifa ya Scotland, Scott McTominay. Picha na Mtandao
Msimu wa 2024-25 ulikuwa mzuri zaidi kwake, baada ya kuisaidia Napoli kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Italia ‘Serie A’, ilipokuwa chini ya meneja Antonio Conte.
McTominay alibadilika kutoka kuwa kiungo wa kawaida aliyekuwa akitumika Old Trafford na kuwa mmoja wa viungo hatari zaidi wanaofika mara kwa mara eneo la hatari la wapinzani.
Alifunga mabao 12, katika Serie A msimu huo na baadaye akachaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa ligi hiyo.
Mafanikio yake yalimwezesha pia kumaliza nafasi ya 18 katika kinyang'anyiro cha tuzo za Ballon d'Or, mwaka 2025, akiwapita nyota kadhaa wakubwa akiwamo Jude Bellingham, Erling Haaland na Michael Olise.