Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashabiki wamgeukia Fofana, Chelsea ikikubali kipigo cha Forest

Muktasari:

  • Fofana, mwenye umri wa miaka 25, amejikuta katika wakati mgumu Stamford Bridge baada ya kuhusishwa na matukio kadhaa yaliyowakasirisha mashabiki, ikiwamo mahojiano yasiyoidhinishwa aliyofanya hivi karibuni kupitia mtandao wa YouTube, ambako alionekana kuchukulia kwa mzaha penalti aliyokosa dhidi ya Liverpoo

BEKI wa Chelsea, Wesley Fofana, amekumbana na wakati mgumu baada ya kuzomewa na mashabiki wa timu yake mwenyewe kufuatia kiwango kibovu katika mchezo ambao The Blues walilala kwa mabao 3-2 dhidi ya Nottingham Forest kwenye Uwanja wa City Ground.

Fofana, mwenye umri wa miaka 25, amejikuta katika wakati mgumu Stamford Bridge baada ya kuhusishwa na matukio kadhaa yaliyowakasirisha mashabiki, ikiwamo mahojiano yasiyoidhinishwa aliyofanya hivi karibuni kupitia mtandao wa YouTube, ambako alionekana kuchukulia kwa mzaha penalti aliyokosa dhidi ya Liverpool.

Ingawa beki huyo raia wa Ufaransa aliomba radhi kutokana na kauli zake, mashabiki wa Chelsea hawakuonekana kuwa tayari kumsamehe.

Katika mchezo dhidi ya Nottingham Forest, mashabiki wa Chelsea waliokuwa ugenini walimzomea kila alipogusa mpira, huku baadhi yao wakisikika wakiimba nyimbo za kumshambulia kwa maneno makali.

Hali hiyo ilizidi kuwa mbaya kwa Fofana baada ya Nottingham Forest kupata bao la mapema dakika ya tano kupitia Igor Jesus, aliyefunga kwa shuti la mpira wa juu na kuipa timu yake uongozi.

Kipindi cha pili kilimzidishia matatizo beki huyo baada ya kushindwa kuudhibiti mpira mrefu uliompita na kumfikia Liam Delap, aliyekuwa mchezaji mwenzake Chelsea.

Katika harakati za kuokoa hatari hiyo, Fofana alimchezea Delap faulo ndani ya eneo la hatari na mwamuzi akaamuru penalti.

Morgan Gibbs-White hakufanya makosa, akafunga na kuongeza uongozi wa Forest, kabla ya kocha Xabi Alonso kumtoa Fofana uwanjani muda mfupi baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Levi Colwill.

Wakati akielekea nje, mashabiki wa Chelsea waliendelea kumzomea kwa nyimbo za kumdhalilisha, hali iliyodhihirisha hasira iliyokuwa imewakumba wafuasi hao.

Akizungumza baada ya mchezo, Alonso alisema timu inapaswa kusimama pamoja na kumsaidia kila mchezaji, akiwamo Fofana, badala ya kumtenga wakati mambo yanapokuwa magumu.

"Tunahitaji kumuunga mkono kila mmoja kwa sababu tunamhitaji kila mmoja. Tunahitaji mashabiki, tunahitaji wachezaji wote na tunapaswa kushikamana, vinginevyo mambo yatakuwa magumu zaidi.

"Ni lazima tushikamane. Kila mtu aliyepo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na ndani ya timu anahitajika. Tunapaswa kusaidiana na kupitia kipindi hiki pamoja. Hatutamwacha mtu yeyote nyuma," alisema Alonso.

Alipoulizwa kama itakuwa vigumu kumrejesha Fofana kwenye kikosi cha kwanza kutokana na mapokezi aliyoyapata kutoka kwa mashabiki, Alonso alisema bado atafikiria kuhusu hilo katika michezo ijayo.

Kocha huyo pia alithibitisha kuwa hakuzungumza na Fofana ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo mara baada ya mchezo.


CHELSEA HOI

Matokeo hayo yameifanya Chelsea kupoteza michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu England, baada ya awali kufungwa na Sunderland na Leeds United.

Alonso alisema licha ya matokeo mabaya, timu yake inaendelea kufanya kazi kutafuta suluhisho, akisisitiza kuwa hakuna mtu kutoka nje atakayewatatulia matatizo yao.

"Tunaendelea kufanya kazi na kujaribu kutafuta suluhisho, lakini mambo hayaendi kama tunavyotaka. Sioni njia nyingine ya kucheza soka zaidi ya kufanya kazi na kujaribu tena.

"Hakuna mtu kutoka nje atakayekuja kutupatia suluhisho. Kazi, ubora na mtazamo tunaouhitaji lazima vitoke ndani ya timu yenyewe," alisema.


EME​GHA AIBUKA

Katika mchezo huo, Nottingham Forest ilionekana kuwa na udhibiti baada ya kufikisha mabao mawili, lakini mchezaji wa akiba Emmanuel Emegha aliifungia Chelsea mabao mawili na kuipa timu hiyo matumaini ya kurejea mchezoni.

Hata hivyo, Gibbs-White alifunga bao jingine na kurejesha tofauti ya mabao mawili kwa wenyeji.

Emegha alifunga tena kwa kichwa na kuifanya Chelsea kuwa na nafasi ya kusawazisha katika dakika za mwisho, lakini jitihada hizo hazikutosha, huku Nottingham Forest ikiondoka na ushindi wa mabao 3-2.

Mchambuzi wa soka, Jamie Redknapp, alisema anamhurumia Fofana na kuhoji uamuzi wa Alonso kumchezesha beki huyo katika mchezo huo, akiamini huenda kocha huyo alipaswa kuzingatia changamoto alizokuwa akipitia mchezaji huyo ndani na nje ya uwanja.

Kwa Chelsea, kipigo hicho kimeongeza presha kwa Alonso na kikosi chake, huku Fofana akibaki kuwa miongoni mwa wachezaji wanaokabiliwa na hasira za mashabiki wa klabu hiyo.