Mashabiki wa Spurs waomba goli, watoka patupu
Muktasari:
- Bango hilo lililoinuliwa na shabiki kabla ya mchezo lilionekana kama ombi la msaada zaidi kuliko wito wa kawaida wa kufunga, huku Tottenham wakiingia kwenye mchezo huo wakitafuta bao lao la kwanza kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
LONDON, ENGLAND: MASHABIKI wa Tottenham Hotspur walifika uwanjani wakiwa na ujumbe mmoja kwa wachezaji wao kabla ya mchezo dhidi ya Everton: “Tafadhali tufungieni goli.” Hata hivyo, kilio hicho hakikusikika uwanjani baada ya Spurs kushindwa kufunga kwa mara nyingine.
Bango hilo lililoinuliwa na shabiki kabla ya mchezo lilionekana kama ombi la msaada zaidi kuliko wito wa kawaida wa kufunga, huku Tottenham wakiingia kwenye mchezo huo wakitafuta bao lao la kwanza kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila bao, ujumbe huo ungeweza kubadilishwa kuwa “Tafadhali pigeni hata shuti”, kwani licha ya kumiliki mpira kwa muda mrefu, kikosi hicho kilichokusanywa kwa gharama Pauni 300 milioni chini ya kocha Roberto De Zerbi kilishindwa kuisumbua vilivyo ngome ya Everton na kipa wake Jordan Pickford.
Hali hiyo iliendelea hadi mwisho huku mashabiki wa Spurs wakizidi kukasirika na kukata tamaa, huku timu hiyo ikifikisha dakika 407 bila kufunga bao kwenye Ligi Kuu.
Ilikuwa mara ya kwanza katika historia yao kushindwa kufunga katika michezo yao minne ya mwanzo ya ligi katika madaraja yote manne ya soka la England. Pia ilikuwa mara ya kwanza tangu Septemba 2006 kwa Tottenham kushindwa kufunga katika michezo minne mfululizo ya Ligi Kuu.
Takwimu hizo ni za kusikitisha zaidi kutokana na ukweli kwamba Spurs walitumia zaidi ya Pauni300 milioni katika usajili msimu huu, sehemu kubwa ikiwa na lengo la kuongeza makali ya kikosi cha De Zerbi.
Badala yake, Tottenham wameonekana kuwa timu isiyo na makali mbele ya lango.
Suluhu hiyo ilikuwa ya kwanza katika historia ya Uwanja wa Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu, tangu ulipoanza kutumika na kufikisha mchezo wake wa 140 wa ligi.
De Zerbi mwenyewe alilazimika kuomba radhi kwa mashabiki baada ya mchezo huo, akikiri kuwa walistahili zaidi kutokana na namna walivyoiunga mkono timu.
“Naomba radhi kwa mashabiki. Tunasikitika kwa mashabiki. Walikuwa wazuri sana, hasa kipindi cha kwanza. Walipoona timu ikicheza vizuri na kusukuma kutafuta suluhisho, walikuwa pamoja na wachezaji wangu,” amesema De Zerbi.
Everton walikuwa na nafasi ya kuifanya hali iwe mbaya zaidi kwa wenyeji, lakini nao walionekana kukosa makali katika eneo la ushambuliaji, jambo lililowasaidia Spurs kuondoka na angalau pointi moja.
Katika kipindi cha pili, Everton walipata nafasi mbili bora zaidi za mchezo kupitia Kiernan Dewsbury-Hall na Brennan Johnson, huku presha ikiendelea kuongezeka kwa Tottenham na mashabiki wao.
Tottenham walipopata shuti lao la kwanza lililolenga lango dakika ya 46 kupitia mchezaji wao mpya aliyesajiliwa kwa Pauni85 milioni, Mateus Fernandes, mashabiki walilipokea kwa makofi ya kejeli.
Kadiri dakika zilivyoyoyoma, De Zerbi alijaribu kubadilisha hali kwa kuwatumia wachezaji wapya, akiwemo Omar Marmoush na Savio kutoka Manchester City, huku Dominic Solanke akipewa nafasi yake ya kwanza kuanza mchezo wa ligi msimu huu.
Baadaye Mohammed Kudus na James Maddison waliingia, lakini ilikuwa ni mchezaji mwingine wa akiba, Lucas Bergvall, aliyekaribia kuipa Spurs ushindi baada ya kupiga shuti la mbali lililookolewa na Pickford.
Pickford mwenyewe ndiye aliyempa Bergvall nafasi hiyo baada ya kumpa mpira, lakini kipa huyo alijirekebisha na kuokoa shuti la Msweden huyo.
Wakati hayo yakitokea, mshambuliaji wa Brazil, Richarlison, mwenye miaka 29, alitazama mchezo huo akiwa jukwaani huku akiwa kwenye mvutano na klabu kuhusu miezi tisa iliyosalia kwenye mkataba wake.
Richarlison aliondolewa kwenye kikosi cha De Zerbi cha Ligi Kuu baada ya mpango wa kurejea katika klabu yake ya zamani, Everton, kushindikana siku ya mwisho ya usajili. Pia mpango wa kurejea Brazil kujiunga na Vasco da Gama haukufanikiwa.
Filimbi ya mwisho ilipulizwa huku Tottenham wakiondoka uwanjani bila bao, na safari yao ya kutafuta bao la kwanza la ligi msimu huu ikiendelea, huku mashabiki wakiwazomea wachezaji wao.