Man City yavunja rekodi kwa Bouaddi
Muktasari:
- Bouaddi, 18, amesaini mkataba wa miaka mitano, huku usajili huo ukisubiri kukamilishwa kwa taratibu za kimataifa. City imelipa Pauni81.4 milioni kama malipo ya awali na Pauni4.2 milioni nyingine zikiwa katika mfumo wa nyongeza.
MANCHESTER, England: MANCHESTER City imemsajili kiungo wa Lille, Ayyoub Bouaddi, kwa ada ya jumla ya Pauni85.6 milioni, na kumfanya kuwa mchezaji chipukizi ghali zaidi kuwahi kusajiliwa katika historia ya Ligi Kuu England.
Bouaddi, 18, amesaini mkataba wa miaka mitano, huku usajili huo ukisubiri kukamilishwa kwa taratibu za kimataifa. City imelipa Pauni81.4 milioni kama malipo ya awali na Pauni4.2 milioni nyingine zikiwa katika mfumo wa nyongeza.
Kocha wa City, Enzo Maresca ameamua kuongeza nguvu kwenye kiungo baada ya klabu hiyo kuwauza Rodri kwenda Barcelona kwa Pauni65 milioni na Tijjani Reijnders kujiunga na Al-Qadsiah kwa Pauni 52milioni.
Bouaddi alionyesha kiwango kizuri katika Kombe la Dunia la mwaka huu, akianza michezo mitano kati ya sita ya Morocco katika safari yao iliyowafikisha robo fainali.
Kabla ya hapo, alikuwa tayari amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Lille kwenye Ligue 1.
“Hii ni siku maalumu kwangu na familia yangu. Kwangu, Manchester City ni klabu bora zaidi duniani. Ni ndoto kuwa hapa na kuweza kujiita mchezaji wa City,” alisema Bouaddi.
“Nimetumia sehemu kubwa ya maisha yangu kufanya kazi kwa bidii ili kuwa mchezaji bora ninayeweza kuwa na kufikia kilele cha mchezo huu.
“Nimekuwa nikiiangalia City kwa miaka mingi na napenda mtindo wao wa uchezaji. City daima inajaribu kucheza soka lenye ubora. Wameonyesha pia kuwa washindi; klabu hii inaonekana imejengwa kwa ajili ya kushinda.”
Ada ya Bouaddi imevuka Pauni 58.9milioni ambazo Manchester United ililipa kumsajili beki wa Ufaransa, Leny Yoro, pia kutoka Lille mwaka 2024.
Bouaddi alicheza jumla ya mechi 96 akiwa Lille tangu alipocheza mchezo wake wa kwanza mwaka 2023, na msimu uliopita aliisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu katika Ligue 1.
Akiwa na miaka 16, alifanya historia kwa kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza mechi ya kikosi cha kwanza cha Lille alipocheza dhidi ya KI ya Visiwa vya Faroe katika Europa League.
Baadaye alijitambulisha zaidi kwenye jukwaa la Ulaya alipokuwa miongoni mwa nyota wa Lille katika ushindi wao dhidi ya Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa mwaka 2024.
Bouaddi atakuwa sehemu ya mabadiliko makubwa katika safu ya kiungo ya City, ambayo tayari imemsajili kiungo wa England, Elliot Anderson, kutoka Nottingham Forest kwa Pauni milioni 116.
Bouaddi anacheza zaidi kama kiungo wa chini anayesimamia ujenzi wa mashambulizi, na anatarajiwa kuendana vizuri na Anderson, ambaye anaweza kucheza kama kiungo wa box-to-box pamoja na nafasi ya namba sita anayocheza akiwa na timu ya taifa ya England.
City pia inatarajiwa kuwasilisha ofa kwa kiungo wa Argentina wa Chelsea, Enzo Fernandez, ingawa bado haijafahamika kama makubaliano yanaweza kufikiwa kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye thamani yake inakadiriwa kufikia Pauni milioni 120.
Usajili wa Bouaddi unakuja siku chache baada ya winga wa Brazil, Savinho, ambaye sasa anatumia jina la Savio, kujiunga na Tottenham kwa Pauni75 milioni.
Tottenham pia imekubaliana kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Misri wa City, Omar Marmoush, huku kiungo wa Hispania, Nico Gonzalez, akitarajiwa kuondoka City na kujiunga na Newcastle kwa ada ya Pauni milioni 52.