Maldini apata ajali baada ya kufunga
Muktasari:
- Maldini, mwenye umri wa miaka 24, alihusika katika ajali hiyo akiwa akiendesha gari yaeke aina ya Porsche Carrera katika maeneo ya pembezoni mwa jiji la Milan, majira ya alfajiri ya Jumapili.
MILAN, Italia: MTOTO wa gwiji wa soka la Italia, Paolo Maldini, Daniel Maldini amekimbizwa hospitalini kwa uchunguzi baada ya kupata ajali ya gari, saa chache tu baada ya kufunga bao la ushindi lililoipa Cagliari pointi tatu muhimu kwenye Serie A.
Maldini, mwenye umri wa miaka 24, alihusika katika ajali hiyo akiwa akiendesha gari yaeke aina ya Porsche Carrera katika maeneo ya pembezoni mwa jiji la Milan, majira ya alfajiri ya Jumapili.
Ajali hiyo ilitokea saa chache baada ya kiungo huyo kufunga penalti ya ushindi dhidi ya klabu yake ya zamani, Atalanta, Jumamosi usiku, katika mchezo ambao Cagliari ilishinda kwa ushindi muhimu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Italia, ANSA, Maldini alidaiwa kufeli kipimo cha pumzi cha ulevi na leseni yake kuchukuliwa baada ya ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 11:15 alfajiri.
Hata hivyo, taarifa hizo bado hazijathibitishwa rasmi na polisi wa Italia.
Watu sita walihusika katika ajali hiyo iliyohusisha magari mawili, huku wote wakiripotiwa kupata majeraha madogo.
Magari matatu ya wagonjwa pamoja na gari la huduma za dharura yalipelekwa eneo la tukio. Mtu mmoja alitibiwa hapo hapo, huku wengine watano, akiwamo Maldini, wakipelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi.
Maldini alipelekwa katika Hospitali ya Fatebenefratelli mjini Milan kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.
Hakuna taarifa zinazoonyesha kuwa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Italia alipata majeraha makubwa kutokana na ajali hiyo.
Tukio hilo lilitokea baada ya Maldini kuwa na usiku wa kukumbukwa uwanjani, akifunga penalti ya ushindi dhidi ya Atalanta na kuendeleza mwanzo wake mzuri wa msimu.
Bao hilo lilikuwa la pili kwa Maldini katika mechi zake nne za Serie A msimu huu.
Maldini ni kizazi cha tatu cha familia maarufu katika soka la Italia, akifuata nyayo za baba yake Paolo na babu yake Cesare Maldini.
Paolo ni mmoja wa mabeki wakubwa zaidi kuwahi kutokea, akitamba kwa muda mrefu katika klabu ya AC Milan na timu ya taifa ya Italia.
Babu yake, Cesare, pia aliichezea Milan na Italia kabla ya kuingia katika ukocha. Tofauti na baba na babu yake waliocheza zaidi nafasi za ulinzi, Daniel anacheza mbele zaidi kama kiungo mshambuliaji.
Alilelewa katika akademi ya Milan na kucheza mechi 24 za kikosi cha kwanza cha miamba hiyo kabla ya kutimkia Spezia, Empoli na Monza kwa nyakati tofauti.
Baadaye alijiunga na Atalanta na msimu uliopita akacheza kwa mkopo katika Lazio kabla ya kuhamia Cagliari kwa mkopo mwingine.
Maldini, ambaye amecheza mechi sita kwa Italia, ameanza vizuri maisha yake Cagliari, huku klabu hiyo ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Serie A.