Mabeki waiokoa Ufaransa Kombe la Dunia U-20
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyopigwa juzi, Ufaransa ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 2-1, lakini mabeki wake wawili, Aude Bizet na Landryna Lushimba, walibadilisha matokeo kipindi cha pili.
UFARANSA imeonyesha kasi ya upambanaji baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ecuador katika mechi ya Kundi C ya Kombe la Dunia la Wanawake la U-20, Poland 2026.
Katika mechi hiyo iliyopigwa juzi, Ufaransa ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 2-1, lakini mabeki wake wawili, Aude Bizet na Landryna Lushimba, walibadilisha matokeo kipindi cha pili.
Bizet, ambaye pia alikuwa nahodha na baadaye akachaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi, alisawazisha dakika ya 48 baada ya kufunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Juliane Denizot.
Lushimba alimalizia kazi hiyo dakika ya 87, akifunga bao la ushindi baada ya kona iliyopigwa na Ornella Graziani na kuipa Ufaransa pointi tatu muhimu.
Lushimba amesema ushindi huo haukuwa wa mtu mmoja, bali matokeo ya kazi ya timu. “Nilimshukuru Mungu kwa sababu nilihisi bao likija litaturudisha mchezoni, tulibaki pamoja na huu ulikuwa ushindi wa timu. Sikuwa mimi peke yangu, kila mmoja alifanya kazi,” amesema.
Kwa upande wake Bizet amesema mechi hiyo, imeifanya timu yao kuwa imara zaidi, huku akisisitiza walikosa kutumia baadhi ya nafasi walizotengeneza.
“Tumepata ugumu kumalizia nafasi zetu, lakini michezo kama hii inatufanya kuwa imara zaidi na tutakuwa tayari kwa kitakachofuata,” amesema Bizet.
Kocha Philippe Joly amesema alilazimika kubadilisha mfumo baada ya kuona sare haitoshi, hasa baada ya Ufaransa kuanza kampeni kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Korea Kusini.
Joly aliwaingiza Lina Gay na Celia Chabod kipindi cha pili na kuwaagiza kuongeza mashambulizi, uamuzi uliozaa matunda na kuifanya timu hiyo irejee mchezoni.
“Tulibadilisha mambo kidogo na wasichana waliitikia vizuri. Kuna njaa kubwa ndani ya kundi hili na moyo wao wa pamoja ulikuwa mzuri,” amesema Joly.
Ushindi huo umeonyesha pia, Ufaransa ina silaha kwenye mipira ya adhabu, baada ya mabao mawili ya ushindi dhidi ya Ecuador kufungwa kupitia mipira iliyokufa.