Straika Kagera Sugar aanza tizi
Muktasari:
- Nyota huyo Mtanzania aliyekuwa anaichezea Kariobangi Sharks ya Kenya msimu wa 2025-2026, amerejea Tanzania na kujiunga na Kagera Sugar, baada ya mkataba wake kuisha, ingawa alikumbwa na majeraha ya misuli ya paja yaliyomfanya asionekane.
MSHAMBULIAJI mpya wa Kagera Sugar, Ally Salum ameanza rasmi mazoezi na timu hiyo, baada ya kushindwa kuitumikia tangu alipojiunga na kikosi hicho, Agosti 3, 2026, akitokea Kariobangi Sharks inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya.
Nyota huyo Mtanzania aliyekuwa anaichezea Kariobangi Sharks ya Kenya msimu wa 2025-2026, amerejea Tanzania na kujiunga na Kagera Sugar, baada ya mkataba wake kuisha, ingawa alikumbwa na majeraha ya misuli ya paja yaliyomfanya asionekane.
Tangu ajiunge na kikosi hicho Agosti 3, 2026, hajacheza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2026-2027, kwa sasa ameanza mazoezi na muda wowote ataanza kuitumikia timu hiyo, inayofundishwa na Kocha Mkuu, Mrundi Cedric Kaze.
Akizungumza na Mwanaspoti, meneja wa timu hiyo, Ronald Okoth, amesema mchezaji huyo ameanza mazoezi na wenzake na kabla ya Ligi Kuu Bara kurejea, mshambuliaji huyo atakuwa yuko fiti kwa asilimia 100, kwa ajili ya kukitumikia kikosi hicho.
Nyota huyo amekuwa na rekodi mbaya, kwani akiichezea Kariobangi Sharks mwishoni mwa mwaka 2024, alipata pia majeraha ya goti yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kucheza kutokana na kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita akiuguza.
Pia, Machi 2026, mshambuliaji huyo alipata majeraha ya kifundo cha mguu, wakati timu hiyo ya Kariobangi Sharks ilipokuwa inacheza dhidi ya Tusker FC, jambo lililochangia kukosa mechi zote zilizobakia za kikosi hicho katika Ligi Kuu ya Kenya.