Leo ndio leo… Droo ya makundi Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Katika droo hiyo wenyeji Canada, Mexico na Marekani wanatarajiwa kuwekwa poti namba moja, kisha timu nyingine 39 zilizobakia zitapangwa katika poti nne ambazo zitakuwa na timu 12 kila moja, kulingana na viwango vyao vya ubora vya FIFA ambavyo mara ya mwisho kuangaliwa ilikuwa ni Jumatano, Novemba 19.
WASHINGTON, MAREKANI: HUKU siku zikiwa zinazidi kwenda kabla ya kuanza kwa michuano ya kwanza ya Kombe la Dunia itakayohusisha timu 48 na kufanyika huko Marekani, Canada na Mexico, leo ni siku ambayo droo ya kupanga makundi ya michuano hiyo itafanyia kwenye ukumbi wa mikutano wa John F. Kennedy Center jijini Washington.
Katika droo hiyo wenyeji Canada, Mexico na Marekani wanatarajiwa kuwekwa poti namba moja, kisha timu nyingine 39 zilizobakia zitapangwa katika poti nne ambazo zitakuwa na timu 12 kila moja, kulingana na viwango vyao vya ubora vya FIFA ambavyo mara ya mwisho kuangaliwa ilikuwa ni Jumatano, Novemba 19.
Pia kutakuwa na nafasi zilizoachwa wazi za timu ambazo bado zinapambana ili kufuzu kutoka mabara tofauti ambapo kutakuwa na nafasi mbili za mabara ya Asia, Africa na Australia pia nafasi nne za bara la Ulaya.
Timu wenyeji katika kapu la droo vipira vyao vitawekwa rangi kuashiria utambulisho wao, ikianzia kwa A1 Mexico kimpira chao kitakuwa na rangi ya kijani, B1 Canada (rangi nyekundu) na D1 Marekani (rangi ya bluu).
Timu nyingine tisa zilizobakia vimpira vya rangi moja kama ilivyo kawaida ya taratibu ilivyozoeleka.
Ili kuhakikisha kuna usawa katika droo, timu nne zinazoongoza katika viwango vya ubora vya FIFA zitapangwa katika namna ambayo hazitoweza kukutana katika hatua ya 16 bora wala robo fainali.
Timu hizo ni pamoja na Hispania na Argentina, lakini pia zile zinazoshika nafasi ya tatu na ya nne ambazo ni Ufaransa na England pia hazitokutana hadi fainali.
Katika droo hii pia kutokana na muundo wake, hakuna kundi ambalo litakuwa na zaidi ya timu moja kutoka bara moja isipokuwa Ulaya ambayo inawakilishwa na timu 16, hivyo kwa upande wao kundi moja linaweza kuwa na timu mbili kutoka bara hilo lakini haitozidi hapo.
Baada ya droo, timu zitatakiwa kusubiri kwa saa 24, kabla ya kutoka kwa ratiba, viwanja na muda ambao zitacheza mechi zao za makundi ingawa kwa mujibu wa BBC ni kwamba utaratibu utakuwa ni timu ya kwanza katika kundi itacheza dhidi ya ile ya pili na ya pili itacheza dhidi ya ile ya tatu kwa mechi za mwanzo.
Mbali ya uwepo wa rais wa Marekani Donald Trump katika droo hiyo, mastaa kibao pia watakuwapo kwa ajili ya kuchezesha ambapo ni pamoja na Tom Brady, mshindi mara saba wa NFL Super Bowl,
Wayne Gretzky, gwiji wa NHL na mshindi mara nne wa Stanley Cup, Aaron Judge, mchezaji wa MLB aliyechaguliwa mara saba kushiriki All-Star akiwa na New York Yankees na Shaquille O’Neal, mshindi wa ubingwa wa NBA mara nne.
Staa wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand ndio atakuwa muongozaji akisaidiwa na mchezaji wa mpira wa miguu wa kike wa Marekani Samantha Johnso pia katika zulia jekundu mchezaji wa zamani wa Rugby nchini Marekani ambaye kwa sasa ni mwandishi wa habari, Eli Manning atasimamia shoo.
POTI ZILIVYO
Pot 1: Canada, Mexico, USA, Hispania, Argentina, Ufaransa, England, Brazil, Ureno, Uholanzi, Ubelgiji, Ujerumani
Pot 2: Croatia, Morocco, Colombia, Uruguay, Uswisi, Japan, Senegal, Iran, Korea Kusini, Ecuador, Austria, Australia
Pot 3: Norway, Panama, Misri, Algeria, Scotland, Paraguay, Tunisia, Côte d’Ivoire, Uzbekistan, Qatar, Saudi Arabia, Afrika Kusini
Pot 4: Jordan, Cabo Verde, Ghana, Curacao, Haiti, New Zealand pamoja na washindi wanne wa mechi za mtoano Ulaya na nafasi mbili za mashindano maalum ya Mchujo ya FIFA ambayo yanajumuisha mabara mengine ikiwamo Afrika.