Kwa viungo hawa, Man United inamuhitaji Carlos Baleba
Muktasari:
- Santos na Tielemans walipewa nafasi ya kuanza nyuma ya nahodha Bruno Fernandes, lakini walishindwa kuonyesha ubora uliotarajiwa na wote wawili walitolewa dakika ya 67.
MANCHESTER, ENGLAND: VIUNGO Youri Tielemans na Andrey Santos wameonyesha kwa nini Manchester United inahitaji kwa udi na uvumba kumsajili Carlos Baleba baada ya viungo hao kushindwa kuonyesha kiwango katika kipigo cha 2-0 dhidi ya Hull City katika mchezo wa kwanza wa ushindani chini ya kocha mpya Michael Carrick.
Santos na Tielemans walipewa nafasi ya kuanza nyuma ya nahodha Bruno Fernandes, lakini walishindwa kuonyesha ubora uliotarajiwa na wote wawili walitolewa dakika ya 67.
Hata hivyo, kuingia kwa Kobbie Mainoo na Benjamin Sesko hakukubadilisha hali ya mchezo, huku United ikishindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa dhidi ya Hull.
Kutokana na udhaifu huo katikati ya uwanja, United sasa inaendelea kusaka kiungo wa tatu katika dirisha hili la usajili, jambo linaloweza kuifanya Brighton kuongeza dau la kiungo wake Carlos Baleba.
Taarifa zinaeleza kuwa United imefikia makubaliano ya ada ya karibu pauni65 milioni kwa ajili ya Baleba, lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa klabu hiyo katika eneo la kiungo, Brighton inaweza kuwa na nafasi ya kudai fedha zaidi.
Baleba anaonekana kuwa aina ya kiungo ambaye United inamhitaji kwa sasa. Tofauti na Santos na Tielemans, raia huyo wa Cameroon ana uwezo wa kupandisha mpira kutoka eneo la chini, kukimbia umbali mrefu na kusaidia timu katika maeneo mbalimbali ya uwanja.
Pia, ana uwezo wa kupiga pasi za umbali mrefu na kufanya mashambulizi ya kushtukiza akiwa anatokea nyuma.
Sifa hizo hazikuonekana kwa Santos na Tielemans dhidi ya Hull.
Santos aliyesajiliwa kutoka Chelsea kwa ada ya pauni50 milioni, alikuwa miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri wakati wa maandalizi ya msimu mpya. Akiwa pamoja na Mason Mount, aliyesajiliwa pia kutoka Chelsea kwa pauni65 milioni, alionyesha kiwango kizuri kwenye ziara ya maandalizi.
Lakini dhidi ya Hull, Santos alionekana kushindwa kuonyesha uwezo huo.
Alikamilisha pasi 52 kati ya 56, sawa na asilimia 93, lakini karibu nusu ya pasi hizo zilipigwa katika eneo la nusu ya uwanja ya Man United.
Pia, alipoteza mpira mara tano na alifanya mara moja tu la kubeba mpira kwa kusogeza timu mbele, licha ya Hull kujilinda karibu na eneo lao la hatari.
Kwa kawaida Santos ni mchezaji anayependa kuvunja mistari ya wapinzani kwa kupandisha mpira, lakini dhidi ya Hull alishindwa kuwa na ushawishi mkubwa.
Alifanya faulo moja na akamaliza mchezo akiwa ameokoa mipira mitatu ya hatari, idadi iliyokuwa kubwa kuliko nafasi alizotengeneza.
Kwa upande mwingine, Tielemans naye alishindwa kabisa kuingia kwenye mchezo.
Kiungo huyo wa Ubelgiji, aliyesajiliwa kutoka Aston Villa kwa pauni35 milioni, alikamilisha chini ya asilimia 50 ya pasi zake 62 katika eneo la Hull.
Alipoteza mpira mara tano alipokuwa akijaribu kupeleka mchezo mbele katika eneo la kati la uwanja, huku akishindwa pia kuwa na ushawishi alipokuwa na mpira.
Hull ilifanikiwa kumpokonya mpira mara 11, huku wachezaji wake wakimpita mara kwa mara walipokuwa wakishambulia.
Tielemans alifanya faulo moja, alipitishwa na wapinzani mara mbili na hakufanya mchango wowote wa kiulinzi.
Kwa kuzingatia kiwango hicho, hata Baleba, ambaye alikumbana na msimu mgumu akiwa Brighton, anaonekana kuwa na uwezo wa kuongeza nguvu na kasi katika safu ya kiungo ya United.
Carrick sasa atalazimika kutafuta suluhisho la haraka ikiwa anataka kuifanya United ianze kuonyesha dalili za ushindani.
Kocha huyo alikuwa ameisifia safu ya msingi ya kikosi chake, akiamini inaweza kuisukuma United katika mbio za ubingwa, lakini kipigo dhidi ya Hull kimemweka katika wakati mgumu.
Mainoo aliachwa benchi tangu mwanzo, jambo lililowauzi baadhi ya mashabiki.
Baadhi ya mashabiki wa United pia walimkosoa vikali Santos na Tielemans kupitia mitandao ya kijamii, wakidai hawakuonyesha kiwango kinachostahili kuanza katika kikosi hicho.
Mmoja amesema Santos bado hayuko tayari kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza, huku mwingine akidai Tielemans alicheza kwa kiwango duni sana.
Shabiki mwingine amesema Santos na Tielemans walipata wakati mgumu hata kuutunza mpira.
Kwa mashabiki wengi wa United, ujio wa Baleba hauwezi kuja mapema zaidi, kutokana na hali ilivyo sasa katika eneo la kiungo.
MASHABIKI WAWASHUKIA MAGUIRE, MAZRAOUI
Mashabiki wa Manchester United walikasirika baada ya mabeki Harry Maguire na Noussair Mazraoui kuonekana wakikabana wenyewe wakati Hull City ilipofunga bao la kwanza katika mchezo uliomalizika kwa United kupoteza 2-0.
Hull, iliyopanda daraja msimu huu, iliishtua United dakika ya 17 kupitia beki Semi Ajayi alifunga bao lililoifanya mashabiki wa Hull kushangilia kwa nguvu, kabla ya VAR kulikagua na hatimaye kulithibitisha.
Hata hivyo, kilichowavutia zaidi mashabiki ni tukio lililotokea ndani ya eneo la hatari la United kabla ya mpira kuingia wavuni.
Marudio ya picha yalionyesha Maguire akiwa amemshikilia Mazraoui kwa mikono wakati wachezaji hao wawili walipokuwa wakijaribu kuzuia hatari katika mpira wa kona.
Tukio hilo liliwaacha mashabiki wakishangaa na haraka wakaanza kulizungumzia kwenye mitandao ya kijamii.
Shabiki mmoja aliandika: “Maguire alikuwa amemshikilia Mazraoui. Manchester United inahitaji mabeki sasa hivi! De Ligt na Martinez wana majeraha, wakati wao ndio mabeki wetu bora wa kati.”
Mwingine alihoji: “Najiuliza Maguire alikuwa anafanya nini kumkumbatia Mazraoui wakati wa kona badala ya kumlinda mpinzani?”
Shabiki wa tatu aliandika kwa kejeli: “Mazraoui, Maguire, Heaven, Shaw mwaka 2026.”
Tukio hilo limeongeza maswali kuhusu uimara wa safu ya ulinzi ya United baada ya timu hiyo kuanza msimu kwa kipigo cha 2-0 dhidi ya Hull.