Kutoka uwanjani hadi kwenye skripti, Ronaldo aanza safari mpya
Muktasari:
- Tamthilia hiyo imejengwa juu ya wazo asilia la wakala wa soka, Darren Dein, na inamfuatilia wakala wa kubuni wa soka huko England anayeitwa Stanley Dalton, ambaye ataigizwa na mwigizaji Damian Lewis.
LONDON, ENGLAND: NYOTA Al Nassr na Ureno, Cristiano Ronaldo anatarajiwa kuwa mtayarishaji na pia mmoja wa waigizaji katika tamthilia mpya ya televisheni iitwayo "Day 1s" akishirikiana na mwongozaji mashuhuri Matthew Vaughn, kwa mujibu wa The Sun.
Tamthilia hiyo imejengwa juu ya wazo asilia la wakala wa soka, Darren Dein, na inamfuatilia wakala wa kubuni wa soka huko England anayeitwa Stanley Dalton, ambaye ataigizwa na mwigizaji Damian Lewis.
Mbali na kuwa mtayarishaji mkuu, Ronaldo pia ataonekana kwenye tamthilia hiyo pamoja na nyota wa zamani wa Ufaransa Thierry Henry na mwanamuziki Dave. Hadithi yake inaendana kwa kiasi kikubwa na ile ya The Playoffs, tamthilia ya hivi karibuni kutoka Brazil inayozungumzia maisha na shughuli za mawakala wa soka.
Day 1s ndiyo tamthilia ya kwanza ya televisheni kutolewa na UR Marv Studios, kampuni iliyoanzishwa kwa ushirikiano kati ya Ronaldo na Matthew Vaughn anayefahamika kwa kuongoza na kutayarisha filamu maarufu kama Kingsman, X-Men: First Class na Lock, Stock and Two Smoking Barrels.
Upigaji picha wa tamthilia hiyo tayari umeanza jijini London na unafadhiliwa kikamilifu na UR Marv Studios. Mbali na tamthilia hiyo, kampuni hiyo tayari imekamilisha utayarishaji wa filamu mbili za michezo.
Akiwa na umri wa miaka 41 na akiendelea kuichezea Al Nassr ya Saudi Arabia, Ronaldo anaonekana kuanza sura mpya katika maisha yake nje ya soka.