Kundi D WAFCON kuna mechi mbili kali
Muktasari:
- Mechi ya kwanza itawakutanisha Ghana dhidi ya Cape Verde mechi itakayopigwa saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Moulay Rachid, Casablanca, kabla ya Cameroon kuvaana na Mali saa 3:00 usiku katika Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca.
LEO, Julai 29, zinapigwa mechi mbili kundi D la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026.
Mechi ya kwanza itawakutanisha Ghana dhidi ya Cape Verde mechi itakayopigwa saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Moulay Rachid, Casablanca, kabla ya Cameroon kuvaana na Mali saa 3:00 usiku katika Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca.
Licha ya kuwa ni mechi za kwanza, lakini matokeo ya mechi hizo yanaweza kuweka mwelekeo wa kundi hilo ambalo linatajwa kuwa miongoni mwa makundi yenye ushindani mkubwa kutokana na historia na ubora wa timu zinazounda kundi hilo.
Ghana inaingia ikiwa moja ya timu zenye uzoefu mkubwa kwenye WAFCON. Black Queens wamewahi kushika nafasi ya pili mara tatu (1998, 2002 na 2006), pia walimaliza nafasi ya tatu mara mbili.
Hata hivyo, hawajawahi kutwaa ubingwa wa Afrika na wanarejea kwenye michuano hii wakiwa na matumaini makubwa.
Kwa upande wa Cape Verde, hii ni mara yao ya kwanza kushiriki WAFCON, jambo linalowafanya kuwa wageni kwenye mashindano hayo.
Mechi ya usiku inatarajiwa kuwa ngumu zaidi kwani inazikutanisha timu mbili zenye uzoefu wa michuano ya Afrika.
Cameroon ni moja ya mataifa makubwa katika soka la wanawake Afrika. Indomitable Lionesses walifika fainali ya WAFCON mwaka 2014 na kumaliza nafasi ya pili, huku pia wakitwaa nafasi ya tatu mara kadhaa.
Pia waliwahi kufuzu Kombe la Dunia la FIFA mara mbili mfululizo mwaka 2015 na 2019.
Mali nao si wageni kwenye mashindano hayo mafanikio makubwa yalikuwa 2018 walipomaliza nafasi ya nne, huku ikiwa moja ya timu zenye nidhamu ya kiuchezaji na inayoweza kuwapa wakati mgumu wapinzani wakubwa.
Katika historia ya WAFCON, Cameroon na Mali wamekutana mara mbili. Cameroon ilishinda mechi zote mbili, ikiwemo ushindi wa mabao 3-0 mwaka 2016 na 3-1 mwaka 2018, jambo linaloipa rekodi nzuri kuelekea mchezo wa leo.