Kona yatupa taulo! Jinsi 'Tyson mpya' Moses Itauma alivyochapwa TKO
Muktasari:
- Huo ulikuwa usiku wa giza kwa ndondi za Uingereza, lakini wenye mvuto mkubwa kutazamwa baada ya Itauma kuchapwa kwa Technical Knockout (TKO) katika raundi ya tisa ya pambano la ubingwa wa uzito wa juu duniani la IBF.
LONDON, ENGLAND: KAULI iliyotia hofu zaidi katika tukio la kichapo cha bondia Moses Itauma ilitolewa na shujaa wa Croatia, Filip Hrgovic ambaye ndiye aliyekuwa stori kubwa usiku wa Jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa O2 Arena, jijini London.
Huo ulikuwa usiku wa giza kwa ndondi za Uingereza, lakini wenye mvuto mkubwa kutazamwa baada ya Itauma kuchapwa kwa Technical Knockout (TKO) katika raundi ya tisa ya pambano la ubingwa wa uzito wa juu duniani la IBF.
Baada ya kumchapa, Hrgovic amesema kuhusu Itauma: “Hapana, sikuhisi kama nguvu zozote.”
Kauli hiyo imetafsiriwa kuwa pigo kubwa kwa kijana huyo aliyewahi kusifiwa kuwa Mike Tyson mpya, sawa na James Bond kuambiwa kwamba hana tena mvuto kwa wanawake. Huenda ikauma zaidi hata kuliko ngumi zilizompeleka kutoka kutawala pambano hadi kushindwa na kulazwa hospitali usiku ambao alitarajiwa kuwa bingwa wa pili kwa umri mdogo zaidi katika historia ya uzito wa juu.
Nguvu imekuwa kama jina la kati la Moses Itauma tangu alipoanza kuwaangusha vigogo kama miti midogo. Ghafla, akiwa na umri wa miaka 21, anaanza kufananishwa na Samson aliyepoteza nguvu zake za kizushi baada ya kukatwa nywele kwenye hadithi za kitabu cha Biblia.
Je, kulikuwa na dalili katika namna Hrgovic alivyonusurika raundi nane za kwanza za pambano hilo la ubingwa wa dunia wa IBF na kuvumilia makonde mengi ambayo kila moja ilionekana kana kwamba ingemwangusha hata farasi? Kusema hivyo kungekuwa kupuuza moyo wa kishujaa na uwezo wa ajabu wa Hrgovic kuvumilia maumivu, ambao ulimwezesha kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kutwaa ubingwa wa dunia.
Na alifanya hivyo akiwa na umri wa miaka 34. Hata hivyo, Itauma hakufanikiwa kumaliza pambano kwa kumchapa Hrgovic. Hilo linaibua masuala mengine. Inatia wasiwasi pia kuona ‘simba huyo mdogo’ wa Uingereza akiishiwa nguvu katika pambano la kwanza kabisa la maisha yake lililomlazimisha kwenda zaidi ya raundi sita.
Kocha Ben Davison sasa anakabiliwa na maswali kuhusu kama kutegemea kwamba Itauma angepata ushindi wa KO mapema kulimfanya asijenge stamina ya kutosha. Au je, alijimaliza mwenyewe kwa kutumia nguvu nyingi katika mashambulizi yake?
Sababu yoyote ile, ilikuwa jambo la kutia wasiwasi kumuona kijana huyo akiwa amechoka kiasi kile akiwa na umri mdogo, huku akiyumba kuelekea kushindwa mapema raundi ya tisa. Hrgovic aliweka kwa maneno kile ambacho wengi walihisi Itauma alishindwa.
Bingwa huyo mpya, ambaye kabla ya pambano alikuwa ameapa “kuuharibu uso wa kijana huyo na kumrudisha shule ya sekondari,” na baada ya kufanya hivyo amesema: “Ana kipaji kikubwa, lakini alipigana kama bondia wa ridhaa na anapaswa kujifunza kupigana kama bondia wa mtalaamu.
Akiwa na uzoefu zaidi angejua kwamba alikuwa akishinda kila raundi na alichopaswa kufanya ni kumaliza pambano kwa kutumia jab yake hadi kupata ushindi wa pointi. Hakupaswa kuendelea kujaribu kunipiga kwa KO. Ingawa nilijua kwamba angechoka kadiri pambano lilivyoendelea.”
Lakini kuhusu madai kwamba Itauma hakuwa na nguvu kwenye ngumi zake? Alipoulizwa kuhusu kuangushwa mara moja kwa muda mfupi katika raundi ya pili, Hrgovic amesema: “Sikuhisi. Ana kasi sana na alinipiga wakati sikuwa nimejiweka sawa kwa ngumi ambayo sikuiona ikija.”
Na hivyo ndivyo ilivyotokea kwamba katika pambano la vizazi viwili, ilikuwa kona ya kijana huyo ndiyo iliyolazimika kutupa taulo jeupe ulingoni.
Kufikia wakati huo, haikuwa tena jambo la kushangaza. Tangu raundi ya tano, Itauma alikuwa ameanza kukunja uso kutokana na mahitaji makubwa ya kimwili yaliyokuwa yakimkabili pamoja na makonde mazito aliyokuwa akipokea.
Katika raundi ya nane alianzisha mashambulizi makali ya kukata tamaa, lakini Hrgovic hakuyavumilia tu, bali pia alifanikiwa kumuumiza kwa makonde yake. Kwa sifa yake, Itauma alijaribu kutupa baadhi ya ngumi mwanzoni mwa raundi ya tisa, lakini alionekana zaidi kama samaki anayepigapiga akiwa ametolewa majini.
Hrgovic alimpiga kwa nguvu ambazo yeye mwenyewe aliziita “nguvu zilizotoka kwa Yesu Kristo.”
NI TYSON MPYA?
Kinachoulizwa ni nini kinamfuata kwa bondia aliyewahi kutajwa kuwa Mike Tyson mpya? Ushauri wa Hrgovic ni huu: “Mapambano kadhaa mepesi ili kupata uzoefu zaidi na kujenga tena kujiamini. Na naamini kwamba kwa kasi aliyonayo ya mikono siku moja atakuwa bingwa wa dunia.”
Promota Frank Warren alionyesha pia huruma kwa Itauma akisema: “Kushindwa kwa mara ya kwanza kunaondoa ile hali ya kutoshindwa. Tutampa Moses muda wote anaohitaji kupona kutokana na hilo. Bado ni kipaji cha kipekee sana.” Wakati huohuo, maisha katika uzito wa juu yanaendelea. Warren ametangaza Oktoba 17 katika Ukumbi wa O2 Arena pambano la marudiano la ubingwa wa dunia wa WBO kati ya bingwa Daniel Dubois na Fabio Wardley, aliyewahi kuwa bondia wa ridhaa kabla ya kuingia katika ulimwengu wa ngumi za kulipwa, pambano ambalo linatarajiwa kuwa la kusisimua.
Na Hrgovic atafanya utetezi wake wa kwanza wa ubingwa dhidi ya mpinzani wa lazima kutoka Cuba, Frank Sanchez kwani tayari ametangaza azma yake akisema: “Nataka kuendelea hadi kwenye pambano la kuunganisha mikanda dhidi ya Daniel.” Itachukua muda kabla ya Itauma kurejea kwenye mapambano, kwani sasa atalazimika kuanzia nyuma kwenye foleni.
Inaelezwa kwamba baada ya kulazwa alitoka hospitali Jumapili akianza kipindi cha kupona kutokana na kipigo kikali alichopokea pamoja na jeraha la mguu alilolipata. Hata hivyo, majeraha ya kisaikolojia yanaweza kuchukua muda mrefu zaidi kupona. Kwa sasa itabidi asome kilichowabeba mabondia Muhammad Ali, Joe Louis, Joe Frazier, George Foreman na Lennox Lewis waliopoteza zaidi ya pambano moja na baadaye wakarejea na kuwa mabingwa.
Lakini je, Moses Itauma ndiye Mike Tyson mpya? Hata wakati Filip Hrgovic akirejea nyumbani Zagreb, Croatia, kupokea mapokezi anayostahili kama shujaa kuna jambo moja unaloweza kulizungumza kwa uhakika, “bado ana nafasi ya kurejea na kusumbua”.