Afrika katika namba Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Mchezo huo utachezwa jijini New Jersey, Marekani kuanzia saa 4:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.
FAINALI za Kombe la Dunia 2026 zinafikia tamati leo kwa mechi ya fainali inayozikutanisha Hispania na Argentina.
Mchezo huo utachezwa jijini New Jersey, Marekani kuanzia saa 4:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.
Afrika iliwakilishwa na timu 10 kwenye mashindano hayo lakini kwa bahati mbaya hakuna hata moja ambayo iliingia hatua ya nusu fainali.
Morocco pekee ndio ilijitutumua na kufika hatua ya robo fainali huku Misri ikiishia hatua ya 16 bora, wakati huo, Algeria, Ghana, Ivory Coast, Cape Verde, Afrika Kusini, Senegal na DR Congo zikikwamia katika hatua ya 32 bora na Tunisia iliondolewa mapema kwenye hatua ya makundi.
Takwimu zifuatazo, zinaangazia ushiriki wa timu za Afrika kwenye Kombe la Dunia 2026.
53
Katika mechi 41 za Fainali za Kombe la Dunia 2026, timu za Afrika zimefunga jumla ya mabao 53.
Idadi kubwa ya mabao ya wawakilishi wa Afrika imefungwa katika hatua ya makundi, kisha hatua ya 32 bora na hatua ya 16 bora.
Timu 10 za Afrika zilizoshiriki mashindano hayo, katika hatua ya makundi zimefunga mabao 40 huku mabao nane yakifungwa kwenye hatua ya 32 bora na katika hatua ya 16 bora, mabao matano tu yamewekwa kimiani.
Morocco na Senegal ndio timu za Afrika zilizofunga idadi kubwa zaidi ya mabao kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu ambapo kila moja imefunga mabao 10.
Inayofuata ni Misri iliyoweka kimiani mabao nane, Ivory Coast, DR Congo na Algeria kila moja imepachika mabao matano, Cape Verde imefunga mabao manne, huku Afrika Kusini, Tunisia na Ghana kila moja ikifunga mabao mawili.
02
Ni mabao mawili tu ya kujifunga kwa timu za Afrika kwenye Kombe la Dunia ambayo yote yalitikisa nyavu za Misri.
Kwa bahati mbaya zaidi, ni mchezaji mmoja ambaye alijifunga mabao yote hayo mawili ambaye ni beki Mohamed Hany aliyejifunga katika mechi dhidi ya Ubelgiji na dhidi ya Australia.
64
Timu za Afrika zimeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 64 katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.
Tunisia ndio timu iliyofungwa idadi kubwa zaidi ya mabao kati ya 10 zilizopeperusha bendera ya bara letu ambapo imeruhusu nyavu zake kufumaniwa mara 12.
Ghana imeondoka katika mashin dano hayo ikiwa ndio timu ya Afrika iliyofungwa idadi ndogo zaidi ya mabao kulinganisha na nyingine ambapo imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu.
Timu nyingine na idadi mabao ambayo kila moja imefungwa kwenye mabano ni Morocco (6), Misri (7), Ivory Coast (4), DR Congo (5), Afrika Kusini (4), Algeria (9), Senegal (9) na Cape Verde (5).
04
Ismaila Sarr wa Senegal ndio nyota wa Afrika aliyefunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu ambapo amefumania nyavu mara nne.
Alifunga mabao mawili dhidi ya Norway na moja dhidi ya Iraq katika hatua ya makundi na kwenye hatua ya 32 bora akapachika bao moja dhidi ya Ubelgiji.
Wanaomfuata Ismaila Sarr ni mshambuliaji wa Morocco, Ismael Saibari na nyota wa DR Congo, Yoanne Wissa ambao kila mmoja amepachika mabao matatu.
12
Kwa wawakilishi wa Afrika mwaka huu, Timu ya taifa ya Misri ndio imeongoza kwa kupata idadi kubwa ya kadi kwenye Fainali za Kombe la Dunia ambapo imeondoka na idadi ya kadi 12 zote zikiwa za njano.
Inafuatiwa na Morocco ambayo imepata idadi ya kadi saba, zote zikiwa za njano sawa na Afrika Kusini ambayo nayo ina idadi hiyo ya kadi huku tano zikiwa za njano na mbili nyekundu.
DR Congo yenyewe imepata idadi ya kadi sita zote zikiwa za njano sawa na Ghana.
Cape Verde imepata kadi tano ambazo ni za njano, Ivory Coast ina kadi nne zote zikiwa za njano, Algeria na Senegal nazo zina kadi tatu kila moja, zote zikiwa za njano na Tunisia ina kadi moja ambayo ni ya njano.
Ikumbukwe, ni wachezaji wawili tu wa timu za Afrika walioonyeshwa kadi nyekundu kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026 ambao wote nj wa Afrika Kusini.
Sh26 bil
Fedha ambazo Tunisia imepata kutoka FIFA baada ya ku ishia katika hatua ya makundi kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia mwaka huu.
Timu zilizokomea kwenye makundi, kila moja inapata kifuta jasho cha Dola 10 milioni (Sh26 bilioni).
Sh32 bil
Timu za Algeria, Cape Verde, Ivory Coast, Ghana na Afrika Kusini kila moja imevuna kiasi cha Dola 12 milioni (Sh32 bilioni) kwa kuishia hatua ya 32 bora.
Sh42 bil
Misri imepata kifuta jasho cha Dola16 milioni (Sh42 bilioni) kwa kuishia hatua ya 16 bora ya mashindano hayo.
Sh53 bil
Morocco ndio timu ya Afrika iliyovuna kiasi kikubwa zaidi cha fedha za bakshishi kwenye Kombe la Dunia 2026 kwa vile iliishia katika hatua ya robo fainali.
Timu inayoishia katika hatua hiyo inavuna kiasi cha Dola 20 milioni (Sh53 bilioni).