Kocha De Zerbi amtolea nje Richarlison
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa Brazil, mwenye umri wa miaka 29, aliondolewa kwenye kikosi cha wachezaji 25 cha Tottenham kinachoshiriki Ligi Kuu England baada ya kuomba kuondoka klabuni hapo mwezi uliopita.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Tottenham Hotspur, Roberto De Zerbi, amempa dongo kali mshambuliaji wake Richarlison, huku akisisitiza kuwa nyota huyo hatapewa nafasi ya kurejea kwenye kikosi licha ya timu hiyo kuwa na changamoto ya kufunga mabao.
De Zerbi jana alithibitisha kuwa Richarlison hatacheza dhidi ya Liverpool katika mchezo wa Kombe la Carabao, licha ya kuwa bado anaruhusiwa kushiriki michuano hiyo.
Mshambuliaji huyo wa Brazil, mwenye umri wa miaka 29, aliondolewa kwenye kikosi cha wachezaji 25 cha Tottenham kinachoshiriki Ligi Kuu England baada ya kuomba kuondoka klabuni hapo mwezi uliopita.
Hata hivyo, Richarlison bado anaweza kucheza kwenye mashindano ya vikombe, lakini De Zerbi amesema hakuna mpango wa kumrejesha kwenye kikosi.
“Richarlison, tayari mnajua kila kitu. Hakuna kilichobadilika kwa Carabao Cup wala Premier League. Hali bado ni ileile,” amesema De Zerbi.
Kauli hiyo imekuja wakati Tottenham ikiwa bado haijafunga bao katika Ligi Kuu msimu huu, lakini De Zerbi anaonekana kutokuwa tayari kumbadili msimamo wake kuhusu mshambuliaji huyo.
Richarlison alicheza katika kipigo cha mabao 3-0 ambacho Tottenham ilikumbana nacho dhidi ya Brentford katika mchezo wa kwanza wa msimu, kabla ya mvutano kuhusu hatma yake klabuni hapo kuibuka.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya mchezo dhidi ya Liverpool, De Zerbi alionekana kusisitiza zaidi kuhusu matokeo hayo alipoulizwa kama safari ya Richarlison ndani ya Tottenham imefikia mwisho.
“Sijui. Hilo si swali langu,” amesema De Zerbi.
Kisha akaongeza kwa msisitizo:
“Kwa vyovyote vile, tulifungwa 3-0 na Brentford tukiwa na Richarlison. Labda mlisahau. Nawakumbusha tu.”
Kocha huyo pia alifunga kabisa mjadala kuhusu uwezekano wa Richarlison kucheza dhidi ya Liverpool.
“Richarlison hatacheza hata kama anaruhusiwa. Hata kwenye Carabao Cup, hapana,” amesema.
ATOA JIBU
Kauli ya De Zerbi haikupita kimya kwa Richarlison, ambaye baadaye alitoa majibu ya kifupi kwenye mitandao ya kijamii baada ya taarifa ya Fabrizio Romano kunukuu kauli ya kocha huyo.
Richarlison aliweka emoji ya kulia kama jibu, kabla ya baadaye kuweka Instagram Story yenye picha ya nukuu ya De Zerbi iliyothibitisha kuwa hatacheza kwenye mchezo wa Kombe la Carabao.
Juu ya picha hiyo, Richarlison aliandika neno moja tu: “Why?” akifuatisha na emoji ya huzuni.
MAUZO YALIGOMA
Tottenham ilijaribu kumuuza Richarlison katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi, lakini mipango ya kumpeleka Everton, Trabzonspor na Vasco da Gama ilikwama baada ya kushindikana kwa makubaliano ya masuala binafsi.
Richarlison alikuwa mfungaji bora wa Tottenham msimu uliopita, lakini sasa anaonekana kuwa nje kabisa ya mipango ya De Zerbi, huku hatma yake katika klabu hiyo ikiwa bado haijulikani.