Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kawempe Muslim imestahili ubingwa CECAFA, mtihani upo CAF

Muktasari:

  • Timu hiyo ambayo kwa mwaka huu ni mara yao ya pili kushiriki fainali hizo baada yam waka 2024 kumaliza nafasi ya tatu imekuwa na mwendelezo mzuri kwenye mashindano ya CECAFA.

KAWEMPE Muslim Ladies imefanya kile ambacho timu nyingi za ukanda wa CECAFA zimekuwa zikishindwa kukifanya kwa miaka ya hivi karibuni kutawala mashindano ya kufuzu na kukata  tiketi ya kuiwakilisha Afrika Mashariki katika  fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika. Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kenya Police Bullets katika fainali iliyopigwa mjini Kigali umeipa Uganda mwakilishi wake wa kwanza katika fainali ya michuano hiyo ya Afrika.

Timu hiyo ambayo kwa mwaka huu ni mara yao ya pili kushiriki fainali hizo baada yam waka 2024 kumaliza nafasi ya tatu imekuwa na mwendelezo mzuri kwenye mashindano ya CECAFA.

Kawempe haikupata tiketi hiyo kwa bahati ilistahili kwani katika kampeni yake jijini Kigali, timu hiyo ilishinda mechi zote nne, ikifunga mabao 13 bila kuruhusu bao hata moja. Katika nusu fainali iliifunga Commercial Bank of Ethiopia (CBE) 3-0, kabla ya kuitandika Kenya Police Bullets kwa bao la Agnes Nabukenya dakika ya 100.

Katika Kundi B, Kawempe Muslim Ladies ilianza kampeni yake kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Commercial Bank of Ethiopia (CBE), kabla ya kuonyesha ubora mkubwa zaidi kwenye mchezo wake wa pili kwa kuichapa FC Ujeco ya Djibouti mabao 8-0. Matokeo hayo mawili yaliipa Kawempe nafasi ya kuongoza kundi na kufuzu hatua ya nusu fainali, ambako ilikutana tena na CBE na kushinda 3-0.

Sasa maswali wanayojiuliza wadau wa soka la wanawake ukanda huu ni Je ubora waliouonyesha kwenye fainali za CECAFA itaweza kuwa na mwendelezo Afrika ambapo zinawakutanisha mabingwa wa kanda tofauti na timu zenye ubora na ushindani mkubwa?.

Historia inaonyesha kuwa hilo limekuwa tatizo kwa mabingwa wengi wa ukanda huo. Tangu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake ianzishwe mwaka 2021, CECAFA imekuwa ikitoa wawakilishi wenye uwezo wa kushindana kikanda, lakini inapofika hatua ya fainali ya Afrika, timu nyingi zimekuwa zikikwama katika hatua ya makundi.

Vihiga Queens ya Kenya mwaka 2021, JKT Queens mwaka 2023 na 2025 pamoja na CBE mwaka 2024 ni miongoni mwa mabingwa wa Afrika walioishia hatua ya makundi.

REKODI YA SIMBA

Simba Queens ndio timu pekee yenye rekodi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa. Mwaka 2022, mabingwa hao wa Tanzania waliingia kwenye fainali za Morocco wakiwa mabingwa wa CECAFA baada ya kampeni iliyowapa matumaini makubwa.

Kwenye michuano ya kufuzu iliyochezwa Dar es Salaam, Simba ilishinda mechi zote tano, ikafunga mabao 18 na kuruhusu moja tu. Kwanza iliichapa Garde Républicaine ya Djibouti 6-0, ikaifunga She Corporate ya Uganda 2-0, kisha Yei Joint Stars ya Sudan Kusini 4-0. Nusu fainali iliifunga AS Kigali 5-1 na kwenye fainali ikairudia She Corporate kwa ushindi wa 1-0, bao la penalti la Vivian Aquino.

Hapo ndipo Simba ilipoonyesha tofauti kati ya kuwa bingwa wa ukanda na kuwa timu inayoweza kuendana na presha ya Afrika. Morocco ilianza kwa pigo baada ya Simba kufungwa 1-0 na wenyeji AS FAR katika mchezo wa kwanza wa Group A. Badala ya kuvurugika, kikosi hicho kikainuka na kuifunga Determine Girls ya Liberia 2-0, kisha Green Buffaloes ya Zambia 2-0 katika mchezo ambao kilihitaji ushindi ili kufuzu.

Simba Queens ilitinga nusu fainali ilipokutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kupoteza 1-0. Sundowns iliingia kwenye mchezo huo ikiwa bado haijapoteza katika mechi zake za mashindano hayo na ikaendelea na rekodi hiyo baada ya kuiondoa Simba.

Baada ya hapo Simba ilipoteza pia mchezo wa kuwania nafasi ya tatu kwa kufungwa 1-0 na Bayelsa Queens ya Nigeria na kumaliza nafasi ya nne. Hivyo, kwa Tanzania, Simba Queens ndiyo timu iliyofika mbali zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa.

Hapo ndipo ilipo kazi ya Kawempe. Ubingwa wa CECAFA ni hatua ya kwanza. Timu inaweza kutawala ukanda kwa kufunga mabao mengi, lakini ikija kukutana na timu za Afrika inahitaji kiwango kingine cha ushindani, hasa kwenye umiliki wa mpira, kasi ya maamuzi, uimara wa safu ya ulinzi na uwezo wa kustahimili presha dhidi ya mabingwa kutoka maeneo yenye ushindani mkubwa kama COSAFA, WAFU na UNAF.

Kwa Kawempe, jambo la kwanza la kujenga ni kuhifadhi msingi wa kikosi kilichofanya vizuri Kigali. Wachezaji wake wameonyesha wanaweza kucheza kwa nidhamu, kulinda na kutumia nafasi. Lakini katika fainali ya Afrika, haitoshi kuwa na rekodi nzuri ya kikanda. Lazima wawe tayari kukutana na timu yenye kasi zaidi, uzoefu mkubwa na wachezaji wanaoweza kubadilisha mchezo kwa tukio moja.

Kawempe imestahili kufuzu, lakini sasa ndiyo imeingia kwenye mtihani mkubwa. Ikiwa itajifunza kutoka kwa Simba Queens ambayo ilifika nusu fainali mwaka 2022 na kuboresha maeneo ambayo timu za CECAFA zimekuwa zikikwama, inaweza kuvuka kile ambacho Vihiga Queens, JKT Queens na CBE walishindwa kukifanya.

HUYU HAPA KOCHA

Kocha wa Kawempe Muslim, Ayub Khalifa Kiyingi, alisifu juhudi za wachezaji wake baada ya mchezo huo, akisema ushindi huo umetokana na kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi chote cha mashindano. “Tulicheza na timu ngumu lakini niwapongeze wachezaji wangu wamefanya kwa juhudi na kujitoa sana,” alisema.