KASHINDIKANA: Kane apiga bao 150 Bayern
Muktasari:
- Bayern ilianza kuonyesha ubabe dakika ya 26, wakati krosi ya chini ya Ismael Saibari ilipogonga mwili wa Kane na mpira kumkuta Lennart Karl aliyekuwa katika lango la mbali na kufunga kirahisi.
MUNICH, Ujerumani: MSHAMBULIAJI Harry Kane ameendelea kuandika historia Bayern Munich baada ya kufikisha mabao 150 katika kikosi hicho, huku bao lake likiipa miamba hiyo ya Ujerumani ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Elversberg kwenye mchezo wa Bundesliga.
Bayern ilianza kuonyesha ubabe dakika ya 26, wakati krosi ya chini ya Ismael Saibari ilipogonga mwili wa Kane na mpira kumkuta Lennart Karl aliyekuwa katika lango la mbali na kufunga kirahisi.
Elversberg, ambayo imekuwa kivutio katika msimu wake wa kwanza kabisa Bundesliga baada ya kuwashangaza Bayer Leverkusen na Borussia Monchengladbach, ilisawazisha dakika ya 61 kupitia Maurice Krattenmacher.
Lakini Kane alihakikisha pointi tatu zinabaki Munich baada ya kupokea mpira ndani ya eneo la hatari na kufyatua shuti kali lililompita kipa Nicolas Kristof upande wake wa karibu.
Bao hilo lilikuwa la 99 kwa Kane katika Bundesliga, akiwa amefikisha idadi hiyo katika mechi 97 pekee. Pia lilikuwa bao lake la kwanza katika kampeni ya Bundesliga msimu wa 2026/27.
Kwa upande mwingine, bao hilo lilimfikisha Kane kwenye mabao 150 katika mechi 153 katika mashindano yote tangu alipojiunga na Bayern akitokea Tottenham Hotspur Agosti 2023. Kane, mwenye umri wa miaka 33, ni miongoni mwa wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or ya mwaka 2026, ambayo itatolewa London mwezi Oktoba.
Tangu kuanza kwa msimu wa 2023/24, Kane amefunga mabao 10 zaidi ya mchezaji mwingine yeyote katika ligi tano kubwa za Ulaya, huku akifunga wastani wa bao moja kila dakika 79.
Pia aliweka rekodi ya kufikisha mabao 50 ya Bundesliga kwa kaharaka zaidi baada ya kufanya hivyo katika mechi 43 tu.
Sasa Kane anaelekea kuweka rekodi nyingine ya kufikisha mabao 100 kwa kasi zaidi katika Bundesliga.