Kane avunja rekodi ya miaka 37
Muktasari:
- Kane hakumaliza kwa kuvunja rekodi pekee, bali pia alifunga bao la ushindi kupitia penalti na kuifikisha idadi yake ya mabao ya kimataifa kuwa 92.
LONDON, ENGLAND: NAHODHA wa England, Harry Kane, ameendelea kujiweka kwenye orodha ya magwiji wa soka duniani baada ya kuvunja rekodi ya miaka 37 ya kucheza mechi nyingi zaidi katika kikosi cha timu ya taifa.
Kane aliweka historia hiyo Alhamisi usiku alipofikisha mechi 126 akiwa na jezi ya England, na kuipiku rekodi ya Peter Shilton aliyekuwa ameshikilia idadi hiyo kwa miaka mingi.
Usiku huo wa kihistoria uliambatana na ushindi wa England wa mabao 2-1 dhidi ya Croatia katika mchezo wa Ligi ya Mataifa (Nations League) uliochezwa Wembley.
Kane hakumaliza kwa kuvunja rekodi pekee, bali pia alifunga bao la ushindi kupitia penalti na kuifikisha idadi yake ya mabao ya kimataifa kuwa 92.
Kabla ya mchezo huo, Kane alipewa heshima maalumu, ambapo Shilton alimkabidhi zawadi ya kumbukumbu ya kufikisha mechi 126.
Baadaye, Prince William alimkabidhi jezi maalumu yenye jina lake na namba 126, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake kwa timu ya taifa.
Kane aliingia uwanjani akiwa na watoto wake wanne, huku mashabiki wakimshangilia na bango kubwa lenye picha yake na ujumbe wa kumtaja kama mmoja wa wachezaji bora wa England likiwa limewekwa uwanjani.
Heshima hizo zimekuja katika kipindi ambacho mshambuliaji huyo anaendelea kuvuna mafanikio makubwa katika soka la dunia.
Baada ya kutwaa tuzo ya Ballon d'Or siku 16 zilizopita, Kane sasa ameongeza rekodi nyingine kubwa katika historia ya timu ya taifa.
Mafanikio yake yanamuweka pamoja na magwiji kama Billy Wright, Bobby Charlton, Bobby Moore na Peter Shilton, ambao waliwahi kuweka viwango vikubwa vya mechi za kimataifa kwa England.
Wright alifikisha mechi 105, Charlton 106, Moore 108, kabla ya Shilton kufikisha 125 na hatimaye rekodi hiyo kuvunjwa na Kane.
Licha ya mafanikio hayo, Kane anaweza kuendelea kuongeza idadi ya mechi zake na huenda akakaribia kufikisha mechi 200 kabla ya kustaafu soka.
Pia anaongoza kwa mabao 92 ya England, rekodi ambayo inaonekana kuwa ngumu kuvunjwa kwa miaka mingi ijayo.
Hata hivyo, kuna jambo moja kubwa ambalo bado halijakamilika katika maisha yake ya soka la kimataifa; kutwaa taji kubwa akiwa na England.
Kane bado hajashinda Kombe la Dunia wala Euro akiwa na timu hiyo, jambo ambalo limekuwa likitajwa kama pengo pekee katika wasifu wake wa mafanikio.
Katika mchezo dhidi ya Croatia, England ilianza vizuri na kupata bao la kwanza kupitia Morgan Rogers, aliyemalizia mpira uliotokana na shambulizi lililoanzishwa na Kane kwa pasi nzuri ya umbali wa takribani mita 27.
Jude Bellingham alipokea pasi hiyo na kupeleka mpira mbele, kabla ya Rogers kuumalizia wavuni.
Hata hivyo, Croatia ilisawazisha dakika ya 60 baada ya Jarell Quansah kushindwa kuondoa vizuri mpira wa kona, hali iliyompa Petar Sucic nafasi ya kufunga.
Dakika tatu baadaye, Quansah alisababisha penalti baada ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Kane akasimama kuipiga na kufanikiwa kufunga kwa utulivu, akiupitisha mpira katikati ya lango huku kipa Dominic Livakovic akijirusha upande wa kushoto.
England ilifanikiwa kulinda ushindi huo hadi mwisho licha ya Croatia kupata nafasi kadhaa za kusawazisha.
Ushindi huo umeiweka England katika nafasi nzuri ya kuwania kumaliza kileleni mwa kundi lake la Nations League, huku mchezo ujao dhidi ya Hispania jijini Madrid ukiwa muhimu katika safari hiyo.
Kwa upande mwingine, kizazi kipya cha England kinaendelea kujengwa chini ya kivuli cha Kane, huku Jude Bellingham, Morgan Rogers, Anthony Gordon na Morgan Gibbs-White wakitajwa kuwa sehemu ya mustakabali wa timu hiyo.
Nyota chipukizi Rio Ngumoha pia alipewa nafasi ya kucheza dakika za mwisho dhidi ya Croatia.
Kane, ambaye alicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa Machi 2015 akiwa na umri wa miaka 21, sasa amekuwa alama muhimu katika historia ya England.
Amevunja rekodi, amevuna tuzo na kuthibitisha ubora wake kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi duniani.
Lakini kwake, mafanikio yote hayo hayatakuwa yamekamilika mpaka siku atakapoweza kuinua kombe kubwa akiwa na England.
Hilo ndilo taji analolihitaji zaidi ili kuhitimisha safari yake ya kihistoria akiwa nahodha wa Simba Watatu.