Kane aongoza mbio za Ballon d'Or, Bayern yamwandalia mrithi
Muktasari:
- Licha ya England kushindwa kutinga fainali ya Kombe la Dunia 2026, Kane ameendelea kuvutia kutokana na kiwango chake bora msimu uliopita, ambapo alifunga mabao 61 katika mashindano yote akiwa na Bayern Munich kabla ya kuongeza mabao sita kwenye fainali za Kombe la Dunia.
LONDON, England: NAHODHA wa England, Harry Kane, anaendelea kupewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo ya Ballon d'Or 2026 baada ya msimu wake bora akiwa Bayern Munich, huku mabingwa hao wa Ujerumani wakianza kupanga maisha ya baada yake kwa kumuweka Benjamin Sesko kwenye rada zao.
Licha ya England kushindwa kutinga fainali ya Kombe la Dunia 2026, Kane ameendelea kuvutia kutokana na kiwango chake bora msimu uliopita, ambapo alifunga mabao 61 katika mashindano yote akiwa na Bayern Munich kabla ya kuongeza mabao sita kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33 ameendelea kuthibitisha ubora wake nchini Ujerumani, akionekana kuzoea mazingira ya Bayern na kuwa mhimili muhimu wa kikosi hicho.
Hata hivyo, wakati wengi wakiamini Kane bado ana miaka kadhaa ya kucheza kwenye kiwango cha juu, Bayern tayari inaanza kufikiria mrithi wake.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Sport Bild, Christian Falk, mabosi wa Bayern wanaamini mshambuliaji wa Manchester United, Benjamin Sesko, ndiye chaguo sahihi la kurithi nafasi ya Kane siku zijazo.
Mpango wa Bayern si kumtoa Kane kikosini haraka, bali ni kumbadilisha majukumu kadri umri unavyoongezeka. Klabu hiyo inaamini mshambuliaji huyo anaweza kucheza zaidi kama kiungo mshambuliaji kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi, kutengeneza nafasi na kuunganisha safu ya ushambuliaji.
Hali hiyo ingeweza kumpa Sesko nafasi ya kucheza mbele yake kama mshambuliaji wa mwisho, kabla ya baadaye kuchukua jukumu hilo moja kwa moja pale Kane atakapopunguza kiwango au kuondoka klabuni.
Falk ameeleza kuwa wazo hilo lilianza kujadiliwa tangu Vincent Kompany alipoteuliwa kuwa kocha wa Bayern mwaka 2024, huku Sesko akiwa mmoja wa majina yaliyokuwa kwenye orodha ya muda mrefu ya klabu hiyo.
Sesko alijijengea jina akiwa Red Bull Salzburg kabla ya kung'ara kwa misimu miwili akiwa RB Leipzig, hatua iliyomuwezesha kujiunga na Manchester United kwa mkataba mkubwa unaomuweka Old Trafford hadi mwaka 2030.
Ingawa bado ni mchezaji muhimu wa United, Bayern inaendelea kumfuatilia kwa karibu, ikiamini ndiye anayefaa kuwa mrithi wa Harry Kane katika miaka ijayo.