Kadi nyekundu zaitega Man United EPL
Muktasari:
- Lakini, wakati kukiwa na malalamiko hayo, Manchester United inayoshika nafasi tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England huenda imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2023/24 iliposhika nafasi ya nne 2022/23.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa muda wa Manchester United, Michael Carrick ametoa lawama kali kwa mwamuzi wa kati Paul Tierney kumpa kati nyekundu beki wa kikosi hicho, Lisandro Martinez dhidi ya Leeds United akidai haikustahili, lakini akienda mbali na kusisitiza kwamba alienda Old Trafford akiwa na matokeo yake mfukoni.
Lakini, wakati kukiwa na malalamiko hayo, Manchester United inayoshika nafasi tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England huenda imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2023/24 iliposhika nafasi ya nne 2022/23.
Mashetani Wekundu walifuzu Ligi ya Mabingwa baada ya kuifumua Chelsea kwa mabao 4-1 katika mechi ya mwisho ya msimu huo chini ya Kocha Erik ten Hag, na tangu wakati huo haijawahi kutinga tena katika mashindano hayo, ukiondoa msimu juzi ilifuzu Europa League na kuzimwa na Tottenham Hotspur katika fainali.
Na sasa kikosi hicho kipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kikiwa na pointi 55 sawa na Aston Villa inayoshika nafasi ya nne zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, lakini alama tatu juu ya Liverpool inayoshika nafasi ya tano yenye 52 na 11 chini ya Man City ambayo ni ya pili.
Namba hizo zinaonyesha ugumu wa mambo ambao kikosi hicho kinakutana hao kikitoka kupoteza kwa mabao 2-1 kutoka kwa Leeds United nyumbani juzi, huku kikiwa kimeshawapoteza mabeki wake mahiri wa kati tegemeo Harry Maguire na Lisandro Martinez kwa kadi nyekundu wakikosa michezo miwili kila mmoja, ilhali Matthijs de Ligt akiwa majeruhi.
Kutokana na pengo hilo kubwa katika safu ya ulinzi linalokikabili kikosi hicho huenda likakiweka kwenye wakati mgumu kikosi hicho kupata matokeo mbele ya timu sita kinachokutana nazo kwenye mechi zilizosalia, huku vita ya kuwania nafasi za kushiriki mashindano ya Ulaya ikishika kasi na ile ya kushuka ikikolea.
Timu hiyo imebakiza mechi dhidi ya Chelsea na Liverpool zinazowania kufuzu mashindano ya Ulaya, na ambazo katika siku za karibuni zimekuwa na matokeo yasiyotabirika, huku ikitarajiwa kucheza na Brentford, Sunderland, Nottingham Forest na Brighton zilizo katika nafasi tofauti kwenye msimamo wa ligi hiyo.
MAGUIRE, MARTINEZ
Siku chache baada ya kusaini mkataba wa kuongeza mwaka mmoja katika kikosi hicho, Maguire alikumbana na rungu la Chama cha Soka England (FA), kusimamishwa mechi dhidi ya Leeds United baada ya kupewa kadi nyekundu kwa kufanya faulo ya makusudi dhidi ya Bournemouth.
Tayari adhabu hiyo imemalizika, lakini ikikiacha kikosi hicho na madhara ya kupoteza mchezo, huku beki hiyo akiwa anakabiliwa na shtaka jingine kutoka FA la utovu wa nidhamu ambalo linaweza kusababisha asimamishwe mechi kadhaa kufuatia tuhuma za utovu wa nidhamu, matumizi ya lugha isiyofaa dhidi ya mwamuzi wa nne baada ya kutolewa nje dakika ya 78 katika mchezo huo.
Kwa sasa mabeki wenye uhakika eneo la katikati Man United ni Leny Yoro na Ayden Heaven kwa mechi ijayo, vinginevyo mashtaka mengine ya Maguire yachelewe kusikilizwa.
Kwa upande wa Martinez, alionekana akivuta nywele za straika wa Leeds United, Dominic Calvert-Lewin, ambapo beki huyo wa kimataifa wa Argentina alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na sasa atakosa mechi tatu zijazo.
Ingawa tukio hilo limeibua mjadala ikiwemo madai kwamba beki huyo alistahili kadi ya njano au onyo kali, lakini uamuzi wa kumpa kadi nyekundu unatoa fursa ya kikosi chake kumkosa kwa nusu ya mechi zilizobaki za kikosi hicho kabla ya msimu kumalizika. Nje na hayo Leeds United iliyopata mabao yake mawili kupitia kwa Noah Okafor, imepata ushindi wake wa kwanza tangu 1981, huku bao la Manchester United likifungwa na kiungo Casemiro.
Akizungumzia matukio hayo, Carrick aliuita uamuzi uliosababisha kadi ya Martinez usiofaa na kwamba, ni miongoni mwa uamuzi mbaya zaidi aliowahi kuuona katika maisha yake ya soka, akidai: “Uamuzi huo ulikuwa wa kushtua kumtoa (Martinez). Hii ni mechi ya pili mfululizo tunaathiriwa na uamuzi kama huu, lakini hili ni moja ya matukio mabaya zaidi niliyowahi kuyaona.”
Kwa upande mwingine, mchambuzi na nahodha wa zamani wa United, Roy Keane, alidai kadi nyekundu dhidi ya Martinez ilikuwa adhabu kali, lakini Carrick anapaswa “kukubaliana na hali hiyo."
“Ni wazi ana hasira, lakini lazima ukubali. United hawakuanza vizuri mechi. Hili ni pigo kubwa. Uamuzi unaweza kuwa mkali, lakini uko ndani ya sheria za mchezo, na tumeshawahi kuona matukio kama haya.”
Calvert-Lewin alijitetea akisema: “Sisimamii sheria. Nilihisi nywele zangu zinavutwa nikamwambia refa, yeye ndiye anafanya uamuzi. Ni bahati mbaya kwake (Martinez), iwe alikusudia au la. Sina kinyongo.”
Kocha wa Leeds, Daniel Farke, alifurahishwa na kiwango cha timu yake licha ya presha ya dakika za mwisho baada ya Casemiro kufunga bao la kufutia machozi. “Kwa kweli tulipaswa kuwa mbele zaidi ya mabao 2-0 kipindi cha kwanza. Kadi nyekundu wakati mwingine hubadilisha mchezo. Tulilala kwenye mpira wa adhabu na ndipo United wakarudi kwenye mchezo. Lakini kushinda hapa kwa mara ya kwanza baada ya karibu miaka 40 ni jambo la ajabu na hatua kubwa mbele.”
ZILIZOBAKI MAN UTD EPL
-Aprili 18 vs Chelsea (ugenini)
-Aprili 27 vs Brentford (nyumbani)
Mei 3 vs Liverpool (nyumbani)
Mei 9 vs Sunderland (ugenini)
Mei 17 vs Nott'm Forest (nyumbani)
Mei 24 vsBrighton (ugenini)