Juventus yajitosa dili la Viktor Gyokeres, yaweka ofa mezani

Muktasari:
- Mabosi wa Juventus wameingia katikati ya vita na wana matumaini ya kuzipiku Arsenal na Manchester United zilizoripotiwa kuhitaji huduma ya fundi huyu wa kimataifa wa Sweden tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
JUVENTUS imemwekea mezani mshambuliaji wa Sporting, Viktor Gyokeres, ofa ya mshahara wa Pauni 11 milioni kwa mwaka, ili kumsajili katika dirisha hili.
Mabosi wa Juventus wameingia katikati ya vita na wana matumaini ya kuzipiku Arsenal na Manchester United zilizoripotiwa kuhitaji huduma ya fundi huyu wa kimataifa wa Sweden tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Fundi huyu mwenye umri wa miaka 27, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Mabosi wa Sporting wameshikilia msimamo wao wa kuhitaji Euro 100 milioni kama ada ya uhamisho ili kumuuza straika huyu licha ya ripoti za awali kudai walikuwa katika makubaliano na wawakilishi wa Gyokeres kwamba ataondoka kwa Pauni 67 milioni tu baada ya kukubali kubakia katika kikosi chao Januari mwaka huu licha ya ofa nono alizopokea.
Kyle Walker
BEKI wa Manchester City na timu ya taifa ya England, Kyle Walker, mwenye umri wa miaka 35, anaripotiwa kukubali kujiunga na Everton kwa mkataba wa mwaka mmoja katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Walker ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo AC Milan na mabosi wa Man City wamempa staa huyu ruhusa ya kuondoka kwa sababu hayupo katika mipango ya kocha wao Pep Guardiola kwa msimu ujao.
Bryan Mbeumo
MSHAMBULIAJI wa Brentford na timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo, mwenye umri wa miaka 25, ameonyesha nia zaidi ya kujiunga na Manchester United katika dirisha hili la majira ya kiangazi licha ya kuhusishwa na Tottenham Hotspur, ambayo inamtumia kocha wake wa zamani Thomas Frank kama sehemu ya ushawishi. Man United imekuwa ikiisaka saini ya nyota huyo huku Brentford ikijaribu kuweka ngumu lakini inaamini itampata.
Joao Pedro
NEWCASTLE United wameanza mazungumzo na Brighton kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Brazil, Joao Pedro, mwenye umri wa miaka 22, katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Mbali ya Joao, ripoti zinaeleza kuwa Newcastle inahitaji pia saini ya beki wa kati wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Ivory Coast, Ousmane Diomande, mwenye umri wa miaka 21.
Nico Williams
BARCELONA wamewapiku Arsenal, Bayern Munich na Chelsea katika kinyang’anyiro cha kumsajili winga wa Athletic Bilbao, Nico Williªms, mwenye umri wa miaka 22, katika dirisha hili baada ya staa huyo kufanya nao makubaliano binafsi. Licha ya mchezaji mwenyewe kukubali kujiunga nao, ripoti zinaeleza Barcelona inashindwa kukamilisha dili hilo kutokana na matatizo ya kifedha.
Hugo Ekitike
MANCHESTER United wamefanya mazungumzo ya awali na Eintracht Frankfurt kuhusu kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Ufaransa, Hugo Ekitike, mwenye umri wa miaka 22, lakini bado hawaja wasilisha ofa rasmi kwa timu hiyo kwa ajili yake. Ekitike ameingia katika rada za Man United inayomhitaji kwa ajili ya kuboresha safu yao ya ushambuliaji.
Alejandro Garnacho
Napoli imewaweka katika rada zao mastaa wawili kutoka Ligi Kuu England, winga wa Manchester United na Argentina, Alejandro Garnacho, mwenye umri wa miaka 20, pamoja na kiungo wa Manchester City na England, Jack Grealish, mwenye umri wa miaka 29. Ripoti zinadai Napoli imeandaa kiasi cha Euro 40 milioni kwa kila mmoja wao.
Darwin Nunez
AC Milan na Napoli wote wanahitaji huduma ya mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay, Darwin Nunez katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Ripoti zinadai Liverpool ipo tayari kumyuza staa huyu lakini kwa timu itakayokuwa tayari kulipa kiasi kisichopungua pauni 51 milioni.