Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jude Bellingham aizamisha Juventus Bernabéu

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza tangu Aprili 1, 2025, Jude Bellingham alisimama tena mbele ya jukwaa la kusini akiwa ameinua mikono yake, akisikiliza mashabiki wa Real Madrid wakiimba kwa furaha.

MADRID, HISPANIA: Haikuwa mechi ya kuvutia sana, lakini nyimbo zilizotokea Santiago Bernabéu zilikuwa na ladha ya kipekee. Ilikuwa muda mrefu tangu mashabiki wa Real Madrid wapate nafasi ya kuimba “Hey Jude”, na walikuwa wameikosa nafasi hiyo.

Kwa mara ya kwanza tangu Aprili 1, 2025, Jude Bellingham alisimama tena mbele ya jukwaa la kusini akiwa ameinua mikono yake, akisikiliza mashabiki wa Real Madrid wakiimba kwa furaha.

Kiungo huyo baada ya kuuguza jeraha la bega na kuzua wasiwasi kuhusu nafasi yake uwanjani, hatimaye alifunga bao lake la kwanza msimu huu, lililowapa Real Madrid ushindi wa 1–0 dhidi ya Juventus, usiku wa Oktoba 22, 2025.

“Tumelazimika kutokwa jasho,” amesema kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois.

Courtois alijua hilo vizuri zaidi kuliko mtu yeyote, kwani aliokoa kwa ustadi shambulizi la uso kwa uso kutoka kwa Dusan Vlahovic, kisha kuzuia mkwaju mwingine muhimu kutoka kwa Khéphren Thuram dakika ya mwisho kabisa, hivyo kuiacha Madrid ikiwa na alama tisa huku kikosi cha Igor Tudor kikiwa chini ya mstari wa kufuzu katika hatua hii.

“Wataliano wanapokuwa taabani, huwa hatari mara mbili,” amesema Xabi Alonso.

Ukweli ni kwamba, Juventus ambao hawakuwa wameshinda tangu Septemba 2025, waliisumbua Madrid mwanzoni na tena mwishoni mwa mchezo. Madrid walitawala mpira kwa 66% dhidi ya 34%, lakini Juventus walikuwa hatari katika mipira ya kushambulia kwa kasi, hasa kupitia Pierre Kalulu na ushirikiano wa Vlahovic, wakipiga jumla ya mashuti 12 dhidi ya 27 ya wenyeji.

Juventus walianza vizuri. Baada ya dakika tatu tu, walidhani wamepata nafasi ya kufunga, lakini Vlahovic alionekana kuwa amemvuta Éder Militão, ikawa faulo.

Dakika tatu baadaye, Raúl Asencio alilazimika kujitupa mbele ya Vlahovic baada ya Kalulu kukimbia vizuri upande wa kulia. Dakika tatu baadaye tena, shuti la Weston McKennie lilitolewa na Courtois.

Dakika 15 zilipofika, Courtois aliokoa vizuri shuti la Federico Gatti. Baada ya hapo, Juventus walipoteza kasi yao, na Madrid wakaanza kutawala mchezo ingawa haukuwa wa kuvutia sana. 

Nafasi bora zaidi zilikuja kwa Aurélien Tchouaméni, ambaye alikosa kwa kichwa mara mbili na mpira mwingine ukatoka pembeni. Militão naye alipoteza nafasi ya kichwa.

Kylian Mbappé hakuonekana sana awali, lakini aliposhika mpira, Madrid walikuwa karibu kufunga. Kwanza, shuti lake liliokolewa na kipa Michele Di Gregorio, ambaye aliokoa jumla ya mipira minane. Kisha Mbappé alionyesha upambanaji akimzungusha Andrea Cambiaso mara mbili kabla ya kuangushwa na kumpasia Militão ambaye alipiga juu ya lango.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Militão alizuia shambulio la Kalulu, kisha Courtois akaokoa mkwaju wa hatari wa Vlahovic ambaye alikuwa amepenya akiwa peke yake baada ya Lloyd Kelly kupiga pasi iliyokatwa vibaya.

Baada ya kuokoa, lilifuata bao la Madrid. Vinícius Júnior alitengeneza nafasi, akipenya kati ya mabeki wanne na kupiga shuti la mguu wa kushoto lililogonga mwamba. Bellingham, aliyekuwa akicheza kama mshambuliaji wa kati, alimalizia kwa kuuweka mpira wavuni.

Madrid walipaswa kuongeza bao zaidi, lakini Mbappé akazuiwa tena na Di Gregorio, kisha shuti la Valverde likazuiwa na Gatti. Di Gregorio baadaye aliokoa mara mbili dhidi ya Mbappé na Brahim Díaz.

Juventus nao walipata nafasi mwishoni, Raúl Asencio alimzuia Loïs Openda ambaye alikuwa amebaki peke yake, kabla ya Courtois kuokoa mpira wa Thuram sekunde za mwisho.

“Ni hisia nzuri sana. Imepita muda mrefu tangu nifunge, muda mrefu nikiwa nje nikitamani wakati kama huu. Kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa na kufunga dhidi ya timu kubwa kama Juventus, tena nyumbani ni kitu cha ajabu. Nilihisi vizuri uwanjani, na kufunga bao la ushindi ni jambo muhimu sana kwa timu,” amesema Bellingham.