Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Joao Pedro atoa laana ya namba 9 Chelsea

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo wa Brazil alifunga bao kwa ustadi baada ya kuutengeza mpira juu ya kipa wa Fulham, Bernd Leno na kuiongoza Chelsea kuanza safari ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Fulham kwenye Uwanja wa Craven Cottage, katika mchezo wa kwanza wa kocha Xabi Alonso akiwa kwenye benchi la timu hiyo.

LONDON, England. MSHAMBULIAJI Joao Pedro alihitaji sekunde 31 tu kuonyesha kuwa hana hofu na kile kinachoitwa ‘laana ya jezi namba tisa’ katika klabu ya Chelsea.

Mshambuliaji huyo wa Brazil alifunga bao kwa ustadi baada ya kuutengeza mpira juu ya kipa wa Fulham, Bernd Leno na kuiongoza Chelsea kuanza safari ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Fulham kwenye Uwanja wa Craven Cottage, katika mchezo wa kwanza wa kocha Xabi Alonso akiwa kwenye benchi la timu hiyo.

Ilikuwa wikiendi ya kipekee kwa Joao Pedro, ambaye alikabidhiwa jezi namba tisa na pia kupewa mkataba mpya wenye maslahi bora ya kifedha, utakaomuweka Stamford Bridge hadi mwaka 2034.

Ingawa inaweza kuonekana kama imani isiyo na msingi, sehemu ya mashabiki wa Chelsea inaamini kwamba kuna ‘laana’ inayohusishwa na jezi hiyo.

Tangu mshambuliaji wa zamani wa Uholanzi, Jimmy Floyd Hasselbaink, aondoke Chelsea mwaka 2004, hakuna mshambuliaji aliyevaa namba tisa aliyekuwa na kiwango cha juu cha ufungaji kwa muda mrefu.

Didier Drogba alitumia jezi namba 11 katika kipindi chake cha mafanikio Stamford Bridge, wakati Diego Costa alivaa namba 19. Hata hivyo, washambuliaji waliokuja baadaye kama Romelu Lukaku, Alvaro Morata, Gonzalo Higuain, Radamel Falcao na Pierre-Emerick Aubameyang walipata wakati mgumu walipovaa namba tisa.

Wote walidumu kwa vipindi vifupi na vilivyojaa changamoto katika klabu hiyo.

Mchezaji wa mwisho kuvaa jezi hiyo kabla ya Joao Pedro alikuwa Liam Delap, ambaye kwa sasa yuko kwenye mazungumzo na Nottingham Forest kuhusu kuondoka Stamford Bridge baada ya kufunga bao moja pekee katika Ligi Kuu msimu uliopita.

Hata hivyo, si washambuliaji pekee waliowahi kuvaa jezi hiyo. Kiungo Steve Sidwell na beki Khalid Boulahrouz pia waliwahi kuitumia, ingawa baadhi ya mashabiki wanaweza kusema Tammy Abraham alifanya vizuri akiwa namba tisa kabla ya kuhamia Roma.

Akizungumza kuhusu suala la ‘laana’ hiyo baada ya kufunga dhidi ya Fulham, Joao Pedro alisema haamini kuwa namba inaweza kuamua kiwango cha presha anachokabiliana nacho.

“Siingi katika imani hiyo. Sidhani kama namba inaweza kuamua presha hii,” alisema Joao Pedro.

Msimu uliopita, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alifunga mabao 20 katika mashindano yote, akifikisha idadi hiyo inayolingana na namba ya jezi yake.

Alikuwa mshambuliaji wa kwanza wa Chelsea kufikisha mabao 20 kwa msimu mmoja tangu Diego Costa afanye hivyo miaka tisa iliyopita.

Kiwango hicho kimeifanya Chelsea kujivunia zaidi uamuzi wa kumsajili kwa Pauni55 milioni, pamoja na Pauni 5milioni za nyongeza, katika makubaliano waliyofikia na Brighton msimu uliopita.

Watu wa karibu na Joao Pedro pia wanaamini anastahili kupewa jukumu hilo, huku wasiwasi wa kushindwa kumudu presha ukiwa haupo kwenye kambi yake.

Kwa mujibu wa watu wake wa karibu, kikosi chake cha wasaidizi kimekuwa sehemu ya safari yake ya kupanda hadi kufikia kiwango cha juu na kinaamini ana uwezo wa kubeba jukumu la kuwa kinara wa Chelsea.