Huyu ndo Sasha, aliyeuteka moyo wa Grealish
Muktasari:
- Grealish na Sasha, ambao wote wanatokea Birmingham nchini England, tayari wamejaliwa mtoto mmoja ingawa bado hawajafunga ndoa. Hata hivyo, bado ni moja ya 'kapo' za mastaa wa soka zinazofuatiliwa sana mitandaoni.
WINGA wa Manchester City anayekipiga Everton kwa mkopo, Jack Grealish, kwa miaka zaidi ya 12 amekuwa katika uhusiano na mpenzi wake, Sasha Attwood, ambaye shughuli zake ni urembo na mitindo.
Grealish na Sasha, ambao wote wanatokea Birmingham nchini England, tayari wamejaliwa mtoto mmoja ingawa bado hawajafunga ndoa. Hata hivyo, bado ni moja ya 'kapo' za mastaa wa soka zinazofuatiliwa sana mitandaoni.
Kwa mujibu wa The Irish Mirror, wawili hao walianza uhusiano wakiwa na umri wa miaka 16, ingawa uhusiano wao umewahi kupitia hali ya kuachana na kurudiana kwa miaka kadhaa.
Walikutana kipindi wakiwa wanasoma katika shule ya St Peter’s Roman Catholic Secondary School iliyopo Solihull, West Midlands, huko England, wakati huo Grealish akiichezea timu ya vijana ya Aston Villa.
Hata alipopandishwa timu ya wakubwa na kuanza kucheza Ligi Kuu England (EPL), bado waliendelea kuwa pamoja hadi pale Grealish alipokuja kupata mafanikio akiwa na Man City, ambapo alishinda mataji mengi makubwa, likiwemo la UEFA.
Sasha ni mwanamitindo na mtu mwenye ushawishi katika mitandao ya kijamii (influencer), ambapo Instagram ana wafuasi zaidi ya 300,000. Mara nyingi hutumia mtandao huo kutangaza bidhaa zake za urembo pamoja na kutoa elimu kuhusu masuala ya urembo.
Akiwa na umri wa miaka 13 ndipo kipaji chake kiligunduliwa na wakala wa mitindo ambaye alikutana naye akiwa pamoja na mama yake katika duka moja mjini Birmingham.
Sasha, akiwa kama mwanamitindo, amewahi kufanya kampeni na matangazo ya bidhaa za kampuni mbalimbali za urembo na mitindo, ikiwemo Boohoo, L’Oreal, Lipsy, Lounge Underwear na GHD.
Mnamo Agosti 2024, Sasha alisaini mkataba mnono na kampuni ya Pretty Little Thing kwa ajili ya kutangaza mavazi ya wajawazito. Hivyo, mrembo huyo ana biashara zake mbali na kujulikana kama mpenzi wa mchezaji maarufu, Grealish.
Ukurasa wake wa Instagram na hata chaneli yake ya YouTube kumejaa maudhui ya kazi zake za urembo, si mtu wa kuanika sana maisha yake ya kimahusiano mtandaoni kama baadhi ya wapenzi wa mastaa wengine.
Mnamo Desemba 2023, familia yao ilipata taharuki kubwa baada ya majambazi kuvamia nyumba yao usiku wakati walipokuwa wakitazama live mechi kati ya Man City dhidi ya Everton.
Sasha, wazazi wa Grealish, bibi yake, dada zake wawili na kaka yake ndio waliokuwepo nyumbani wakati huo wa uvamizi.
Polisi walifika kwenye nyumba yao huku kukiwa na hofu kwamba huenda kulikuwa na tukio la utekaji. Hata hivyo, kundi hilo la wezi lilifanikiwa kutoroka likiwa limeiba saa na vito vya thamani vilivyokadiriwa kuwa na thamani ya Pauni 1 milioni.
“Wezi waliliiba saa nyingi na vito vya thamani. Walitekeleza uvamizi huo wakati Manchester City inacheza, kwa hiyo familia yote ilikuwa sehemu moja kutazama mechi hiyo kama sehemu ya kumuunga mkono Grealish,” chanzo kimoja kiliiambia The Sun.
Iliripotiwa kuwa nyumba hiyo ni kubwa sana, hivyo ilikuwa ni vigumu kwao kugundua uvamizi huo kwa haraka, ila baada ya kusikia kengele ya usalama pamoja na kelele za mbwa, ndipo wakapiga simu polisi. Hakuna mtu aliyejeruhiwa, lakini tukio hilo lilisababisha hofu kwao.
Baada ya kuachwa katika kikosi cha England kwa ajili ya michuano ya Euro 2024, Grealish alitumia muda huo kupumzika pamoja na mpenzi wake Sasha, lakini kubwa zaidi ndipo walitangaza kuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza.
Sasha aliposti Instagram picha za ujauzito wake na kuandika; Nusu yangu, nusu yako - tumebarikiwa zaidi ya tunavyoweza kueleza.
Hatimaye, wawili hao walijaliwa kupata mtoto wao wa kwanza Septemba 27, 2024, mtoto huyo wa kike walimpa jina la Rose Grealish. Walitangaza kuzaliwa kwake Oktoba 7 kupitia Instagram kwa kuposti picha yake ambayo inamuonyesha akiwa ameshikilia kidole cha mmoja wa wazazi wake.
Baadhi ya wachezaji wenzake Grealish na waliowahi kucheza naye walimpongeza, baadhi yao ni Marcus Rashford, Declan Rice, Alex Zinchenko na Ross Barkley.
Kwa upande wake, Sasha aliposti picha hiyo ya mtoto wake na kuandika; 27/09/24 Mila Rose Grealish. Huu ndio wakati wa kipekee zaidi katika maisha yangu.
Wakati Grealish anasaini mkataba wa kujiunga na Everton, Sasha naye alikuwepo pamoja na mtoto wao, Mila Rose, ambaye alivaa jezi ya klabu hiyo. Huu ni uthibitisho kuwa mchezaji huyo amekuwa akiungwa mkono na familia yake kwa kila hatua anayopiga katika safari yake ya soka.